Monday, November 23, 2015

Ufafanuzi wa Ziada kuhusu maadhimisho ya Uhuru Na maamuzi ya Rais

Kwa mujibu wa  Sheria ya Sikukuu za Kitaifa  (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike  kwa kufanya kazi.  Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu  (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu.  Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.
Aidha, kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi,  fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.
Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo,   sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
23 Novemba, 2015

No comments: