Friday, June 3, 2016

SERIKALI YA MTAKIA USHINDI MELISA

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka
Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Leah Kihimbi (kulia) akimkabidhi
Bendera ya Taifa kwa mshindi wa Airtel Trace Music Stars Tanzania Bi. Melisa
John (kushoto) leo Jijini Dar es Salaam anayetarajia kwenda nchini Nigeria
kushiriki michuano ya shindano hilo kwa nchi za Afrika,wa pili kushoto ni
Meneja Mahusiano Airtel Bw.Jackson Mmbando.
 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Leah Kihimbi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam,wakati wa kumuaga mshindi wa shindano la Airtel Trace Music Stars Tanzania  Bi. Melisa John (kulia) anayetarajia kushiriki
mashindano hayo  nchini Nigeria Juni 11mwaka huu litakaloshirikisha nchi za tisa za Afrika (kushoto) Meneja Mahusiano Airtel Jackson Mmbando . 
 
Meneja Mahusiano Airtel Jackson Mmbando akizungumza na waandishi wa habari kuhusu dhamira ya Airtel ya kuwawezesha Vijana katika sanaa ya muziki leo Jijini Dar es Salaam,(katikati) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Leah Kihimbi na (kulia) mshindi wa shindano la Airtel Trace Music Stars Tanzania Bi. Melisa
John.
 
Mshindi wa Shindano la Airtel Trace Music Stars Tanzania Bi. Melisa John (kulia) akiimba moja ya  nyimbo kwa waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam  (hawapo picha)  alipokuwa akiagwa na kukabidhiwa bendera ya Taifa kwa ajili ya kuwakilisha nchi katika mashindano yanayotarajiwa kufanyika nchini Nigeria Juni 11 mwaka huu, (katikati) Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Leah Kihimbi na (kushoto) Meneja Mahusiano Airtel Jackson Mmbando akifurahia wimbo huo.( Picha na Anitha Jonas).
 
Na Lorietha Laurence
Taasisi na Mashirika binafsi nchini zimeombwa kushirikiana na serikali  katika  kutekeleza sera ya Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997 inayosisitiza kukuza na kuendeleza sanaa na wasanii  kwa lengo la  kuinua vipaji na kutimiza ndoto za vijana wengi wanajihusisha na sanaa.
 
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi. Leah Kihimbi wakati wa kukabidhi bendera ya Taifa kwa mshindi wa Airtel Trace Music Star Bi. Melisa John ambaye ataiwakilisha nchi katika mashindano ya Airtel Afrika nchini Nigeria.
 
Bi.Kihimbi ameleeza kuwa fursa inayotolewa na Kampuni ya Airtel ni adhimu na mfano tosha kwa makampuni, taasisi na mashiriki mengine nchini kuunga mkono juhudi hizo kwa kuanzisha program za kuwakwamua vijana kiuchumi kupitia sanaa ya muziki.
 
“Sanaa ya muziki ni kazi kama kazi nyingine,hivyo nashukuru kampuni ya Airtel  kwa kuamua kuunga mkono serikali katika mpango huu wa kuibua vipaji vya vijana  kupitia sanaa ya muziki” alisema Bi.Kihimbi.
 
Aidha aliongeza kuwa nafasi aliyoipata Melisa ni adhimu hivyo haina budi kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuikuza talanta yake  ya kuimba na hatimaye kukua kimuziki na kuweza kuitangaza nchini kitaifa na kimataifa.
 
Naye Meneja Uhusiano wa Airtel Jackson Mmbando amesema kuwa kampuni yao ipo tayari kuendelea kuwekeza katika sanaa kwa kuwawezesha vijana pamoja na wanamuziki chipukizi kuweza kufikia ndoto zao kupitia Airtel Trace Music Star.
“Tunafurahi kuwawezesha wanamuziki chipukizi vijana kupata nafasi adimu za kufanya kazi na magwiji wa muziki duniani kama Akon na Keri Hilson hivyo tunaomba watanzania watumie fursa
hii kwa kushiriki katika mashindano ya Airtel Trace Music Star ili waweze kukuza vipaji vyao”alisema Bw. Mmbando.
Kwa upande wake mshindi wa Airtel Trace Music Star Bi.Melisa John ameishukuru Serikali na Airtel kwa ushirikiano wao katika kukuza tasnia ya muziki na kuchochea ajira kwa vijana
wengi na kuahidi kurudi na ushindi.
Shindano la Airtel Trace Music Star Kitaifa yalifanyika jijini Dar es Salaam ambapo Bi.Melisa John aliibuka mshindi na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo kimataifa yatakayoshirikisha nchi tisa ambazo ni Niger,DRCongo,Gabon,Malawi,Nigeria,Madagascar,Kenya,Zambia na Ghana yanayotarajiwa kufanyika nchini Nigeria Juni 11 mwaka huu. 

No comments: