Sunday, November 15, 2015

Kalamu ya Msaka Habari—KIFO CHA ALPHONCE MAWAZO NI JARIBIO LA KWANZA KWA SERIKALI MPYA YA DR MAGUFULI



Unaweza ukadhani kuwa watanzania wanaishi kwa furaha na upendo mkubwa kwa kuwatizama nyuso zao,lakini laiti kama kungekuwa na uwezo wa kupima mtanzania mmoja mmoja kutizama mioyo yao inawaza nini na kufikiria nini hakika tungeogopana hata kusalimiana kwa kuogopa kuwa lolote linaweza kutokea.

Siasa za Tanzania ni siasa ambazo tumeaminishwa kuwa ni siasa za kistaarabu na za kuheshimiana huku tukiongozwa na wimbo maarufu sana ambao watu wameanza kuchoka kuuimba wa TUITUNZE AMANI YETU,NA UMOJA WETU.Ni ukweli ulio waazi kuwa utambulisho mkubwa wa mtanzania popote alipo ni amani na mioyo yetu ya ukarimu tuliyopewa kama zawadi kutoka kwa mwenyezi mungu na tumekuwa tukiishi kwa misingi ya kuamini kuwa bado mioyo hiyo tunayo huku tukiwa hatujui tunawaza nini ndani yetu.

Tuachane na hayo ambayo nahisi hata nikiendelea kuyaeleza unaweza kukasirika na kuacha hata kusoma nilichokusudia kuandika kwa siku ya leo,ni wiki takribani mbili na zaidi zimekatika tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania ambao ulifanikiwa kutupatia watanzania Rais Mpya na wabunge pamoja na madiwani na nachukua nafasi hii kuwapongeza wale wote ambao walichaguliwa na kupata nafasi ya kuiongoza Tanzania bila kujali walioshindwa wanasemaje.

Tukiwa tunaongozwa na kauli mbiu ya KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI kauli ambayo kwa kuisikiliza kwa harakani kauli nikauli ambayo inatufanya watanzania tuendelee kujenga umoja wetu na undugu ambao umekuwa ni kama nembo ya mtanzania,lakini ukijaribu kuchambua maisha ya watanzania baada ya uchaguzi utagundua kuwa kauli mbiu hiyo kila mtu anaweza kuitumia kutokana na mazingira husika.


Tukiwa katika maisha baada ya uchaguzi siasa za Tanzania na vijana wa kitanzania wamepata pigo kubwa sana ambalo halikustahili kutokea katika kipindi hiki ambacho tunaamini uchaguzi wa Tanzania umemalizika kwa amani na tayari tumeanza kujenga umoja wetu ambao ulitoweka wakati wa uchaguzi.

Kwa watanzania wapenda siasa za harakati na watanzania wote hawawezi kushindwa kumfahamu ALPHONCE MAWAZO ambaye mbali na kuwa kiongozi wa CHADEMA mkoa wa GEITA pia amewahi kuwa kiongozi wa CCM na Diwani mkoani arusha hivyo imani yangu ni kwamba watanzania wote wameguswa na kifo cha mwanaharakati huyu.

Kinachosikitisha kwa sasa sio kifo cha Bwana MAWAZO ila kinachosikitisha wengi kwa sasa ni aina ya kifo alichokufa,unaweza ukajiuliza hivi Tanzania hii imekosa amani kiasi kwamba mtu unaweza kushambuliwa na watanzania wenzako mchana kweupe hadi wanakuondoa uhai wako na wanatokomea kusikojulikana.

Unaweza kujiuliza hivi Tanzania hii amani imetoweka kwa kiasi hiki hadi inafika mahali watanzania ambao tunaishi nao mitaani wanaweza kukuweka katikati na mapanga wakakukatakata hadi kukusababishia mauti na wakatoweka na baadae vyombo husika vikaja na taarifa ile ile ya uchunguzi unafanyika kuwabaini wahusika wimbo ambao umeimbwa tangu enzi za HAINES KIWIA NA WENJE,kuvamiwa mwanza,umeimbwa tangu enzi za DK ULIMBOKA umeimbwa tangu enzi za ABSALUM KIBANDA, umeimbwa kwa mwanahabari MWANGOSI hao wale na wengine ambao hata nikiwataja hapa ni kwazidishia watanzania machungu,bado tunasubiri uchunguzi wa kubaini wahusika.

Hivi watanzania hawa ambao tunawaaminisha kuwa wao ni watu wa amani na upendo waendelee kusubiri uchunguzi ufanyike juu ya kifo cha ALPHONCE MAWAZO ambaye watu wameshughudia akiuwawa na wananchi ambao kwa silaha za jadi,hivi watanzania hawa watakuwa na mioyo migumu kasi gani ili waendelee kuamini kuwa Tanzania kuna amani ilihali watu wamepoteza ndugu zao na wanaona kabisa hakuna haki iliyotendeka.

Nilipokua mdogo mtaani kwetu aliwahi kushambuliwa kiongozi Fulani wa moja kati ya vyombo vyetu vya usalama,nilichokishughudia kipindi hicho ni msaka mkoali ulioendeshwa mchana na usiku na walifanikiwa kiwakamata wote waliohusika na walipelekwa mahakani siku mbili baadae na sheria ilichukua mkondo wake,hivi hili la viongozi wetu wa kisiasa ambao wana umati mkubwa unaaowaamini inashindikanaje kufanyika jambo kama hili.

Watanzania wengi ukizngumza nao kuna baadhi ya maneno wamechoka kuyasikia,mfano uchgunguzi unaendelea,watu wasiojulikana,kesi ipo Mahakamani,ameachiwa kwa dhamana,hakimu wa kesi anaumwa hivyo imesogezwa mbele,na maneno mengine ambayo yamekuwa yakitokea baada ya matukio makubwa kama haya kutokea na mwisho wa siku picha inamalizika kama filamu isiyokuwa na muongozaji.

Nasema haya kama tahadhari nikiwa nina imani kubwa sana na serikali mpya kuwa inaweza ikaja na majibu ya matatizo haya ambayo kama yakiachiwa yaendelee kutokea na tukaendelea kuwapumbaza watanzanian na wimbo wa AMANI YETU historia itatuhukumu,hili la GEITA sio tukio la kwanza kuondoka na roho ya mtu bila sababu yoyote na vyombo husika vikanyamaza.

Jeshi la polisi hili ni jaribio la kwanza pamoja na serikali ya Rais wetu mpya Docta JOHN MAGUFULI,hapa ndipo tunapotaka kuona serikali ikitenda haki na sio tu kutenda haki lakini haki yenyee ionekane ikitendeka,tunaimani sana na serikali yetu mpya na tunaimani na utendaji kazi wa kiongozi wetu wa nchi,nimeamua kumuomba ombi maalumu awarudishe watanzania katika umoja wao kwa kuhakikisha kuwa hili la Kuuawa kwa mwenyekiti wa CHADEMA huko GEITA rafiki wa watanzania ALPHONCE MAWAZO linakuwa ni mfano na wahusika wote wanatiwa mikononi mwa polisi na haki ionekane ikitendeka.
ASANTENI.

R.I.P ALPHONCE MAWAZO

No comments: