Mkuu wa Kitengo Cha Utafiti na Ubora wa Mifumo Bw. Benny Mallya kutoka Ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu utekelezaji wa sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali sura 182 ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kwa wasafirishaji na watumiaji wa kemikali hapa nchini. Kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Frank Mvungi na kulia ni Afisa Habari wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bw. Sylvester Omari.
Mkuu wa Kitengo Cha Utafiti na Ubora wa Mifumo Bw. Benny Mallya kutoka Ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo kutoa mafunzo kwa wasimamizi 61 wa shughuli za usafirishaji wa kemikali na madereva 123 hapa nchini. Kulia ni Afisa Habari wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bw. Sylvester Omari.
…………………………………………………………………………………………………….
Frank Mvungi-Maelezo
Serikali itatoa mafunzo kwa wasimamizi 61 wa shughuli za Kemikali na madereva 123 wanaosafirisha Kemikali mbalimbali ili kuzuia athari zinazotokana na matumizi yasiyozingatia sheria na kanuni za kemikali.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano na vyombo vya habari Mkuu wa Kitengo Cha Utafiti na ubora wa Mifumo Bw. Benny Mallya kutoka Ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani sura 182.
Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 matukio ya kemikali yalisababisha vifo 14.
“Jumla ya matukio 11 ya ajali za Kemikali yalitolewa taarifa katika kipindi cha mwaka jana pekee na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali ikiwemo kuungua moto magari na tani 250 za kemikali”.alisisitiza Mallya.
Akifafanua kuhusu matukio hayo Mallya amesema kuwa ajali hizo zilisababishwa na kukosekana kwa uelewa juu ya athari zinazoweza kusababishwa na kemikali hizo miongoni mwa wasafirishaji na watumiaji.
Kama sehemu ya utekelezaji wa sheria hii,Serikali inatarajia kuendelea kufanya mafunzo ya wadau kuhusiana na kemikali zenye kusababisha mlipuko.
Mafunzo hayo yatatolewa kwa wakuu wa polisi wa Usalama barabarani nchi nzima yanalenga kuongeza uelewa kwa wadau wanaohusika katik a kutumia na kusafirisha kemikali ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza.
Katika kukabiliana na madhara yatokanayo na matumizi yasiliyo salama,ajali na matukio ya kemikali,Serikali iliamua kutunga sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani sura 182 (The Industrial and Consumer Chemicals Management and Control) Act Capt 182).
Lengo kuu la sheria hii ni kuhakikisha kuwa kemikali zinatumika katika hali iliyo salama bila kuleta athari kwa watu na mazingira.
No comments:
Post a Comment