Friday, December 18, 2015

Wakulima wa Korosho Mtwara Wamtaka Rais Magufuli Kuivunja Bodi Ya Korosho Tanzania,kutokana na kutowasaidia

Picha na Maktaba
                                         Haika Kimaro
Masasi.Wakulima wa zao la korosho jimbo la Ndanda wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara wamemwomba rais John Magufuli kuivunja bodo kuu ya Korosho nchini (CBT) kwa madai kuwa imekuwa haiwatetei wakulima na badala yake inawakumbatia wachache wenye maslahi binafsi kwa kisingizio cha mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuwanyonya.



Wamesema kuwa bodi kwa kushirikina na wadau wamekuwa wakiwapanga bei elekezi ya zao la korosho kila msimu na kuwataka kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani lakini wamekuwa hawapewi pesa zao kwa wakati licha ya kuwa kwenye midada huuzwa kwa bei ya juu zaidi ya elekezi.

Sebastian Mrope mkazi wa kijiji cha Msabaa alisema kuwa wamekuwa wakikatazwa kuuza mazao yao na kutakiwa kuyakusanya kupitia vyama vya ushirika kwaajili ya kupelekwa maghalani kwaajili yam nada lakini yanapouzwa hupewa bei nusu nusu.

“ Tunamwomba rais wa awamu ya tano kuivunja bodi ya korosho kwasababu haiko kwa maslahi ya wakulima bodi kwa kushirikiana na wadau hupanga bei elekezi na kwa msimu huu ilikuwa Sh 1,200 kwa kilo lakini tunapopeleka mazao yetu maghalani na kuuzwa kwa mnada tunapatiwa Sh 1,000 na 200 ni majaliwa lakini tunajua inauzwa bei juu zaidi ya hiyo,”alisema Mrope

Naye Mzee hassani alisema wamekuwa wakikusanya mazao yao kwenye maghala kwa kuamini bodi inayowasimamia lakini korosho zao zimekuwa zikiibiwa na kuamabulia hasara pasipo wahusika kuchukuliwa hatua.

“Wakulima hatuoni sababu ya uwepo wa bodi,tunaomba kuwe na soko huru la korosho kama ilivyo kwa mazao mengine kwani tunapokusanya korosho zetu maghalani zinapotea pasipo sisi kulipwa wala wahusika kuwajibishwa,”alisema Hassani

Akizungumza mbunge wa jimbo la Ndanda Cecil Mwambe alisema tayari amepokea malalamiko toka kwa wakulima wa zao hilo na kuwa tayari anaandaa hoja kupinga zao hilo kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwani inakuwa haisaidii wakulima.

Aidha alisema wakulima wamekuwa wakitumia gharama kubwa kuzalisha lakini bado wanapangiwa bei ambayo hata hivyo hawaipati kwa wakati na kuwa vyama vya  msingi na ushirika vimekuwa na vyeo vya kugombea lakini hawasaidii wakulima.

“Hii ni nchi yetu wote lazima kila mmoja anufaike na kile anafanya wakulima wanazalisha wenyewe kwa gharama zao lakini bado wanapangiwa bei na pesa zao zinapita kwenye mikono mingi mimi nitaandaa hoja kuupinga mfumo wa stakabadhi ghalani na ninamwomba rais aivunje bodi ya korosho kwasababu wakulima hawaoni sababu ya kuendelea kuwepo,”alisema Mwambe

Hata hivyo alikiri kupokea taarifa za kupotea kwa korosho tani 103 katika msimu wa mwaka 2014/2015 katika ghalala Buco Masasi na kuahidi kulifanyia kazi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa bodi ya korosho, Mfaume juma alisema bei ya korosho kwa msimu wa mwaka 2015/2016 kilo moja katika minada inauzwa kati ya Sh 2400 hadi 2900 lakini kwa baadhi ya wakulima wa wilaya ya Masasi wameuza kati ya 1000 na 1,200 kwa kilo licha ya kuwa wanatumia mfumo wa stakabadhi ghalani.

No comments: