.

SERIKALI IMEWATAKA WANANCHI KUYATUNZA MAENEO YENYE ARDHI OEVU.

1
Afisa Wanyamapori kutoka Wizara ya Mali Asili na Utalii Bw.Sadick Lotha akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu maadhimisho ya siku ya ardhi oevu Duniani inayotarajiwa kufanyika februari 2,2016 ambapo siku hiyo itatumika kutoa elimu kwa kuwakumbusha watu kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za ardhi oevu. Kulia ni Afisa Habari wa Wizara hiyo Bw. Lusungu Helela, kushoto ni Afisa Wanyamapori Mkuu na Mratibu Kitaifa wa Uhifadhi Ardhi Oevu Bw. Pellage Kauzeni.
2
Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Mali Asili na Utalii Bw. Pellage Kauzeni akitoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya ardhi oevu kushirikiana na Serikali katika kuyatunza maeneo hayo kushoto ni Afisa Wanyamapori kutoka Wizara ya Mali Asili na Utalii Bw.Sadick Lotha na kulia ni Afisa Habari wa wizara hiyo Bw. Lusungu Helela.
3
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatlia mkutano wa Wizara ya Mali Asili na Utalii uliolenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maadhimisho ya siku ya ardhioevu ambayo huzuia mmomonyoko wa udongo kwenye fukwe unaoweza kusababishwa na mawimbi ya bahari.
( Picha zote na Frank Mvungi )

………………………………………………………………………………..
Na Fatma Salum-Maelezo
Serikali imewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yenye ardhi oevu kushiriki katika kuyatunza maeneo hayo ili waweze kunufaika na rasilimali zinazotokana na uwepo wa maeneo hayo.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar Es Salaam na Afisa Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Sadiki Lotha wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
“Ardhi oevu husaidia upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mimea na wanyama hivyo vyanzo vyake havina budi kulindwa kwa kuepuka shughuli zinazopelekea kuathiri vyanzo hivyo.” Alisema Bw. Lotha.
Akizitaja baadhi ya shughuli zinazoathiri ardh ioevu Bw. Lotha alisema ni ufugaji holela, ujenzi kwenye vyanzo vya maji, kilimo na ukataji wa miti ovyo.
Naye Mratibu wa Kitaifa wa Uhifadhi wa ardhi oevu Bw. Pellage Kauzeni alisema kuwa uharibifu wa ardhi oevu hupelekea athari katika sekta ya uvuvi, utalii, kilimo cha umwagiliaji na ufugaji hivyo kuharibu bioanwai, uchumi, shughuli za kijamii na kiikolojia.
Aidha Bw. Kauzeni alisema Tanzania imeridhia makubaliano ya kimataifa ya mkataba wa Ramsar kuwa ndio msingi wa usimamizi na matumizi endelevu ya ardhi oevu duniani uliosainiwa na nchi wanachama mjini Ramsar nchini Iran mwaka 1971.
Siku ya Ardhi Oevu duniani itafanyika kesho tarehe 2 Februari, 2016 ikiwa na kaulimbiu “MAISHA YA KIPATO ENDELEVU”.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.