Thursday, May 28, 2015

UMESKIA HII ALIYOSEMA SALUM MWALIM KUHUSU MSWADA WA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA,SOMA HAPA



 Picha na maktaba yetu





Wakati uamuzi wa Serikali kukusudia kuwasilisha bungeni miswada mwili kwa ajili ya kutunga sheria za Huduma ya Vyombo vya Habari  na Haki ya Kupata Taarifa ukiendelea kupingwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zanzibar, Salum Mwalim ameenda mbali na kuwashauri Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT) kususia habari taarifa za serikali kwa wiki moja.


Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Endasaki, Hanang, mkoani Manyara, Mwalim alisema kuwa MOAT wanapaswa kuacha kutoa taarifa zinazoihusu Serikali akisema kuwa hiyo ni mojawapo ya njia za kuonesha hisia zao dhidi ya kile alichodai kuwa ni njama za serikali kwa vyombo vya habari na wanahabari.
Mwalim ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari alisema kuwa anaungana na wadau wa vyombo vya habari nchini wakiwemo wamiliki na Baraza la Habari nchini (MCT) katika kupinga miswada hiyo, hususan ule wa Huduma ya Vyombo vya Habari ambao umeelezwa kuwa na vipengele vinavyolenga kuminya uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa kwa vyombo vya habari na wananchi wa kawaida.
“Naomba kuungana na wanahabari wenzangu na Watanzania wote kwa ujumla kuupinga muswada huu unaolenga kuminya na kukandamiza uhuru wa habari si kwa vyombo vya habari pekee bali mwananchi mmoja mmoja katika haki ya kupata taarifa.
“Naungana na wamiliki wa vyombo vya habari na Baraza la Habari nchini kwa uamuzi wao wa kuupinga vikali na kuamua kutuma timu ya watu kwenda Dodoma kuzungumza na wabunge ambao hawako tayari kuona nchi inakuwa na sheria zinazoturudisha nyuma badala ya kusonga mbele pamoja na mataifa mengine yanayoendelea kwa sababu ya kuheshimu uhuru wa habari na wananchi kupata taarifa.
“Badala ya serikali kupeleka muswada ambao utapitishwa na kuwa sheria yenye maslahi kwa na nia njema kwa wamiliki wa vyombo vya habari, wanataaluma na taaluma yenyewe ya habari, inafikiria namna ya kuminya hata uhuru huu mdogo uliopo sasa ambao nao tumekuwa tukiulalamikia kwa sababu ya kuwepo kwa sheria kandamizi kama ile ya Magazeti, Usalama wa Taifa na zingine,” alisem Mwalim na kuongeza;
“Nawashauri MOAT ili serikali hii ielewe kuwa suala hili si la mzaha, waache kutoa taarifa zinazoihusu serikali hii ya CCM kwa muda wa wiki moja ili kuelezea hisia zao kuwa hawakubaliani kabisa na njama za kuminya uhuru wa habari.”
Kiongozi huyo ambaye alizindua mafunzo ya uzalendo kwa vijana wa chama hicho wilayani Hanang akiendelea na ziara ya chama hicho katika kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa wingi kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka huu, alidai kuwa kuminya uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa hutokana na hofu ya watawala kuondolewa madarakani.
Alisema kuwa wakulima wanapokuwa na shida ni vyombo vya habari ambavyo huwasemea hivyo hivyo kwa makundi mengine katika jamii kama wafugaji, walimu, madktari, wanafunzi, hivyo akavitaka vyombo vya habari na wanahabari nao kuchukua hatua ngumu za kujisaidia na kuokoa taaluma yao.
Alisema kipengele kinachotaka vyombo vya habari vya binafsi kuungana na Shirika la Utangazaji la Taifa ni kulirudisha nyuma taifa na kukaribisha udikteta usioweza kuvumilika.
Aliwataka Watanzania kuona kuwa suala hili ni muhimu kwao wala halihusu watu wachache pekee kwani kunyamaza kimya kutasababisha watawala kutunga sheria ambayo itawalazimisha wananchi wote kutazama TBC hata kama hawataki.
Mwalim alikwenda mbali na kusema kuwa kipengele hicho ni cha ajabu kwa sababu kwa ufahamu wake, hata viongozi wa serikali wenyewe wakiwemo mawaziri hawaiamini TBC ambapo aliongeza kuwa uzoefu unaonesha wanapokuwa na mikutano na waandishi wa habari kisha ikawepo TBC pekee huwa hawaendelei hadi vyombo vya habari vingine viwepo.
Aliwataka Watanzania kupinga muswada huo akisisitiza kuwa vyombo vya habari ni mhimili wa nne unaojitegemea ambao unapaswa kuwa huru kadri inavyotakiwa ili kuiangalia mihimili mingine mitatu ya serikali.
Kiongozi huyo anaendelea na ziara yake ambapo leo Ijumaa, kesho Jumamosi na Jumapili atakuwa katika Mkoa wa Kilimanjaro ambako anatarajiwa kufanya vikao vya ndani, kuwa mgeni rasmi mahafali Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa CHADEMA (CHASO) Mkoa wa Kilimanjaro na kufanya mikutano ya hadhara.

No comments: