Friday, May 8, 2015

MANENO YA JERRY MURO YAMPONZA,SOMA ALICHOFANYIWA NA TFF


JERRY MURO APIGWA FAINI MILIONI 5

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF iliyoketi jumanne tarehe 5 Mei, 2015 imempiga faini ya sh. 5,000,00 (milioni tano), Afisa Habari wa klabu ya Yanga SC Jerry Muro kwa kutoa kauli za chuki, kisirani na uchochezi dhidi ya uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) nchini na TFF.

Akitoa utetezi wake mbele ya Kamati ya Nidhamu, Jerry Muro alikiri na kujutia kufanya kosa hilo na kudai ilitokana na ugeni wake katika uongozi wa michezo, kwa kuzingatia hilo kamati ilimuepusha na adhabu ya kufungiwa..

Kwa mujibu wa Ibara ya 53 (2)ya Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la 2012, kwa kuidhalilisha TFF na Bodi yake ya Ligi mbele ya umma, kamati imemtoza faini ya sh. 5,000,000 (millioni tano), Jerry Muro na kuwaonya viongozi wengine wa familia ya mpira wa miguu kutojihusisha na vitendo vya matamshi ya aina hiyo.


Shitaka linalomhusisha mchezaji wa Yanga, Amissi Tambwe kumshika kwa kumdhalilisha mchezaji wa Simba SC Juuko Mursheed, na kiongozi wa Friend Rangers Hery Chibakasa wa Friends Rangers kuhamasisha vurugu katika mchezo wa timu yake na dhidi ya Majimaji ya Songea Januari 29, 2015, kamati imeahirisha mashitaka hayo mpaka tarehe nyingine itakapopangwa.

Kamati iliahirisha malalamiko dhidi ya Mohamed Hussein, Muhibu Kanu, Manfred Luambano, Venance Joseph, Mussa Senyange, Saleh Ali, Shafii Maganga na Ismail Salim baada ya kupokea taarifa za udhuru zilizosbabishwa na mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria ya mikoani.
 RAIS TFF AAGIZA USIMAMIZI MECHI ZA MWISHO VPL
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewaagiza wasimamizi wa vituo vya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuhakikisha sheria na taratibu zote za mechi zinafuatwa.

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu huu 2014/2015 inafikia tamati kesho (Mei 9, 2015) ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani katika mechi ambazo ndizo zitakazotoa hatma ya timu zinazoshuka daraja.

Mechi hizo zitakuwa kati ya Ndanda na Yanga (Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara), JKT Ruvu na Simba (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Azam na Mgambo Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Stand United na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), Kagera Sugar na Tanzania Prisons (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mbeya City na Polisi Morogoro (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya), na Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu, Morogoro).


KUMRADHI WANAHABARI
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Mwesigwa Selestine ameomba radhi kwa vyombo kufuatia madai ya waandishi wa habari kupata usumbufu wakati wa utoaji wa Zawadi kwa Mabingwa na washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Mwesigwa alisema kwa niaba ya TFF anaomba radhi kwa usumbufu wowote uliowapata waandishi na wadau wote walioshindwa kushuhudia vema tukio hilo.

“TFF na FIFA vinatambua umuhimu na nafasi ya wanahabri na vyombo vya habari si tu katika kuutangaza mchezo, bali pia katika kutia chachu maendeleo ya mchezo wenyewe “ alisema Mwesigwa.

Hali mbaya ya hewa ilivuruga utaratibu uliokuwa umepangwa awali kuanzia itifaki ya shughuli za kabla na wakati wa mchezo na zile za utoaji tuzo.

Aidha Mwesigwa alisema TFF itaendelea kushirikiana vema na jumuiya ya wanahabari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wana mazingira mazuri wanapofanya kazi kwenye matukio ya mpira wa miguu.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: