1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwa
mujibu wa kanuni ya 99(9) ya Kanuni za kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2013
naomba kuwasilisha maoni ya kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya
wizara ya ujenzi kwa mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, kwa
unyenyekevu mkubwa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu na uwezo wa
kusimama mbele ya Bunge lako tukufu kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya
Upinzani kwa sekta nzima ya ujenzi. Sekta ambayo kibajeti inachukua asilimia
kubwa ya bajeti lakini kihalisia nisekta yenye madeni makubwa sana toka kwa
wakandarasi na washauri.
Mheshimiwa Spika,
nichukue fursa hii kuwapongeza viongozi wetu wakuu wa vyama vinavyounda
ushirikiano wa UKAWA kwa kusikiliza kilio cha miaka mingi ya wananchi juu ya
kuunganisha nguvu ili kuiondoa Serikali ya CCM ambayo imeondoka kwenye misingi
yake ya awali ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi na kuwa chama cha
kukumbatia wala rushwa, mafisadi na mabwanyeye
na wahujumu wakubwa wa rasilimali za watanzania.
Mheshimiwa Spika,kwa
umuhimu wa kipekee ni kwapongeza wananchi wa Jimbo la Muhambwe kwa ushirikiano
wanaonipatia katika kuhakikisha ninafanya vyema kazi yangu ya uwakilishi niwapo
nje na ndani ya Bunge. Nasema asanteni sana, na ninasema sasa Daftari la Kudumu
la Wapiga kura linaloendelea Kigoma, tuhamasishane kuhakikisha kila mwenye sifa
anajiandikisha kwani hilo ndilo litaondoa utawala wa Serikali ya CCM uliolewa
madaraka kwa kudhani kuwa watanzania wana macho lakini hawaoni matendo maovu
yanayofanywa na wanachama na watendaji
wao.
Mheshimiwa Spika, Wizara
ya Ujenzi, kutokana na muundo wake wa kiutawala, ina majukumu yafuatayo:
kusimamia sekta ya ujenzi ambayo inajumuisha Barabara Kuu na Barabara za Mikoa,
Vivuko, Nyumba na Majengo ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Aidha,
Wizara ina jukumu la kusimamia Taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta ya
Ujenzi, taasisi hizo ni pamoja na wakala wa Barabara, wakala wa majengo ya
Serikali, wakala wa ufundi umeme, bodi ya mfuko wa barabara, baraza la taifa la
ujenzi, bodi ya usajili makandarasi, bodi ya usajili wa wahandisi, bodi ya
usajili wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi. Pia wizara inasimamia chuo
cha ujenzi Morogoro na chuo cha Matumizi stahiki ya nguvukazi.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kutoa utangulizo huo sasa, hotuba yetu itajikita zaidi katika maeneo
ambayo tunaona bado yana matatizo makubwa.
2. MADENI
MAKUBWA YA WAKANDARASI
Mheshimiwa Spika,katika mawasilisho ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha
Bungeni aliliambia Bunge lako tukufu kwamba kulikuwa na kikosi kazi cha
kuhakiki madeni ambayo wizara mbalimbali zinadaiwa na wazabuni. Moja ya Wizara
ambazo zinadaiwa na wazabuni na wakandarasi ni wizara hii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa
Waziri wa Ujenzi alieleze Bunge kwamba, kile kikosi kazi kilichoundwa na Wizara
ya fedha ili kuhakiki uhalali wa madeni ya wizara yake.Kimebaini Wizara ya
ujenzi inadaiwa kiasi gani na Wakandarasi pamoja na Wazabuni wengine?
Mheshimiwa Spika,Wizara ya ujenzi ni wizara ambayo imekuwa
ikitengewa fedha nyingi za miradi ya maendeleo
katika bajeti kuliko wizara zingine. Kwa mwaka wa fedha 2011/12 zilitengwa
shilingi 1,155,976,936,000/-, Je madeni yalikuwa ni kiasi gani na fedha za
zilizoenda kwenye ujenzi zilikuwa ni kiasi gani?Mwaka 2012/13 zilitengwa
shilingi 693,948,272,000/-, Je, madeni ya wakandarasi nawashauri yalikuwa kiasi
gani na fedha zilizoelekezwa kwenye ujenzi zilikuwa ni kiasi gani?Mwaka 2013/14
fedha zilizotengwa ni shilingi 845,225,979,000/- Je madeni ya wakandarasi na
washauri yalikuwa ni kiasi gani na fedha zilizoelekezwa kwenye ujenzi zilikuwa
ni kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imetaka kuelewa madeni yaliyokuwa inadaiwa
Wizara ili kuona kweli kilometa za Barabara anazosema Mhe Dr. Magufuli John
Pombe ni halisia au ni ngonjera tu?
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, wizara ya
ujenzi imetengewa jumla ya shilling bilioni 662,234,027,000.00 kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo. Hadi kufikia Januari, 2014 madeni ya
makandarasi na washauri yalikua ni shilingi bilioni 663,870,970,636.26
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi mpaka sasa inadaiwa zaidi ya
Billion 800 na hakuna majibu juu ya ulipwaji wa madei hayo. Licha ya
uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara hii kuwa na kelele na mbwembwe nyingi ukweli
ni kwamba madeni ya Wizara yanazidi fedha za maendeleo tunazaopitisha na Bunge
lako Tukufu. Mfano mzuri ni Bajeti ya
2014/2015 Wizara ilikuwa na madeni yaliyofikia shilingi Billioni 760. Huku
bajeti ya maendeleo kwa wizara na taasisi zake ikiwa ni bilioni 762. Ni dhahiri
kabisa kuwa Wizara hii haikuwa na fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha
2014/2015.
Hivyo
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri kulieleza ukweli Bunge lako tukufu
kwamba kwenye Bajeti ya 2014/2015 ni
fedha kiasi gani zimelipa madeni na fedha kiasi gani zimekwenda kwenye miradi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika,kwa upande mwingine Kambi Rasmi ya Upinzani
inamtaka Waziri kuacha mbwembwe nyingi bali aeleze kuwa madeni hayo ya Billioni
zaidi ya 800 yanatoka kwenye barabara zipi? Yatalipwaje? Na riba ni kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, hata kwamwaka huu wa fedha, Bajaeti ya maendeleo ni Billion
890,572,000.00 kwa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hukumadeni yakiwa
zaidi ya Bilioni 800. Hivyo hakuna
uhalisia kati ya fedha za maendeleo zinazoombwa na madeni husika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatakuelewa kwa undani suala hili, kutokana
na kilio kilichotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakandarasi
(CRB) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Contractors Association of Tanzania(CAT),
Mhandisi Bi.Consolata Ngimbwa kwenye
Mkutano wa Mashauriano na Maonyesho uliofanyika tarehe 14 MEI,2015 kwenye
ukumbi wa Mlimani City.
Mheshimiwa Spika, Kwa uchungu mkubwa Mhandisi huyo aliueleza umma kwamba wakandarasi
watatu wamekufa kutokana na msongo wa kudaiwa na watu waliokuwa wanatoa huduma
katika Kampuni zao, hii ni kutokana na Serikali kutowalipa madeni yao pale wanapomaliza
kazi. Hii ni hasara kubwa kupoteza waandisi ambao tunaamini kama taifa bado
tunauhitaji mkubwa wa watu hao.
3. AHADI
ZA UONGO ZA CCM KATIKA UTENGENEZAJI WA BARABARA
Mheshimiwa Spika, kila inapofika mwaka wa uchaguzi CCM imekuwa
ikiahidi kujenga barabara kwa lengo la kupata kura tu, lakini haitimizi ujenzi wa barabara walizoahidi.
Mifano ya
Barabara ambazo Serikali ya CCM iliahidi kwenye
ilani yake na nyingine akaahidi
Mgombea wa Urais na hazijajengwa ni pamoja na:-
1. Barabara ya
Nyakanazi, Kibondo, Kasulu kidahwe Km 310 hii ni ahadi ya Serikali ya awamu ya
Tatu naya awamu ya nne hivyo wananchi wa Nyakanazi, Kakonko, Kibondo, Kasulu na
Kigoma kwa ujumla n,k hatupaswi kuchagua CCM kwa kuwa imeahidi uongo zaidi ya miaka 20.
2. Barabara ya Karatu – Mang’ola – Matala, barabara
hii iliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami lakini mpaka sasa haijajengwa
hivyo CCM iliahidi 2010 uongo na wananchi wanaendelea kula vumbi tu.
3. Barabara ya Karatu – Mbulu KM 77 iliahidiwa 2010
kwenye ilani ya CCM lakini. Barabara hii nayo iliahidiwa kujengwa kwa kiwango
cha lami mpaka sasa wananhi wanaendelea kula vumbi tu.
4. Aidha katika ukurasa wa 76 wa ilani ya CCM,
iliahidi uongo kujenga barabara ya
Arusha – Moshi – Himo – Holili KM 140 mpaka sasa ni vumbi tubado haijajengwa.
5. Barabara ya Bunda – Kisorya – Nansio KM 93. Hii nayo iliahidiwa nabado jaijajengwa hata
KM 1. Tazama ukurasa wa 74 wa ilani ya
CCM 2010.
6. Barabara kilombelo – Ifakara – Mahenge bado
haijajengwa wakati ni ahadi ya kutafuta kura za Morogoro.
7. Barabara ya Mpemba - Isongole yenye urefu wa km
51.5 haijajengwa ni ahadi katika Ilani yenu, hivyo wananchi wa Ileje mjihadhari
na uongo wa CCM.
8. Kolandoto –Meatu-Mto Sibiti-Singida nayo
haijajengwa kama ilivyoahidiwa, hata upembuzi yakinifu bado haujafanyika, na
barabara nyingine nyingi hiyo ni mifano michache tu.
Aidha zipo
ahadi mbalimbali za uongo zilizotolewa na Rais Kikwete mpaka sasa hazijajengwa katika
miji midogo mbalimbali nchini . Mifano
ya Ahadi za kutafutia kura na hazijatekelezwa ni pamoja na:-
1. Ujenzi wa KM 2 mjini Karatu
2. Ujenzi wa KM 1 ½
Kibondo Mjini
3. Ujenzi wa lami mjini kondoa na Mbunge wake amekua
akilia kila siku hapa Bungeni, na ahadi nyingine lukuki hiyo ni mifano tu.
Mheshimiwa
Spika, pia yapo madaraja
mbalimbali yaliyoahidiwa kwa mbwembwe nyingi kwa lengo la kutafuta kula tu lakini hayajajengwa mpaka sasa mfano wa
madaraja hayo ni daraja la mto sibiti ambalo mwaka 2014/15 ilitengewa shilingi
bilioni 3 lakini fedha hizo hazikutolewa na Hazina. Mwaka huu wa fedha Wizara
haijatenga chochote kuhusiana na daraja hilo na Mkandaraji ameondoka site.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka ufafanuzi juu ya
daraja hili.
Mheshimiwa
Spika,daraja lingine nidaraja
la Kigamboni, ambapo Rais Kikwete aliahidi mwaka jana alipotembelea ujenzi wa
daraja hilo kwamba litakamilika mwezi wa sita mwaka huu, kwa hali ilivyo
inaonesha kuwa ahadi hiyo haitekelezeki.
4. UNUNUZI
WA KIVUKO CHA DAR – BAGAMOYO
Mheshimiwa Spika, kivuko hiki, kimenunuliwa kwa takribani Bilion nane fedha za
kitanzania, kivuko hiki kinabeba abiria 300 na pia kinatumia masaa matatu
kutoka Dar kwenda Bagamoyo.
Mheshimiwa Spika,ni jambo la ajabu kununua kivuko chakizamani au
chakavu chenye spidi ndogo. Azam Bakhresa ana Meli inayotoka Dar kwenda
Zanzibar kwa muda wa dakika 90 tu na kinabeba abiria 500 na kwa taarifa tulizonazo
kinauzwa kati ya Bilioni 4 na Bilioni 5 tu.
Kambi Rasmi
ya Upinzni Bungeni inaombaBunge lako kuunda Tume kwenda kuchunguza ununuzi wa
kivuko hiki kibovu na cha kizamani kilichonunuliwa kwa bei kubwa huku kwa siku
kikiweza kwenda Dar es Salaam mara moja tu na kurudi Bagamoyo mara moja tu,
Aidha kivuko hiki kimekosa abiria kwani wananchi wanaona bora kupanda daladala
kuliko kupanda kivuko kinchotumia masaa matatu.
Hivyo
mbwembe na kelele za Magufuli kwamba watanunua meli kusaidi kupunguza foleni
zimegonga mwamba kwa kununua kivuko kibovu na cha kizamani kinachokosa abiria.
5. UANDISHI
WA HOTUBA ZA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI KUANDIKWA KISANII
Mheshimiwa Spika, Wizara ya ujenzi imekuwa ikiandika hotuba
ndefu kuwachanganya Wabunge. Wizara hii inaandika barabara zilizojengwa
miaka ya 80 na miaka ya 90 kama vile zimejengwa hivi karibuni.
Aidha
Wizara hii haina ufafanuzi unaoridhisha juu ya fedha zinazotengwa na KM
zinazojengwa, mfano ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam = Chalinze – Morogoro
KM 200, Sehemu ya Dar es S alaam Chalinze imetengewe Billion 2.45. Lakini hakuna ufafanuzi kwani kilometa 100
haziwezi kujengwa kwa Billioni mbili tu.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Dr. Waziri alieleze Bunge hili tukufu, hizo
fedha zilizotengwa shilingi bilioni 2.45 kwa ajili ya kujenga kipande cha Dar
es Salaam hadi Chalinze zitajenga kilometa ngapi kati ya hizo kilometa 100 anazotuambia?
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Usagara – Geita – Kyamyorwa KM 424 sehemu ya Uyovu –
Bwanga – Biharamulo KM 112 imetengewa Billioni 4.97 lakini hakuna ufafanuzi
fedha hizo zinakwenda kujenga KM ngapi kati ya KM 424?
Mheshimiwa Spika, Barabara ya IBANDA-ITUNGI/KAJUNJUMELE-KIWIRA
PORT (KM 26): Shilingi Milioni 405 kwa
mwaka wa fedha 2015/16 lengo la Serikali ni kufanya ukarabati wa barabara hiyo
kwa kiwango cha lami. Hoja hapa ni je kilometa hizo 26 ukarabati huo utakuwa ni
wa aina gani?
Mheshimiwa Spika, barabara ya NZEGA-TABORA (KM 114.7): shilingi
milioni 5,336 au shilingibilioni 5.336 kati ya hizo shilingi bilioni 2.623 ni
kulipa deni la Mkandarasi kwa sehemu ya Puge –Tabora –KM 56.1 na KM 58.6
Nzega-Puge ujenzi bado unaendelea na zimetengwa shilingi bilioni 2.713. Je,
fedha hizi zilizooneshwa hapa ni kulipa deni la huyo mkandarasi anayejenga
Nzega-Puge ni kiasi gani? Na zinabakia kiasi gani kwa ajili ya ujenzi wa hizo
Kilometa?
Mheshimiwa Spika, barabara ya SUMBAWANGA-MPANDA-KIDAHWE (KM 438):
shilingi milioni 11,692,000/- lengo ni kujenga barabara hii kwa kiwango cha
lami kwa mwaka wa fedha 2015/16. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.586
fedha za ndani ni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa sehemu ya
Sumbawanga-Kanazi, shilingi bilioni 3.586 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa
sehemu ya Kanazi-Kizi-Kibaoni.Shilingi bilioni 2.681 kwa ajili ya ujenzi wa
sehemu ya Kizi-Sitalike-Mpanda. Je, hapa madeni ni kiasi gani na fedha halisi
za ujenzi ni kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, kwa eneo jipya la Kizi-Sitalike-Mpanda ni
kilometa ngapi na kiasi hicho cha shilingi bilioni 2.681 kazi gani zinakwenda
kufanyika?
Mheshimiwa Spika,kiasi cha shilingi bilioni 1.839 kwa ajili ya
kuendelea na ujenzi wa sehemu ya Mpanda-Mishamo kilometa 100. Kama tulivyohoji
hapo awali fedha hizi fedha kiasi gani nikulipa wakandarasi waliokuwa
wamesimamisha ujenzi (madeni) na ni kiasi gani kwa ajili ya ujenzi?
Mheshimiwa Spika, waheshimiwa wabunge tutaweza kuelewa vyema mahesabu ya Mheshimiwa
Dr.Magufuli John Pombe, pale tutakapoelewa ni kiasi gani cha fedha kinajenga
kilometa moja ya barabara kwa kiwango cha lami. Hivyo tunamtaka alieleze Bunge
lako tukufu ni Shilingi ngapi zinajenga kilometa moja ya barabara kwa kiwango
cha lami? Kinyume cha hapo ni kupeana matumaini yasiyokuwepo katika uhalisia
kwa maeneo husika.
6. BARABARA
ZILIZOJENGWA NI CHINI YA KIWANGO
Mheshimiwa
Spika, licha ya kwamba
Wizara na hata Waziri Mkuu wanajigamba kujenga KM 13,000 za lami katika awamu
ya nne ambacho ni kiwango kidogo sana ikilinganishwa na zaidi ya kilometa 86000
zinazopaswa kujengwa kwa lami. Kambi Rasmi ya Upinzani inaelewa vizuri mtandao
wa Barabara ni kutoka Dar es Salaam hadi Kagera, Dar es Salaam hadi Kigoma, Dar
es Salaam hadi Songea, Dar es Salaam hadi Tunduma Dar es Salaam hadi Masasi n.k.Mitandao
yote hiyo wakati Serikali ya Mkapa inamaliza muda wake barabara hizo zilikuwa
za lami na zingine zilikuwa zimebakiza vipande vichache vya kuunganishwa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inamtaka Mhe Dr. Magufuli John Jombe alieleze Bunge hizo kilometa
13,000 wanazosema kuwa Serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete imezijenga. Ziko
wapi?, azitaje hizo barabara, urefu wa kila moja?na zina hali gani kwa sasa,
wakati atakapohitimisha hoja yake.
Mheshimiwa
Spika,hata hizo barabara
ambazo zinasemwa,zimejengwa chini ya viwango na zinabomoka na kuharibika miezi sita au pungufu au mwaka
mmoja baada ya matengenezo. Hii
inaonesha kuna rushwa na parcent katika ujenzi wa Barabara za lami. Mifano ya
barabara zilizojengwana kubomoka kwa muda mfupi ni:-
1. Barabara ya Dar es Salaam hadi Dodoma hii
imebonyea upande wa kushoto na inatengenezwa kila wakati lakini inaharibika.
2. Barabara yaBagamoyo Msata imeanza kuharibika hata kabla
haijakabidhiwa.
3. Barabara ya Dodoma Iringa nayo imejaa mashimo
kwenye maeneo kadhaa, maana yake ni kwamba imejengwa chini ya kiwango.
4. Barabara ya Dodoma- Mwanza hasa maeneo ya mlima wa
Sekenke ilibomoka muda mfupi mara tu ya kukabidhiwa Serikalini
Mheshimiwa
Spika, hoja hii ya barabara
kujengwa chini ya kiwango imepata nguvu zaidi kutokana na majibu ya Mhe.Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi alipolieleza Bunge kuwa kuongezeko kwa ajali za
barabarani kunachangiwa na ubovu wa miundombinu kwa asilimia 7 katika ajali
zote za barabarani. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza hivi barabara zilizojengwa
chini ya viwango mnazipokea je kutoka kwa wakandarasi?
7. BARABARA
MBOVU KATIKA MIJI YETU
Mheshimiwa
Spika, ifahamike kwamba jiji
la Dar es Salaam halina planning na mara ya mwisho limepimwa mwaka 1979.
Kutokana na Serikali ya CCM kushindwa kuwa na mipangoya muda mrefu hali inazidi
kuwa tete katika jiji la Dar es Salaam.
Ikumbukwe kwamba kama Wizara ya Ardhi haiwezi kupima maeneo ya Miji na
kufahamu barabara zitapita wapi ni dhahiri,kwamba ujenzi wa barabara utakuwa
mgumu sana.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani
inazidi kutupa lawama kwa Serikali hii ya CCM kujenga Daraja la Jangwani kwa
mabilioni ya shilingi lakinimvua zilizonyesha hivi karibuni zimepelekeamaji kupita
juu ya daraja hilo na hivyo njia hiyo kufungwa kwa muda. Aidha ujenzi wa Mradi
wa mabasi yaendayo kasi yaani DART umesababisha adha kubwa maeneo mbalimbali
jijini Dar es Salaam.
8. KUPUNGUZA
MSONGAMANO KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, kabla ya kusema
chochote naomba ninukuu, sehemu ya hotuba ya Mhe.Waziri wa Ujenzi aliyoitoa
Bungeni mwaka 2011/12 kuhusiana na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es
Salaam, “MIRADI YA KUPUNGUZA MSONGAMANO
WA MAGARI KATIKA JIJI LA DSM. Mheshimiwa
Spika, Wizara inaendelea na mpango wa kujenga Fyovers ili kupunguza msongamano
wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Usanifu wa Flyover eneo la makutano ya
Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere eneo la TAZARA umekamilika chini ya
ufadhili wa JICA, mradi wa Mwenge-Tegeta unaendelea. Sehemu ya Mwenge-Morocco
usanifu umekamilika na ujenzi utaanza mwaka 2012/2013 chini ya ufadhili wa JICA
na mradi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni unaendelea.”
Mheshimiwa Spika, Kama tulivyosisitiza mwaka jana Kambi ya Upinzani Bungeni tunaamini
juu ya ujenzi wa Flyovers ili kuepusha
kero kubwa kwenye jiji la Dar es Salaam maeneo ya TAZARA, MOROCO, UBUNGO,
MAGOMENI, SURRENDER BRIDGE n.k. Serikali haina nia ya dhati kwa hilo, kwani
bajeti ya 2011/12 kama ilivyonukuliwa inaonesha kuwa angalau kwa sasa tungekuwa
na Fly over moja imekamilika lakini hakuna dalili zozote. Hii inaonesha kuwa
Bajeti za Mhe Dr. Magufuli John Pombe (Mb) ni story za kuwafurahisha wabunge na
watanzania tu. Leo anatuambia tenda za ujenzi wa fly over ya TAZARA
itafunguliwa mwezi wa sita nchini Japan.
Mheshimiwa Spika, Aidha Kambi Upinzani inaamini kwamba planning za Serikali ya CCM ni
finyu mno kwani flyovers zinapaswa kujengwa miji yote mikubwa kama Arusha, Mwanza,
Mbeya, Iringa, Tanga n.k. Pia hata
Mikoani na Miji mingine inayokua.
9. WAKALA
WA BARABARA VIJIJINI
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mwaka juzi na mwaka jana tuliishauri Serikali
kuanzisha wakala wa Barabara vijijini, nanukuu tulichokisema, “Mheshimiwa
Spika, tunatambua barabara vijijini zinasimamiwa na Halmashauri zetu ambazo
nyingi hazina uwezo mkubwa wa kifedha na pia hutengewa fedha kidogo na mfuko wa
barabara kulingana na kazi kubwa wanayotakiwa kufanya ya kuhakikisha kuwa
barabara zinapitika katika kipindi chote cha mwaka mzima, Aidha wana ukosefu
mkubwa wa nyenzo na wataalam. Kutokana na umuhimu wa barabara hizi kwa uchumi
wa wananchi wetu ambao wanaishi vijijini, kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya
Upinzani inapenda kuishauri Serikali na kupendekeza kuwepo na WAKALA WA
BARABARA VIJIJINI (RURAL ROADS AGENCY) kwa ajili ya usimamizi, ufanisi na
ujenzi wa barabara bora vijijini”.
Mheshimiwa Spika, hoja ya Kambi Rasmi ya kuanzishwa kwa Wakala wa
Barabara Vijijini ni uwepo wa umuhimu wa kusimamia matumizi ya mabilioni ya
fedha zinazotolewa kila mwaka lakini hazionyeshi kama zinafanya kazi kulingana
na thamani ya fedha zinazotolewa. Aidha aina ya barabara na madaraja
vinavyojengwa haviendani na fedha zinazotengwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kuwanzisha
wakala hii ili kusimamia barabara zinazojengwa na Halmashauri, Serikali ijayo
ya UKAWA itahakikisha inaanzisha WAKALA WA BARABARA VIJIJINI ili kusimamia
ubora wa barabara na madaraja yanayojengwa kwa fedha za Halmashauri.
10.
WAKALA
WA UFUNDI NA UMEME-TEMESA
Mheshimiwa Spika, Majukumu
ya TEMESA ni kushughulikia matengenezo ya magari, mitambo,pikipiki, mifumo ya
umeme,majokofu,viyoyozi na elektroniki kwa Serikali na sekta binafsi. Aidha,
Wakala unaendesha na kusimamia vivuko vya Serikali na ukodishaji wa magari na
mitambo ya kusaga kokoto (Stone Crushers) na kutoa ushauri wa kitaalamu katika
Nyanja mbalimbali za kihandisi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri kueleza kwanini magari ya
Serikali yanatengenezwa kwenye kalakana binafsi kwa gharama kubwa wakati wakala huyu yupo?
11.
MAGARI
YANAYOZIDISHA UZITO, MIZANI NA UHARIBIFU WA BARABARA
Mheshimiwa
Spika, Matakwa ya sheria
Sheria Na. 30 ya 1973 na kanuni Namba 30 ya 2001 iliyotangazwa kwenye
Gazeti la Serikali tangazo Namba 30 la tarehe 9 Februari , 2001 iliyoanza
kutumika tarehe 24 Januari 2001 inafafanua uzito wa magari unaotakiwa.
Kipengele cha saba cha sheria hiyo pamoja na kanuni ya 7(3) ninaeleza magari
yote yenye uzito kuanzia tani 3.5 na kuendelea na aina ya makosa ya uzidishaji
uzito, ambapo kifungu cha 2, 3 na 4 vinafafanua matumizi ya uzito uliozidi
asilimia tano.
Mheshimiwa Spika, Waziri
wa ujenzi Mhe. Magufuli aliwahi kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria
ya barabara namba 30 ya mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha
hakuna magari ambayo yanazidisha uzito na kuharibu barabara. Namnukuu Mhe. Dr.
John Pombe Magufuli“Nchini Ujerumani,
uzito wa magari yote ni tani 40, Uingereza tani 40, Ufaransa tani 40, Urusi
tani 38 lakini Tanzania tani 56, wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,”
alisema,Magufuli.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka maeleza ikiwa uzito unaokubalika kwa barabara za
Ulaya ni chini ya ule unaotakiwa hapa kwetu, na tunaamini barabara za Ulaya
zina ubora zaidi ya ubora wa barabara zetu. Je anasimamia nini hasa kama uzito
anaoruhusu ni mkubwa kwa uhai wa barabara zetu?
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea
kupinga kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ya kuruhusu malori
yanayozidisha uzito kuendelea kuharibu barabara zetu. Sambamba na hilo ni
kuitaka Wizara ya Ujenzi kitengo cha mizani kuwa na mizani ambayo inauwezo wa
kupima uhalisia wa uzito wa gari kinyume na ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa
Spika, baada ya kusema hayo
kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
…………………………………….
Felix Francis Mkosamali(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya
Ujenzi.
27.05.2015
No comments:
Post a Comment