Wednesday, October 28, 2015

TUME YATOA UFAFANUZI KUHUSU UCHELEWESHWAJI WA MATOKEO YA URAIS

1Na Beatrice Lyimo-Maelezo Dar es salaam.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji mstaafu Damian Lubuva ametoa ufafanuzi juu ya ucheleweshaji wa matokeo ya  awali ya ngazi Rais kutoka majimbo mbalimbali nchini.

Akitangaza matokeo hayo katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 27, 2015  jijini Dar es salaam Jaji Lubuva amesema kuwa Tume inasubiri matokeo hayo kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi kutoka katika majimbo yote nchini.

“waandishi wa habari mnatakiwa kuwa wavumilivu na kutangaza kile ambacho mnakisikia  na si kupotosha umma kwani Tume inatoa matokeo bila kupendelea chama chochote” aliongeza Jaji Lubuva.
Mbali na hayo jumla ya majimbo 87 yameshaleta majibu ya awali ya matokeo ya urais yakiwemo Mkoa wa Kusini Pemba Jimbo la Nchonga ambapo jumla ya wananchi 8,018 walijiandikisha, 5949 walipiga kura na kura halali zilikuwa 5771 ambayo ni asilimia 97.01 na 178.29 zilikataliwa.

Vilevile katika Jimbo la Chunguni waliojiandikisha walikuwa 13,416 ambapo wananchi 10,108 sawa na asilimia 75.34 walipiga kura, kura halali zilikuwa 9,792 sawa na asilimia 96.92 pamoja na kura 311 zilikataliwa ambayo ni sawa na asilimia 3.08.

Halikadhalika katika   Mkoa wa Mbeya Jimbo la Ileje jumla ya wananchi 56,002 walijiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ambapo asilimia 78.56 sawa na 43,997 walipiga kura, kati ya idadi hiyo kura 43,098 zilikuwa halali na kura 896 sawa na asalimia 2.04 zilikataliwa.

Jaji Lubuva aliongeza kuwa katika Jimbo la Ileje mkoani Mbeya ACT ilipata kura 501, ADC kura 347, CCM kura 26,368, CHADEMA kura 15, 651, CHAUMA walipata kura 155, NRA kura 26,TLP kura 36, pamoja na kura 20 kutoka chama cha UPDP.

Mbali na hayo majimbo mengine yaliyowakilisha matokeo hayo ni pamoja an Jimbo la Mtama kutoka Mkoa wa Lindi, Jimbo la Tunguu Mkoa wa kusini Unguja, Jimbo la kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, Jimbo la Nachingwea, Jimbo la mtama kutoka  mkoani Lindi, Jimbo la Mafia mkoani Pwani pamoja  Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani.

Pia Mkoa wa Katavi Jimbo la Mpanda vijijini, Mkoa wa Magharibi Mjini Jimbo la Fuoni, Jimbo la Kikwajuni, Jimbo la Mwera, Jimbo la Amani na Jimbo la Magomeni Mkoa wa Unguja Jimbo la Nungwi, Kaskazini Unguja Jimbo la Bumbwini, mkoa wa Rukwa Jimbo la nkasi kusini, Mkoa wa Kagera Jimbo la Nkenge na  Jimbo la Byalamuro, kutoka Mkoani Arusha Jimbo la Arusha Mjini yaliwakilisha matokeo yao.

Kwa upande wake Msaidizi wa  Mkurugenzi wa Uchaguzi Chadema Bwa. Matson Chizi  amesema kuwa mchakato mzima wa Uchaguzi ni mzuri wa wapo tayari kupokea matokeo hayo kwa jinsi yatakavyokuwa.

No comments: