Friday, December 11, 2015

Najua Hujazinasa Hizi Kutoka kwa Kamishna Kova leo,Soma


 

WAKAGUZI WA POLISI 07 PAMOJA NA ASKARI WA VYEO MBALIMBALI 157 JUMLA 164 WA POLISI KANDA MAALUM  DAR ES SALAA WABADILISHWA KITENGO CHA USALAMA BARABARANI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewabadilisha kazi wakaguzi 07 na askari wa vyeo mbalimbali 157 wa kikosi cha Usalama barabarani ambao utendaji wao umekosa tija. Uamuzi wa kuwabadilisha askari hao kutoka kikosi cha usalama barabarani kwenda kazi nyingine mbalimbali za kawaida umetokana na ufuatiliaji wa muda mrefu wa tabia na mwenendo wa askari hao wakati wa utendaji wao wa kazi.

Utendaji wao umeonekana sio wa kuridhisha ndiyo maana baadhi yao wamekuwa wakilalamikiwa mara kwa mara na wananchi. Aidha makamanda wa Mikoa yote ya Polisi mkoa wa Dar es Salaam ya ILALA, KINONDONI na TEMEKE wametakiwa kufuatilia kwa makini tabia na mienendo ya askari walio chini yao ili kuhakikisha kwamba hazijitokezi kero dhidi ya wananchi na kinachotakiwa ni huduma nzuri zitakazolifanya Jeshi la Polisi lionekane kwamba linatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia weledi na ufanisi wa hali ya juu.

Kubadilishwa askari hao ni hatua ya kwanza kwani bado uchunguzi zaidi unafanyika kwa wale ambao wataendelea kufanya kazi chini ya kiwango. Aidha askari ambao watabainika wamejihusisha ma makosa ya moja kwa moja ya jinai kama vile kujihahusisha na vitendo vya rushwa au ukiukwaji wa maadili ya Jeshi la Polisi watashtakiwa katika mahakama za kijeshi au za kawaida kwa makosa yatakayothibitishwa.
Uchunguzi zaidi unaendelea kuhusu vikosi vingine vya Kanda Maalum na Jeshi la Polisi kwa jumla ili kubaini kama kuna askari, Mkaguzi au Afisa anayefanya kazi chini ya kiwango, bila tija katika utendaji au anafanya kazi katika kiwango kisichoridhisha na analalamikiwa, nao watachukuliwa hatua kama hizi au nyingine za kisheria.

Watendaji wote wa Jeshi la Polisi wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii na weledi wa hali ya juu ili kuwahakikishia wananchi kwamba wananufaika kutokana na utendaji wa Jeshi la Polisi na kulifanya jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla pawe mahali salama pa kuishi.

WAHAMIAJI HARAMU 105 WAKAMATWA KWA KUINGIA NCHINI BILA KIBALI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam asubuhi ya leo 26/11/2015 limewakamata wahamiaji haramu wapatao 105 huko Tabata Segerea Ilala jijini Dar es Salaam. Baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa huko maeneo ya Tabata Segerea kuna nyumba ina wahamiaji haramu, Polisi walizunguka nyumba hiyo tangu alfajiri ya leo na hatimaye kwa kutumia utaratibu wa kisheria nyumba hiyo ilipekuliwa ndipo walipokutwa watu hao 105 wanaume na iligundulika kwamba wanatoka nchini Ethiopia.

Watuhumiwa wote walihojiwa kuhusu vibali vya kuingia nchini na kukutwa hawana ndipo ilipogundulika waliingia kupitia njia za panya au kwa mbinu ambazo bado zinachunguzwa.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba watu hawa walikuwa chini ya usimamizi wa mtu mmoja aitwaye ZABIBU D/O UMWIZA, Miaka 25, anayesemekana ni raia wa Burundi anayejihusisha na biashara ya usafirishaji wa binadamu kutoka nchi za Afrika kwenda Ulaya kwa malipo yanayosemekana kufikia US Dolla 1000 kwa mtu mmoja. Kutokana na tukio hili jinsi lilivyo tumewajulisha idara ya uhamiaji na tunashirikiana nao katika upelelezi ili hatimaye sheria ichukiue mkondo wake.

Tunawaomba wananchi washirikiane na Jeshi la Polisi katika kuzuia makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na hili la wahamiaji haramu ambao wanaweza kuwa tishio kwa usalama wa maisha ya wananchi na hata kwa uchumi wa taifa.

KUKAMATWA KWA SILAHA SMG MOJA, BASTOLA NNE, JUMLA YA RISASI 36 PAMOJA NA WATUHUMIWA 13.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na oparesheni kali ya kuwasaka kuwakamata wahalifu wa aina zote na kuhakikisha hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.

Katika oparesheni hiyo Jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 13 kwa tuhuma za makosa mbalimbali yakiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, unyang’anyi wa kutumia nguvu, wanaojihusisha na mitandao ya kigaidi pamoja na makosa mengine. Watuhumiwa hao wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kufuatia ushirikiano toka kwa wananchi.

Pia oparesheni hiyo imefanikisha kukamatwa kwa bunduki moja CHINESE 56 (SMG) iliyofutwa namba zake, bastola tatu ambapo mbili ni aina ya BERETA na bastola moja aina ya CHINESE zote zikiwa zimefutwa namba zake. Aidha zimekamatwa jumla ya risasi 36 katika mchanganuo ufuatao: risasi za SMG zipo 08, risasi za bastola zipo 13, na risasi za shotgun zipo 15. Aidha wamekamatwa jumla ya watuhumiwa 30 kuhusiana na matukio haya ambapo upelelezi unaendelea ili hatua kali dhidi yao ziweze kuchukuliwa.

POLISI KANDA MAALUM DAR ES SALAAM YATOA ONYO KALI KWA WENYE TABIA YA KUJICHUKULIA SHERIA MIKONONI. WATUHUMIWA 49 WASHIKILIWA NA KADHAA WAFIKISHWA MAHAKAMANI.

        Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linawashikilia watu 31 kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi katika matukio tofauti yaliyosababisha vifo, majeruhi, na uharibifu wa mali kwa baadhi ya watu. Hii ni tabia iliyoanza kuota mizizi jijini Dar es Salaam na mikoa mingine ambayo pia ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Katika tukio la kwanza mnamo tarehe 27/10/2015 huko maeneo ya SUKITA Buguruni, Ilala jijini Dar es Salaam walikamatwa watu 27 kwa tuhuma a kujichukulia sheria mikononi baada ya kumshambulia mtu mmoja jina halijafamika kwa kumpiga mawe sehemu mbalimbali za mwili kisha kumchoma moto lakini aliokolewa na askari waliokuwa doria.

Katika kuwatafuta wahusika, alikamatwa mtuhumiwa ELIUD S/O ELIA MWAKISUNGA @ MAJANI na wenzake 27. Aidha, watuhumiwa 08 kati ya waliokamatwa wametambuliwa kuhusika na tukio hilo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote.
Katika tukio lingine Jeshi la Polisi kanda Maalum linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumshambulia mtu mmoja aliyejulikana kwa jina maarufu la “Kinjunga”, miaka 27, mkazi wa Somangila, Temeke jijini dare s Salaam.

Tukio hilo lililotokea tarehe 21/11/2015 huko Malimbika kata ya Somangila, wilaya ya Kigamboni, Temeke jijini Dar es Salaam ambapo watu hao wanadaiwa kumshambulia na kumpiga kwa fimbo na mawe hadi kufa na kisha kumchoma moto baada ya kumtuhumu kutaka kumpora abiria mmoja aliyekuwa akiteremka kutoka katika daladala ambalo halikusomeka namba zake mara moja.

Taarifa za awali zinasema marehemu alikuwa na wenzake  wakitumia pikipiki ambayo pia haikusomeka namba yake na KINJUNGA alishuka na kujaribu kumpota abiria huyo aliyepiga kelele ndipo watu walimvamia na kumpiga hadi kumuua. Katika tukio hilo watuhumiwa kadhaa wamekamatwa ambao ni:

1.    RUDOVICK S/O VINCENT, Miaka 27, Mkazi wa Malimbika Somangila.
2.  JOHN S/O SALUM, Miaka 36, Mkazi wa Malimbika Somangila.
3. MOHAMED S/O SALUM, Miaka 36, Mkazi wa Malimbika Somangila.
Katika tukio lingine, tarehe 27/10/2015 majira ya saa07:20 huko mtaa wa Sandali, Temeke walikamatwa  watuhumiwa 08 wanaosadikiwa ni wafuasi wa chama fulani cha siasa kwa tuhuma za kuchoma moto ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Sandali na kuteketeza maboksi yaliyokuwa na matokeo ya kura za udiwani. Watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani.
Majina ya watuhumiwa hao ni kama ifuatavyo:

1.    SHABANI S/O ABDALLAH @ POLLOMO, Miaka 40, Mkazi wa Temeke.
2.  SALIM S/O ABDALLAH NGUNDA, Miaka 27, Mfanyabiashara , Mkazi wa Mbagala Charambe.
3.  RAJAB S/O OMARY, Miaka 25, Mwanafunzi, Mkazi wa Temeke Mikoroshini.
4.  SEIPA S/O RAMADHANI KANIKI, Miaka 38, Mkazi wa Temeke Mikoroshini.
5.  OMARY S/O JUMA BOMEZA, Miaka 56,  Mfanyabiashara, Mkazi wa Temeke Sandali.
6.  MARIAM D/O SIFA, Miaka 51, Mkazi wa Temeke Mikoroshini.
7.  BONIPHASI S/O RAYMOND, Miaka 30, Mfanyabiashara, Mkazi wa Temeke Maganga.
8.  NORBERT S/O RAYMOND, Miaka 26, Mfanyabiashara, Mkazi wa Temeke Maganga.

Aidha, Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa watu au kundi la watu wenye tabia ya aina hii kuacha mara moja kwani ni vitendo vya kihuni, kikatili na havikubaliki katika jamii ya watanzania. Pia, vitendo hivi ni kinyume cha sheria za nchi yetu na kinyume cha haki za binadamu. Kikundi au mtu yeyote atakayekamatwa kuhusiana na tuhuma za aina hii atachukuliwa hatua kali za kisheria bila ajizi.


S. H. KOVA

KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

No comments: