Tuesday, June 30, 2015

TIZAMA VIJANA WA MKWASA WANAVYOJIFUA KUWAFWATA UGANDA KWAO



 STARS KUWAFUATA UGANDA ALHAMIS
Timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager inatarajiwa kuondoka nchini siku ya alhamis kuelekea nchini Uganda kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaofanyika siku ya jumamosi nchini humo.

Mchezo huo wa marudiano kuwania kufuzu kwa fainali za CHAN 2017 zitakazofanyika nchini Rwanda utachezwa siku ya jumamosi katika uwanja wa Nakivubo jijini Kampala kuanzia majira ya saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Kocha mkuu wa Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa amesema kikosi chake kinaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo huo utakaochezwa mwishoni mwa juma nchini Uganda.

“Wachezaji wote waliopo kambini wanaendelea na mazoezi, vijana wanajituma mazoezin, morali ni ya hali ya juu naamini tutafanya vizuri katika mchezo wetu wa siku ya jumamosi” alisem Mkwasa.

Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini siku ya alhamisi jioni kwa usafiri wa shirika la ndege la Rwanda (Rwanda Air) ikiwa na kikosi cha wachezaji 20, benchi la ufundi pamoja na viongozi.

Aidha Mkwasa amesema ataongea na waandishi wa habari siku ya alhamis asubuhi saa 5 kamili - Karume juu ya maandalizi ya kikosi chake kuelekea kwenye mchezo wa marudiano na kuweka wazi kikosi kitakachosafiri kuelekea nchini Uganda.

Stars imeweka kambi yake katika hoteli ya Kiromo mjini Bagamoyo na inafanya mazoezi katika uwanja wa Boko Veterani kila siku jioni kuanzia majira ya saa 10 jioni.

FDL KUCHEZWA MAKUNDI MATATU 2015/2016
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa msimu wa 2015/2016 itachezwa katika makundi matatu ya timu nane nane kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.

Mfuko huo wa makundi matatu umetokana na marekebisho ya Kanuni za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) yaliyofanywa hivi karibuni na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao cake kilichofanyika mjini Zanzibar.

Timu ya kwanza katika kila kundi la ligi hiyo itakayoanza Septemba 12 mwaka huu itapanda kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa msimu wa 2016/2017 wakati timu itakayoshika nafasi ya mwisho katika kila kundi itashuka kucheza Ligi Daraja la Pili (SDL) kwa msimu wa 2016/2017.

Kundi A linaundwa na timu za African Lyon FC (Dar es Salaam), Ashanti United SC (Dar es Salaam), Friends Rangers FC (Dar es Salaam), Kiluvya United FC (Pwani), Kinondoni Municipal Council FC (Dar es Salaam), Mji Mkuu FC (Dodoma), Polisi Dar es Salaam na Polisi Dodoma.

Timu zinazounda kundi B ni Burkina Faso FC (Morogoro), Kimondo SC (Mbeya), Kurugenzi Mafinga FC (Iringa), Lipuli FC (Iringa), Njombe Mji FC (Njombe), Polisi Morogoro na Ruvu Shooting (Pwani). 

Kundi C ni Geita Gold SC (Geita), JKT Kanembwa FC (Kigoma), JKT Oljoro (Arusha), Mbao FC (Mwanza), Panone FC (Kilimanjaro), Polisi Mara, Polisi Tabora na Rhino Rangers (Tabora).

U15 YAREJEA DAR
Kikosi cha timu ya Taifa cha vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U-15) leo kinarejea jijini Dar es salaam kikitokea mkoani Mbeya ambapo jana kiliibuk ana ushindi wa ushindi wa mabao 4-1.

U15 ambayo inaandaliwa kwa ajili ya kuwania kufuzu kwa fainali za vijana chini ya miaka 17 barani Afrika kilikua na ziara ya michezo ya kirafiki miwili jijini Mbeya ambapo katika mchezo wa awali pia kiliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Mara baada ya kurejea leo jioni jijini Dar es salaam, kambi ya timu hiyo itavunjwa mpaka watakapokutana tena mwisho wa mwezi ujao kwa ajili ya kuelekea visiwani zanzibar kwa jili ya michezo ya kirafiki.

Lengo la michezo hiyo ya kirafiki ni kutoa nafasi ya kocha Bakari Shime kutambua uwezo wa vijana wake na kuongeza wachezaji wengine katika kikosi hicho kisha kuandaa kikosi bora kitakachoshirki kuwania kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika nchini Madagascar mwaka 2017.




No comments: