.

MOHAMED MTOI KUZIKWA KESHO,MBOWE KUHUDHURIA


Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano, kwa masikitiko makubwa inatangaza msiba wa aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Lushoto ambaye pia alikuwa Ofisa Mwandamizi wa Makao Makuu ya Chama, Ndugu Mohamed Kanyawana Shemg'ombe Mtoi akiratibu Kanda za Chama Taifa.

Kamanda Mtoi alifariki dunia baada ya kupata ajali, Jumamosi ya Septemba 12, mwaka huu, eneo la Magamba alipokuwa njiani kurejea nyumbani kwao Mkuzi baada ya shughuli za kampeni jimboni humo.


Ofisi ya Katibu Mkuu na Chama kwa ujumla kimempoteza mmoja wa wanachama, mtendaji na kiongozi mahiri kabisa katika wakati ambapo mchango wake ulikuwa ukihitajika sana.

Mazishi ya Ndugu Mohamed yamepangwa kufanyika kesho saa 7 mchana nyumbani kwao Mkuzi, Lushoto ambapo Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe atashiriki.

Chama kwa kushirikiana na familia kinafanya uratibu wa msiba huo na taarifa zaidi zitaendelewa kutolewa.

Pamoja na mambo mengi, Ndugu Mohamed atakumbukwa sana kwa namna alivyoratibu na kusimamia uendeshaji wa Kanda za Chama kupitia idara yake chini ya Kurugenzi ya Oganaizesheni, Mafunzo na Uratibu wa Kanda.

Kama inavyojulikana, dhana ya kuendesha chama kupitia Kanda, imekuwa ni utekelezaji kwa vitendo wa mojawapo ya sera muhimu za chama, iitwayo Mfumo Mpya wa Utawala, hivyo Ndugu Mohamed alikuwa aliaminika na kupewa majukumu makubwa ya kuhakikisha chama kinathibitisha kwa Watanzania kuwa mawazo mbadala ya mabadiliko yanawezekana kwa manufaa ya taifa letu.

Wasomaji wa kupitia njia mbalimbali za mitandao ya kijamii na baadhi ya magazeti, watakumbuka namna Mohamed alivyokuwa na mchango mkubwa katika kupigania chama kutokana na imani yake kubwa katika kupigania mabadiliko na kutoyumba.

Chama kinatoa pole kwa familia ya Ndugu Mohamed kwa kumpoteza baba, mmoja wa nguzo muhimu na mtu wa karibu katika maisha yao. Tunaomba Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi na kuwapatia moyo wa ujasiri katika wakati huu mgumu.

Aidha chama kinatoa salaam za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki wa Mohamed halikadhalika viongozi, wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na Watanzania wote walioguswa na msiba huo.
Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un.
Imetolewa leo Jumapili, Septemba 13 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.