CHAMA CHA DEMOKRASIA NA
MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amepokea kwa masikitiko
na majonzi makubwa taarifa za kifo cha mwanasiasa mkongwe katika siasa za
mageuzi nchini, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party, Mchungaji Christopher
Mtikila kilichotokea leo alfajiri kwa ajali ya gari.
Katika
salaam zake za pole kwa familia ya Mchungaji Mtikila, Katibu Mkuu wa DP,
viongozi na wanachama wa chama hicho kwa ujumla, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa
kifo cha Mchungaji Mtikila kimeacha pengo kubwa katika siasa za mageuzi nchini
hasa katika kupigania Tanganyika na suala la mgombea huru kuwa haki ya kikatiba
nchini.
“Mwenyekiti
wa DP Mtikila atakumbukwa kwa msimamo wake usioyumba katika mambo makubwa
mawili, kwanza kwa msimamo wake wa kuipigania Tanganyika kwa muda mrefu bila
kuchoka akitumia kila njia na majukwaa mbalimbali kujenga hoja za kudai
Tanganyika.
“Suala
jingine ambalo nalo pia alilipigania kwa ujasiri kisiasa na kisheria lilikuwa
ni agenda ya mgombea huru ili iwe mojawapo ya haki za msingi zinazotambulika
katika katiba yetu ya nchi.
“Ni jambo la
kusikitisha sana Mchungaji Mtikila ameaga dunia bila kuona mambo hayo makubwa
mawili yakitimia akingali hai. Ni imani yangu kuwa kizazi cha sasa ambacho
kinapigania mabadiliko katika nchi yetu hasa kupitia uchaguzi huu, kitajifunza
mengi kutoka kwa kiongozi huyo wa kisiasa na kuyaenzi yale yote mazuri
aliyoyapigania kuhakikisha yanatimia kwa manufaa ya Watanzania,” amesema
Mwenyekiti Mbowe na kuongeza;
“Kwa
masikitiko na majonzi makubwa natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa
na marafiki kwa kumpoteza mpendwa wao na moja ya guzo muhimu katika maisha.
Mwenyezi Mungu awasimamie na kuwatia nguvu katika wakati huu mgumu wa majonzi
katika kuukabili ukweli wa msiba huo mkubwa katika familia.
“Kwa niaba
ya viongozi wenzangu wa CHADEMA, wapenzi, wafuasi, mashabiki na wanachama wote
kwa ujumla, pia natoa pole na salaam za rambirambi kwa Katibu Mkuu wa DP kwa
niaba ya viongozi na wanachama wa chama hicho kwa kuondokewa na kiongozi wao
mkuu,” amesema Mwenyekiti Mbowe katika salaam zake.
Imetolewa leo Oktoba 4, 2015 na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment