MWENYEKITI
wa Chama cha National League for Democracy (NLD) ambaye pia ni mgombea ubunge
Jimbo la Masasi mkoani Mtwara, Dk. Emmanuel Makaidi amefariki dunia mchana huu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).
Mke wa marehemu, Modesta Makaidi,
amethibitisha kifo cha Dk. Makaidi akisema “kimetokea katika hospitali ya
Nyangao, kiasi cha saa 9 mchana.”
Modesta amesema walimpeleka hospitali
haraka Dk. Makaidi baada ya hali yake kubadilika ghafla nyumbani kwake mjini
Masasi wakati akijaandaa kutekeleza ratiba yake ya shughuli za kampeni ya
uchaguzi.
“Ni kweli Makaidi amefariki, kama dakika
45 zilizopita. Mimi ni mke wake naitwa Modesta Makaidi,” amesema alipopigiwa
simu na mwandishi wa habari hizi kuulizwa juu ya taarifa zilizopatikana awali
kuhusu hali ya Dk. Makaidi.
Modesta amesema “juzi wakati Makaidi
akiwa anaenda Kata ya Mbonde, ghafla alijisikia vibaya. Tukampeleka zahanati ya
Best ambako ikabainika ana presha kubwa. Akapewa dripu. Jioni akaruhusiwa. Leo
akaamka vizuri, lakini hali yake ikabadilika. Ndipo tukampeleka hospitali.”
Aidha, Khamis Hamad, Katibu Mwenezi na
msemaji wa NLD, ambaye awali alipopigiwasimu kuulizwa taarifa hizo alishtuka
akisema hakuwa na habari, alithibitisha kuwa tayari chama kimepokea taarifa na
kwamba walitarajia kufanya kikao jana kujadili namna ya kushiriki katika msiba
huo.
“Ni kweli, tumethibitisha kifo cha
Mwenyekiti wetu, Dk. Makaidi. Tunajiandaa kuelekea Ngome kufanya kikao pamoja
na vyama washirika wa Ukawa, na baadaye kwa familia yamarehemu Dk. Makaidi. Na
tutatoa taarifa kadri zitakavyopatikana,” amesema Khamis.
Dk. Makaidi aliteuliwa na Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA) kugombea ubunge jimbo la Masasi likiwa moja ya
majimbo matatu ambayo chama hicho kilipata katika mgao wa viti vya ubunge,
uliosimamiwa na muungano huo unaoshirikisha pia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Majimbo mengine ambayo NLD ilipewa
katika mgao wa maridhiano wa Ukawa ni Ndanda na Lulindi yote yakiwepo mkoani
Mtwara.
Hata hivyo, ugombeaji wake ulipata
kikwazo baada ya wananchi jimboni kumgomea.
Wananchi hao walitamka mbele ya mgombea
urais anayewakilisha Ukawa, Edward Lowassa kwamba chaguo lao ni Ismail Makombe
(Kundambanda), aliyeteuliwa na CUF kabla ya mgao wa majimbo kutangazwa.
Lowassa ambaye alipita Masasi wiki tatu
zilizopita kuomba ridhaa ya wananchi, alitoa fursa kwa wagombea wote wawili
kuhutubia wananchi kwenye mkutano huo na akawauliza ni yupi watakaemchagua,
wakajibu “tunamtaka Kundambanda.”
Dk. Makaidi aligoma hata Lowassa
alipotoa kauli kuwa angeachia uamuzi wa wananchi; aliondoka mkutanoni na
akashutumu alichoita mpango wa hujuma unaolenga kunufaisha adui zake Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Aliendelea kufanya kampeni na akaapa
kuendelea mpaka siku ya mwisho kwa kuwa anauhakika “nitaiangusha CCM.”
Dk. Makaidi aliungana na viongozi wakuu
wa vyama vya UKAWA tangu wakati wa Bunge Maalum la Katiba akiwa amepinga
mkakati wa CCM kuvuruga Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kutokana na maoni ya wananchi.
Wakati fulani Dk. Makaidi alisema wazi
kuwa ameamua kuungana na UKAWA kwa sababu anaamini Tanzania inahitaji
mabadiliko sasa.
Akiwa mmoja wa wenyeviti wenza wa umoja
huo, alijijengea umaarufu kwa hatua yake hiyo huku akitajika zaidi kwa
kaulimbiu ya chama chake ya “NLD motomoto moto.”
Siku ambayo Lowassa alitambulishwa rasmi
kujiunga na Chadema, katika salamu zake za pongezi, Dk. Makaidi alimwambia
Lowassa, “sasa umekuja huku kwetu itabidi utufuate sisi kwa haya
tunayoyapigania UKAWA, yale ya kule CCM uyaache kule.”
Kifo cha Dk. Makaidi kitasababisha
uchaguzi wa jimbo hilo kuhairishwa, na kjuwa jimbo la tano la ubunge uchaguzi
wake kuhairishwa baada ya wagombea kufariki. Majimbo hayo ni Lushoto mgombea
aliyefariki, Mohamed Mtoi (Chadema), Handeni Mjini mgombea Dk. Abdallah Kigoda
(CCM), Ulanga Mashariki mgombea ni Celina Kombani (CCM) na Arusha Mjini,
Estomih Malla (ACT).
|
No comments:
Post a Comment