Monday, February 22, 2016

KOMBE LA SHIRIKISHO KUENDELEA WIKI HII


Michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) inatarajiwa kuendelea wiki hii mzunguko wa nne katika hatua ya 16 bora, kwa michezo nane kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini.

Jumatano Februari 24, 2016 kutakua na mchezo mmoja tu, ambapo timu ya Young Africans watawakaribisha maafande wa JKT Mlale kutoka mkoani Ruvuma katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, mchezo utakaochezwa majira ya saa 10:30 jioni.
Michezo miwili itachezwa siku ya Ijumaa ambapo, Ndanda FC watakua wenyeji wa JKT Ruvu katika uwanja wa Nagwanda Sijaon mjini Mtwara, huku Coastal Union wakiwakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Jumamosi Februari 27, Mwadui FC watawakaribisha maafande wa Rhino Rangers katika uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga, wakati jijini Mbeya Tanzania Prisons watacheza dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Sokoine jijini humo.
Mzunguko huo wa nne utakamilika siku ya Jumapili ambapo, Simba SC watawakaribisha Singida United katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Panone FC dhidi ya Azam FC uwanja wa Ushirika mjini Moshi, huku Toto Africans wakicheza dhidi ya Geita Gold katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
NB: Rais wa TFF, Jamal Malinzi kesho Jumanne saa 5 kamili asubuhi, ataongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume.

No comments: