Tuesday, May 19, 2015

TANZANIA SASA NAMBA MOJA KWA UTALII

 Kama ilivyoripotiwa na kituo cha utangazaji cha CNN cha nchini Marekani, napenda kutumia fursa hii kuwajulisha kuwa nchi yetu imeendelea kufanya vizuri duniani katika kunadi vivutio vya utalii vilivyoko hapa nchini. Hii inatokana na hatua madhubuti tulizochukua kama nchi, katika suala zima la uhifadhi hasa kwenye ulinzi wa maliasili zetu dhidi ya ujangili ili kuifanya sekta ya utalii iwe nambari moja kwenye ukuzaji uchumi hapa nchini.



Ni uthubutu huo, uliosababisha mafanikio makubwa kwenye mapambano dhidi ya ujangili kwenye hifadhi zetu ambapo kwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo uanzishaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), idadi ya wanyamapori waliokuwa hatarini kutoweka sasa inaongezeka hivyo kuwavutia wageni wengi kutembelea hifadhi zetu mara wanaposikia taarifa kuhusu sekta ya utalii ya Tanzania.


Jambo lililosababisha nizungumze na ninyi asubuhi hii ni kuwajulisha kuwa, nchi yetu kutokana na jitihada mbalimbali ambazo tayari tumezionyesha kwenye sekta hii ya utalii kwa ujumla wake; hivi karibuni imetajwa kuwa ya kwanza barani Afrika kwa ubora na mvuto wa kutembelewa na watalii.



Heshima hii kwa taifa letu ni matokeo ya utafiti wa kina uliofanywa na mtandao wa kimataifa wa nchini Uholanzi unaoshughulika na masuala ya utalii unaofahamika kamasafaribookings.com,  ambao ulitumia takriban miaka miwili kukusanya maoni ya watalii maarufu na wataalamu wa masuala ya maliasili kote duniani, ambao hao walizungumzia uzoefu wao na hali ya sekta ya utalii katika nchi za Afrika, wakieleza wazi juu ya nchi bora kwenye Utalii kwa sasa.


Matokeo hayo yanaonyesha zaidi ya watu 1,000 kutoka nchi 53 walihusishwa kwenye utafiti huo ambao kati ya jumla ya pointi tano za zilizotolewa kwa wastani, Tanzania ilipata pointi 4.8 ambazo ndio alama za juu ikifuatiwa na Botswana yenye pointi 4.75, Kenya 4.66; Zambia 4.58; Afrika Kusini 4.55; Namibia 4.54; Uganda 4.16 na Zimbabwe 4.14. 


Sababu zilizotajwa na watafiti hao, kuwa siri ya ushindi wa Tanzania barani Afrika kwenye sekta ya utalii ni utajiri wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori ambayo mawili kati yao ni maeneo ya urithi wa dunia yanayotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO; maisha ya asili ya wanyamapori hifadhini Serengeti ambako kwa mwaka zaidi ya wanyama hasa nyumbu milioni mbili huhama kuelekea Mbuga ya Maasai Mara kwa upande wa Kenya kisha kurudi nchini.


Pia uwepo wa maeneo ya malazi ya hadhi tofauti tofauti kwenye maeneo yetu ya vivutio kulingana na uwezo wa mtu kiuchumi, fukwe za kuvutia, uwepo wa wanyamapori wasiopatikana maeneo mengine duniani, Mlima Kilimanjaro ambao ni wa kwanza kwa urefu Afrika na hali ya usalama, amani kisiasa zimetajwa kuwa sababu kuu za mafanikio yetu kwenye sekta ya utalii Afrika.


Aidha matokeo ya utafiti huo yamezitaja hifadhi zetu 10 kati ya 16 zilizopo hapa nchini kuwa chachu nyingine ya ushindi kwakuwa Wanyamapori watano wakubwa mbugani ambao ni Simba, Faru, Tembo, Chui na Nyati wanapatikana kwenye baadhi ya hifadhi hizi ambazo ni Serengeti, Selous, Ngorongoro, Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara na Arusha huku Mahale ikitajwa kwa upekee wake wa idadi kubwa ya Chimpanzee.  


Watafiti walistaajabishwa zaidi na Tanzania kwasababu ni nchi pekee ambayo kutokana na utajiri wetu wa maliasili, hatuna majira ya mwaka ambayo utalii hauwezekani kabisa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa au majira; tofauti na nchi zingine ambazo kwenye baadhi ya miezi hali huwa mbaya na watalii huacha kuzitembelea mpaka kipindi hicho kipite.


Ni wazi kuwa tunastahili kujipongeza kwa mafanikio haya, kwani nchi tulizoshindanishwa nazo pia zina ubora wake kwa namna mbalimbali kwenye sekta ya utalii, hivyo hatujawa washindi kati ya wabovu bali washindi miongoni mwa washindi hivyo ni mafanikio makubwa ambayo wote tu mashahidi kuwa kutokana na serikali ya awamu ya nne ya CCM kuonyesha nia ya kutumia utalii kukuza uchumi na kufanya kwa vitendo; tumeweza na tunaendelea kusonga mbele.


Tunajifunza nini kwenye suala hili? Hatulewi sifa, tunaendelea kuchapakazi ambapo katika kulithibitisha hili, hivi karibuni tuliwaalika waandaji maarufu wa filamu bora duniani kutoka Hollywood wakachukua picha kwenye hifadhi zetu ili kuandaa tangazo la viwango vya kimataifa ambalo litarushwa kwenye vituo vya televisheni vya mashirika ya kimataifa ya habari ikiwemo CNN ili kuvutia watalii wengi zaidi.


Tangazo hilo ambalo litakamilika na kukabidhiwa kwetu hivi karibuni, litazinduliwa na Mhe. Rais Dk. Jakaya Kikwete, ili lianze kurushwa rasmi kwenye vituo hivyo kote duniani; Watanzania tunachotakiwa kufanya ni kuendelea kuitunza amani iliyopo, kutunza mazingira yanayozunguka hifadhi zetu na ndani ya hifadhi bila kusahau kutoa ushirikiano kwa TAWA na mamlaka zingine juu ya taarifa za majangili ili tuendelee kuwa bora Afrika na duniani.
Lazaro Nyalandu
……………………
Waziri wa Maliasili na Utalii

No comments: