Monday, June 6, 2016

Lowasa atuma salamu za mwezi wa Ramadhani huku akiwapa watanzania maneno mazito,yasome hapa

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewatakia waumini wa dini ya Kiislamu nchini, Mfungo mwema wa Ramadhan.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana ilisema: "Kwa niaba ya mke wangu, Regina na mimi binafsi, nachukua nafasi hii kuwatakia Waislamu wote nchini kila la kheri na baraka tele kwenye mwezi huu."
Hata hivyo, Lowassa alisema ansononeshwa na hali ya maisha ya Watanzania nchini hivi sasa inavyozidi kuwa ngumu.

"Bei za bidhaa mbalimbali zimezidi kupanda na zaidi kuadimika kwa sukari ambayo ni bidhaa muhimu sana hasa katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan," alisema Lowassa ambaye pia alikuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Lowassa amewaomba wafanyabiashara kupunguza bei ya bidhaa hususan zile muhimu katika mwezi huu Waislamu watimize ibada yao vizuri.

Aidha, amewaomba waumini wa dini ya Kiislamu, kuutumia mwezi huu kuliombea taifa amani, upendo na mshikamano.
Waumini wa dini ya Kiislamu nchini, wanaungana na wenzao kote duniani katika kutimiza moja ya nguzo tano za Uislamu kufunga Ramadhan. 
"Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan, ni kipindi muhimu sana kwa Waislamu kuwa karibu na Mola wao," taarifa ilisema.

Aidha, Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, katika taarifa yake hiyo alisema anaomba haki na hamu ya Watanzania kuona mabadiliko ya kisiasa yanafanyika kwa amani na wale wenye ulevi wa kuminya haki hiyo, hawapati tena nafasi na kuwaombea viongozi ili wawe na hofu ya Mungu.

No comments: