HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O. MBILINYI (MB) KUHUSU
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA
MICHEZO KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za
Bunge toleo la mwaka 2013)
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, napenda
kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu. Namshukuru Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Mhe. Freeman A. Mbowe kwa kuniamini kwa miaka mitano kwenye nafasi hii ya
uwaziri kivuli ili kusimamia mausala ya habari, vijana, utamaduni na michezo.
Pia nawapongeza wenyeviti wenza wa UKAWA, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba , Mwenyekiti wa CUF, Mheshimiwa James Mbatia,
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi pamoja na Mwenyekiti wa NLD Mheshimiwa Dr. Emmanuel
Makaidi kwa kazi nzuri nzuri wanayoifanya ya kuwaunganisha watanzania mpaka hivi sasa wako tayari
kukiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani kwa ushindi wa kishindo ifikapo Oktoba
2015 .
Aidha,
nasisitiza kuwa shukrani zangu za dhati kwa wana Mbeya wenzangu nitakuja
kuzitoa mkoani Mbeya baada ya kuhitimisha majukumu yangu ya Bunge hili la 10
kwa kuwa agano letu lilifanyika katika ardhi ya Mbeya hivyo sina budi kurudi
tena kwenye ardhi hiyo kuwashukuru watu wangu wa nguvu, kwa nafasi na heshima
kubwa mliyonipa kwa miaka hii mitano na nawaahidi uwakilishi wa kiwango kile
kile kwa miaka mitano ijayo.
UHURU WA HABARI
Mheshimiwa Spika,
Taswira nzuri ya Tanzania kimataifa kama nchi inayofuata utawala bora na
demokrasia inazidi kupotea kutokana na ubabe wa Serikali ya CCM katika kuminya
uhuru wa habari nchini. Kushindwa kwa hila za Serikali ya CCM mbali na kufungia
magazeti na hata kuwateka, kuwatesa na kuwaua wanahabari wanaotimiza wajibu wao
sasa kumehamia katika kutunga sheria kandamizi ambazo zina malengo ya kuwafunga
midomo wanahabari. Ni hivi karibuni, vyombo vya kimataifa ikiwemo gazeti kongwe
Washington Post la Marekani, lilianika
ubabe wa Serikali ya CCM na kushinikiza wafadhili na wahisani hasa Serikali ya
Marekani na Benki ya Dunia kusitisha kuipa Tanzania misaada ili kuishinikiza
Serikali ya CCM kuzirekebisha Sheria hizo kandamizi ambazo zilisainiwa na Rais
Kikwete hivi karibuni kwa kuwa zinaminya uhuru wa habari.
Mheshimiwa Spika,
Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya
Makosa ya Mitandao ambayo inalenga kuua uhuru wa habari hata baina ya
mtu na mtu ambapo mtu anaweza kwenda jela kwa kosa la kufowadi ujumbe, taarifa
ama picha ambayo ameipokea kutoka kwa mtu mwengine( yaani spams). Lakini pia,
vyombo vya kimataifa vinaeleza kuwa kupitishwa kwa Sheria ya Takwimu kutatia
hatiani watu hasa wanahabari kwa kigezo kuwa wametoa takwimu ambazo Serikali
itaona si za kweli n a bila kupata kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Mheshimiwa Spika,
inashangaza kuona kuwa Taifa linapelekwa gizani kwa Sheria hizi za kibabe
zisizozingatia dhana ya uwazi ambayo Serikali inajidai kuitekeleza. Sote ni
mashahidi kuwa mara nyingi Serikali imekua haitoi takwimu sahihi za mambo
mbalimbali na kwa nyakati tofauti Serikali pia imekiri kuwa haina takwimu
kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo taarifa za ajira na ukosefu wa ajira. Ikumbukwe
kuwa, wakati wa ajali ya Meli ya MV Spice Islander, Serikali haikutoa idadi
sahihi ya watu waliokuwepo kwenye meli ile kwa kuwa haikua na takwimu. Ni
vyombo vya habari ambavyo vilifichua idadi sahihi ya wahanga wa ajali ile kwa
kuwa vilikuwepo eneo la uokoaji, leo hii unapowanyima watu uhuru wa kutoa
taarifa zinazoambatana na takwimu za masuala husika mpaka kupata kibali cha
Ofisi ya Takwimu, tunalenga kuficha ukweli gani?
Mheshimiwa Spika,
kuelekea uchaguzi Mkuu ambapo mara nyingi matukio ya udanganyifu juu ya takwimu
za matokeo ya uchaguzi zimekua zikichakachuliwa na Serikali , Sheria hii ya
Takwimu inalenga kwa namna yoyote ile kuminya haki ya watanzania kupata takwimu
sahihi ambazo zinaweza kutolewa kwa usahihi na wadau wengine ambao wanashiriki
katika mchakato wa uchaguzi Mkuu. Hii inalenga kupotosha umma wa Tanzania
katika kupata taairfa sahihi.
Mheshimiwa Spika ,
muendelezo wa malalamiko dhidi ya Sheria hizo kandamizi pamoja na muswada wa
Habari ambao unaelezwa kuwa katika mkakati wa kuletwa ndani ya Bunge hili,
umepingwa vikali pia na wadau wengi nchini ikiwemo Chama cha Wamiliki wa Vyombo
vya Habari Nchini (MOAT) ambao walifanya kikao tarehe 26 Mei mwaka huu jijiji Dar es Salaam, walielezea kuwa muswada
huu kandamizi ni tishio kwa demokrasia na amani nchini. Kambi ya Upinzani
Bungeni, inaungana na wadau wote wanaoupinga muswada huu kandamizi na
tunaitahadharisha Serikali ya CCM kutouleta muswada huu bila ya kuurudisha kwa
wadau wake wakubwa na kufanya nao madhiriano na kurekebisha vifungu ambavyo
vinaendeleza ubabe wa Serikali hii
kuminya uhuru wa habari nchini hasa kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2015.
Aidha,
Kambi ya Upinzani Bungeni inalaani taarifa za kutishiwa maisha kwa mmiliki wa
kituo cha televisheni cha ITV, Dr. Reginald Mengi eti kwa madai kwamba kituo
chake kimekua kikitoa habari za kiuchochezi zinazosababisha kuyumba kwa
Serikali ya Rais Kikwete ikiwemo habari za kashfa ya ufisadi wa Mabilioni ya Akaunti
ya Tegeta ESCROW.
MAENDELEO YA VIJANA
Mheshimiwa Spika, Serikali
ya CCM haijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kushughulikia changamoto na
matatizo ya vijana wa taifa hili hasa ukosefu wa ajira. Mara nyingi Serikali
hii imekuwa ikiyatumia makundi mbalimbali ya wananchi ikiwemo vijana pale
inapowahitaji hasa nyakati za uchaguzi. Mfano halisi ni namna ambavyo ilipora
Muswada wa uanzishwaji wa Baraza la Vijana kwa kuhisi kuwa endapo muswada
Binafsi wa Mbunge wa Upinzani Mheshimiwa John Mnyika ungepita, CCM ingepoteza
kura za vijana. Kwa kuwa Serikali ya CCM iliingilia mchakato huu bila kujiandaa
matokeo yake ni kuvuruga mchakato mzima wa uendeshaji wa Baraza hilo. Ikumbukwe
kuwa, kwenye mchakato huu wa Baraza la Vijana Bungeni, Kambi ya Upinzani
Bungeni ilipendekeza uanzishwaji wa Baraza la Vijana uende sambamba na
uanzishwaji wa Mfuko wa Vijana ambao ungewezesha Baraza hilo kujiendesha kwa
uhuru. Kwa kuwa Serikali haikua na dhamira wala nia ya dhati ya kuanzisha
Baraza la Vijana lakini waliutumia mchakato huo kisiasa ili kuwalaghai vijana
wa Taifa hili; Serikali ilipinga kwa nguvu zote kuanzishwa kwa Mfuko wa Vijana
ili Baraza hilo liwe tegemezi kwa Serikali kama njia mojawapo ya kulidhibiti.
Serikali hii ya CCM pia haina nia ya dhati ya kutatua changamoto za vijana za
kiuchumi na ndio maana imeshindwa kutekeleza agizo la kuzitaka halmashauri zote
nchini kutenga asilimia 5 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana.
Kambi
ya Upinzani Bungeni, inawaahidi vijana wote nchini kuwa, UKAWA itakaposhika
madaraka itahakikisha kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaanzishwa sambamba na
utekelezaji wa agizo la kuzitaka halmashauri zote kutenga fedha kwa ajili yao.
BARAZA LA KISWAHILI TANZANIA
Mheshimiwa Spika,
suala la kukuza na kukiendeleza Kiswahili ni kipaumbele cha Baraza la Kiswahili
Tanzania. Kwa muda mrefu , Serikali hii si tu kuwa imeshindwa kuwawezesha
BAKITA kibajeti bali hata viongozi wakuu wa Serikali ya CCM wameshindwa kuunga
mkono juhudi za BAKITA katika kueneza Kiswahili. Ni kama Viongozi wetu wanaona aibu kutumia lugha ya
Kiswahili kwenye majukwaa ya kimataifa ili kukitangaza Kiswahili. Katika hili,
Rais Kikwete amekua kinara wa kutumia Kiingereza badala ya kutumia lugha yetu
ya Taifa kwenye shughuli mbalimbali za kimataifa wakati viongozi wa mataifa mengine
wakitumia lugha za mataifa yao; kwa mfano alipokuja Rais wa China, Rais wa
Marekani Obama na hata kwenye mkutano wa
Usuluhishi wa Burundi hivi karibuni.
Lakini, Rais Nyussi wa Msumbiji alipolihutubia Bunge lako hivi karibuni
alitumia lugha ya taifa lake ambayo ni kireno japokuwa ana uwezo wa kuzungumza
lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.
KUZOROTA KWA SEKTA
YA MICHEZO NCHINI
A. Viwanja Vya Michezo
Mheshimiwa Spika,
kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeendelea kuona umuhimu wa
taifa kuwekeza katika viwanja vya michezo ili kuweza kupanua wigo wa taifa
kujitangaza na kukusanya mapato yanayotokana na viwanja vya michezo nchini.
Labda, wizara mpaka sasa haijaweza kujua hasara ambazo kama taifa tunapata
kutokana na kutotumia nafasi zinazotokea na kutowekeza vya kutosha katika
kuboresha michezo nchini.
Mheshimiwa Spika,
enzi za chama kimoja, majengo na maeneo yote ya umma yalikuwa chini ya
Serikali. Ujenzi na uendelezaji wa maeneo hayo ulisimamiwa na Serikali kupitia
kodi za wananchi, michango, fedha za wafadhili na wahisani mbalimbali na hasa
wananchi kujitolea nguvukazi. Baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama
vingi mwaka 1992, mambo yote yaliyokuwa yakisimamiwa na Serikali ya CCM
yalirudishwa kwa umma isipokuwa viwanja mbalimbali vya michezo ikiwemo uwanja wa CCM Kirumba (Mwanza),
Samora (Iringa), Sokoine (Mbeya), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Majimaji
(Songea), Kaitaba (Kagera) n.k. ambavyo CCM ilivipora na kuvihodhi.
Mheshimiwa Spika,
leo hii pamoja na CCM kuendelea kuhodhi viwanja hivi imeshindwa kuviendeleza na
matokeo yake kuwanyima fursa wananchi wa maeneo husika kushuhudia michezo
mbalimbali kwa kuwa viwanja hivyo huwa havikidhi viwango vya ubora vya michezo
hali inayofanya michezo mingi mikubwa ikiwemo ya kimataifa kufanyika Dar Es Salaam
pekee. UKAWA inawaahidi watanzania kuwa pamoja na kujenga viwanja vipya vya
kisasa pia tutavirudisha viwanja hivyi vyote kuwa mali ya umma chini ya
halmashauri za miji ili vitunzwe na vilete tija zaidi kwenye maendeleo ya
michezo.
B. Kushuka kwa Viwango vya Michezo
Mheshimiwa Spika, pamoja
na tatizo la ukosefu na usimamizi wa viwanja vya michezo nchini (stadiums),
Serikali ya CCM inamaliza awamu ya nne huku ikiwa imeua sekta ya michezo
kabisa. Leo Tanzania inaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu kuanzia kwenye
riadha, ngumi, netiboli, mpira wa kikapu na kwa kiwango kikubwa kwenye mchezo
wa soka ambao Serikali imeshindwa hata
kwenda sambamba na juhudi za makampuni binafsi na wadau mbalimbali katika
kuendeleza michezo. Mara nyingi tumeishauri Serikali kuwapa kipaumbele na
kuwaendeleza makocha wazawa badala yake imekuwa ikiendekeza makocha wa kigeni
ambao mpaka leo hawajatusaidia wakati historia inaonesha kuwa makocha wazalendo
kama Joel Bendera, Marehemu Zakaria Kinanda na wengineo walifanya kazi nzuri
kwenye timu yetu na kuipa sifa nchi. Lakini leo hii tunafungwa na timu kama
Lesotho tukiwa chini ya kocha wa kigeni ambaye analipwa fedha nyingi za walipa
kodi. Na ndio maana si ajabu leo Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Jamal
Malinzi anapoulizwa mafanikio yake toka apokee kijiti cha uongozi kutoka kwa
Leonard Edgar Tenga, anajibu kuwa ni kufanikiwa kuonesha mechi 12 za kimataifa
laivu kwenye luninga.
MAPATO YA VIINGILIO VYA VIWANJA
VYA MICHEZO
Mheshimiwa Spika,
katika miaka ya karibuni tumeshuhudia kukua kwa viwango vya michezo
mbalimbali ikiwemo riadha, soka, mpira wa pete na mpira wa kikapu
kunakokwenda sanjari na ongezeko la wapenzi wa michezo huo katika miji
mbalimbali. Hata hivyo, ongezeko hilo linaonekana wazi kutokwenda sambamba na
ujenzi wa viwanja vipya, upanuzi na uboreshaji wa viwanja vya soka vilivyopo.
Mbali
na Uwanja wa Taifa, kwa takribani miaka thelathini hapajakuwa na maendeleo
yoyote ya ujenzi wa viwanja vipya au ukarabati wa vilivyopo ili kukidhi matakwa
ya ongezeko la wapenzi wa michezo hiyo pamoka
na maendeleo ya michezo kwa ujumla. Katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita FIFA imeisaidia Tanzania kukarabati viwanja kadhaa, lakini jitihada
hizo zimekuwa zikikwamishwa na serikali kwa kutoza kodi kubwa vifaa vya ujenzi
na ukarabati wa viwanja hivyo. Ukarabati wa Uwanja wa Kaitaba unaoendelea mjini
Bukoba umekumbwa na changamoto hiyo ya kodi.
Kwa
mujibu wa Ripoti ya Kamati Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha Mapato ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyotolewa Mei 2011, viwanja vingi vinavyotumika
katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) vilijengwa miaka ya 1970 na 1980
na havina miundombinu inayokidhi masharti ya ulinzi, usalama na burudani.
Ukurasa
wa 10 wa ripoti hiyo yenye jumla ya kurasa 95 na viambatanisho tisa unasema:
“Viwanja vyetu vingi havitoi fursa kwa watazamaji kuingia uwanjani bila
bughudha, kukaa kwa raha na starehe na urahisi wa kutoka uwanjani baada ya
mechi.”
“Pia havitoa fursa ya
watazamaji kupata viburudisho kama vinywaji na vitafunwa, sehemu ya kuuzia
kumbukumbu kama picha na machapisho mbalimbali ya michezo mfano ratiba za ligi
na kalenda. Haviwakingi watazamaji dhidi ya jua kali au mvua na havina huduma
nzuri ya vyoo kwa ajili ya wachezaji na watazamaji,” inaongeza ripoti hiyo.
Mheshimiwa Spika,
mojawapo wa vyanzo vya mapato vya wizara hii ni mapato ya viingilio vya
uwanjani. Lakini leo Serikali hii iambayo imehodhi viwanja vya mali ya
wanatanganyika, inawezje kujipatia mapato ikiwa inashindwa kuendelea viwanja
vya watanganyika na badala yake imevihodhi kiujanja ujanja tu?
Mheshimiwa Spika,
Katikati mwa msimu wa 2013/14 wa VPL, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
ilivifungia viwanja vyote vya soka vinavyomilikiwa na CCM pamoja na Uwanja wa
Kaitaba, kutumika kwa mechi za ligi kuu na Ligi Daraja la Kwanza kutokana na dosari
mbalimbali. Mbali na mfumo wa tiketi za elektroniki (ETS) uliosimikwa na CRDB
kwenye baadhi ya viwanja kisha kusitishwa kibabe siku nne kabla ya mechi ya
mzunguko wa pili wa VPL msimu huu ya Simba dhidi ya Yanga, viwanja vya soka
nchini havina vifaa vya ukaguzi, uthibiti wa tiketi na uingiaji viwanjani
(ticketing and access control facilities).
Mheshimiwa Spika,
leo hii kuna mazingira makubwa ya ubadhirifu wa mapato ya viwanja vya michezo
na badala yake, kusitishwa kwa mfumo wa tiketi za kieletroniki kumepelekea watu
wachache kunufaika na fedha za mapato huku sekta ya michezo ikidorora.
Tunaishangaa serikali ya CCM kuanzisha mambo ambayo kimsingi utekelezaji wake
kwao ni mzigo na bado wanadhani watapewa ridhaa ya kutumikia watanzania.
Inawezekanaje uwanja wa mpira ujae kwa kiwango cha level seats lakini
watazamaji wazidi kiwango cha uwezo wa uwanja kubeba watazamaji? Je Serikali
hii chovu inasubiri yatokee maafa uwanjani ndio wajue kuwa kuna umuhimu wa
kufuata utaratibu ambao wanashindwa kuutekeleza?
Mheshimiwa Spika,
wakati serikali ikitangaza kusitisha matumizi ya mfumo wa tiketi za elektroniki
(ETS) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ni mojawapo wa mikakati ya
Serikali ya CCM kuhalalisha ‘madudu’ ya ulaji kwa watendaji wa shirikisho na
serikali kupitia matumizi ya tiketi za vishina. Uamuzi wa kusitisha matumizi ya
ETS umelenga kurudisha ulaji wa mapato ya milangoni kupitia mauzo ya tiketi za
ziada na bandia za mfumo wa kizamani wa vishina. Ikumbukwe kuwa, tiketi za
elektroniki zilifuta ubebaji wa fedha za mapato kwenye viroba. Zimekuwa chungu
kwa maofisa wa TFF na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambao
walikuwa wameshazoea kujineemesha kwa kubeba fedha kwenye viroba na rumbesa.
Mheshimiwa Spika,
toka kutangazwa kufutwa kwa mfumo hhuo wa ukataji wa tiketi kwa njia ya
kieletronki kuna taarifa kuwa wakati
baadhi ya klabu zikidai kwamba hakuna uwazi kwa maofisa wa CRDB katika
kutengeneza na kuuza tiketi, taairafa hzio ni za uongo kwa kuwa zimelanga
kuweka Milano ya ubadhirifu wa mapato ya viingilio kwa kuwa TFF walipewa Nyila (password) na CRDB inayowawezesha maofisa wa shirikisho
kuona moja kwa moja pesa inayoingia kupitia mauzo ya tiketi. Pia kuna makubaliano
ya kuonyesha idadi ya watu waliokata tiketi dakika 10 kabla ya mechi kumalizika.
Mheshimiwa Spika,
aidha mpaka sasa si TFF wala wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na michezo
ambazo zimeeleza ni nani anayetengeneza tiketi kwa sasa? Huu uvunjaji wa katiba
ya shirikisho. Ni aibu kwa Wizara hii kutoka kwenye mfumo wa kisasa wenye
manufaa na kurudi kwenye mfumo wa kizamani ambako nchi nyingi zimeshauacha ili
kuweza kuwanufaisha watu wachache huku Serikali iikosa mapato ambayo
yangetumika kuimarisha viwanja ambavyo vimepokwa na CCM.
MCHAKATO WA VAZI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika,
naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa serikali ya CCM imetumia fedha
nyingi za walipa kodi kuendesha mchakato
wa kutafuta vazi la taifa kama vile vazi la Taifa lingeweza kutatua matatizo ya
watanzania endapo lingepatikana. Leo ikiwa imepita miaka mitatu toka kamati
iliyokua ikisimamia mchakato wa vazi la taifa kukabidhi ripoti yake, ripoti
hiyo haijawekwa hadahrani na hakuna anayejua azma ya fedha za walipa kodi
zilizohalalishwa kutumika kwa ajili ya vazi la taifa na tena kwa kufanya
mchakato huo mara mbili.
Mheshimiwa Spika,
mavazi ya nchi hii yanafahamika, kama khanga, kitenge, lubega, kaniki,
kibwebwe na mengineyo mengi. Kitendo cha Serikali ya CCM kuwaaminisha wananchi
kuna ulazima wa kuwa na vazi la Taifa huku viongozi wa Kitaifa wakiwa
wanaendelea na maisha yao ya kila siku bila uwepo wa vazi hilo ni dhahiri
haujatatua matatizo yao ikiwemo ukoefu wa huduma za afya, elimu duni, ukosefu
wa maji safi na salama na ongezeko la gharama za maisha.
MBIO ZA MWENGE
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekua ikipingana na utumiaji wa fedha za
walipa kodi na kitendo cha Serikali kuendelea kuwatoza wananchi kwa mashinikizo
bila ridhaa zao kuchangia shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru. Ni kweli kuwa
Mwenge wa uhuru ni hazina kwa taifa letu jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inakubaliana nalo na kwa muda mrefu tumependekeza Mwenge wa uhuru
uwekwe katika makumbusho ya taifa ili kuweza kuwapatia fursa wananchi kuweza
kujifunza hapo.
Mheshimiwa Spika, Suala la kuenzi historia
ya Taifa ni la lazima lakini kuendelea kutumia gharama kubwa kwa jambo hili
wakati Watanzania wengi hawana huduma muhimu ni dharau kubwa. Aidha, katika kipindi
hiki ambacho mwenge wa uhuru unapitishwa katika sehemu mbalimbali za nchi,
chama tawala nacho kinapita katika maeneo mbalimbali ya nchi kuangalia
utekelezaji wa ilani yake pamoja na kuzindua miradi ya maendeleo ya wananchi.
Huu ni usanii mkubwa unaofanywa na Serikali ya CCM kwa dhumuni la kuwanyonya
watanzania masikini kwa kigezo cha kuwa wanachangia shughuli za maendeleo
wakati ukweli ni kuwa watanzania wanachangishwa mpaka fedha kwa ajili ya malazi
na chakula kwa wakimbiza mwenge kama alivyojibu Waziri Mkuu. Na kwa kuwa
kumekua na malalamiko kutoka wa wafanyabiashara, wafanyakazi wa Serikali na
hasa walimu sehemu mbalimbali nchini kuwa wanalazimishwa kuchangia mwenge bila
ridhaa yao. Na kama CCM inataka bado mambo ya mbio za mwenge basi wagharamie wenyewe kwa asilimia 100 na si kuwalazimisha wananchi
kuchangia hasa ukizingatia kuwa Waziri Mkuu alitoa kauli wiki hii kuwa
kuchangia mbio za mwenge wa uhuru ni hiyari. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaendelea kusisitiza kuwa sasa ni wakati muafaka mwenge wa uhuru
kupelekwa jumba la Makumbusho ya Taifa.
Mheshimiwa Spika,
ikumbukwe kuwa pamoja na Serikali kusema kuwa mwenge huu unahamasisha ushiriki
wa shughuli za miradi ya maendelepo, leo hii halmashauri na mikoa mingi nchi
zimepokea takribani asilimia kati ya 15-25 tu ya miradi ya maendeleo, ni
maendeleo gani ambayo CCM inayahamasisha huku Serikali ikiwa haifikishi fedha
za maendeleo na matukio ya ngono zembe na maambukizo ya UKIMWI yakishamiri?
HITIMISHO
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inawataka
vijana, wana utamaduni, wanamichezo na wadau wa habari wote kufanya maamuzi
sahihi itakapofika Otoba mwaka huu. Pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha
katika daftari la wapiga kura na wawe tayari kuiondoa Serikali hii ya CCM
inayopenda kuanzisha migogoro na wananchi kila siku kitu ambacho ni hatari kwa
amani ya nchi hii. Serikali hii tayari ina migogoro na wafanyakazi, walimu,
wanafunzi, vijana, wazee, viongozi wa dini, wafanyabiashara, madereva na sasa
bila sababu za msingi inazidisha vita na wadau wa habari.
Mheshimiwa Spika,
naomba kuwasilisha.
…………………………..
JOSEPH
O. MBILINYI (MB)
MSEMAJI
MKUU WA KAMBI YA UPINZANI-WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO.
28.05.2015
No comments:
Post a Comment