Tuesday, November 17, 2015

SERIKALI KUBORESHA HUDUMA YA MAJI KWA WAKAZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM.

indexKaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Maji Bw. Athumani Sharif akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mikakati ya Serikali kutatua tatizo la upatikanaji wa maji jijini Dar es Salaam mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha na Fatma Salum.)
…………………………………………………………………………………………..

Na. Georgina Misama – Maelezo
Serikali inatarajia kuzalisha maji lita milioni 270 kwa siku baada ya kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa Chanzo cha Maji cha Ruvu Chini na upanuzi wa mtambo wa kusafishia maji.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimarekani la Millenium Challenge Co-operation umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 66.24 na unatarajiwa kukamilika wakati wowote baada ya kukamilika kwa kazi ya kulaza bomba linalosafirisha maji toka Ruvu chini kuja Jijini Dar es Salaam.
Akiongea na waandishi wa habari, leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Maji, Bw. Shariff Athumani amesema kwamba mradi wa upanuzi wa mtambo wa ujenzi wa bomba la Ruvu Chini utapunguza kero ya maji kwa wakazi wote wanaotumia maji kutoka Ruvu Chini.
Akiyataja maeneo yatakayofaidika na kukamilika kwa mradi huo ni pamoja na Bagamoyo na vitongoji vyake, Bunju, Mabwepande, Boko, Tegeta Kunduchi na Mbezi Beach. Maeneo mengine ni pamoja na Mbezi Juu, Salasala, Kawe, Makongo, Chuo Kikuu, Mikocheni, Msasani, Masaki, Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni, Sinza, Manzese, Ubungo, Mabibo, Kigogo, Buguruni, Ilala, Kurasini, Bandarini na maeneo yote ya katikati ya jiji la Dar es Salaam.

No comments: