Saturday, August 13, 2016

Vyama 10 Vya Upinzani Vyaungana Kuupinga UKUTA Wa Chadema


VIONGOZI wa vyama vya siasa wanaounda Klabu ya Viongozi wamesema hawaungi mkono maandamano yaliyopangwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika kulinda amani ya nchi.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fahmi Dovutwa alisema uamuzi wa kutounga maandamano hayo imefikiwa kwenye kikao cha viongozi wa vyama wa siasa wa klabu hiyo waliokutana jana kujadili hali ya siasa nchini.
“Vyama vya siasa tumekutana leo (jana) ili kufanya tafakari juu ya hali ya siasa nchini hususan tamko la Chadema la kufanya maandamano na hatimaye mikutano sehemu mbalimbali. Pia tumezingatia tamko lililotolewa na Serikali na Rais John Magufuli la kutaka amani ya nchi idumishwe, hivyo hatuungi mkono maandamano,” alisema.
Alisema pamoja na kutounga mkono, viongozi hao wanataka kufanyika kwa mkutano ambao utashirikisha vyama vyote vya siasa nchini ili kupata muafaka ambao utaepusha nchi kuingia katika malumbano na misuguano.
“Tarehe waliyopanga kufanya hayo maandamano ni maadhimisho ya Siku ya Majeshi Duniani kote, hivyo wanajeshi watakuwa na shughuli zao ambazo zinaweza kuleta taswira ya jeshi kuingilia maandamano, lakini jambo la msingi ni kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa vyama vyote,” alisema Dovutwa.
Vyama vilivyohudhuria mkutano huo ni Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Alliance For Tanzania Farmers Party (AFP), Chama cha Democratic (DP), D-Makini, JAHAZI Asilia, Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), United Peoples Democratic Party (UPDP), ADA-TADEA na Chama Cha Kijamii (CCK).
Hivi karibuni, Chadema ilitoa tamko la kufanya maandamano na mikutano nchi nzima katika kampeni waliyoiita Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA).
Azma ya Chadema inakuja baada ya siku kadhaa za Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano kwa sababu za kiusalama.
Hata hivyo, Rais Magufuli alipiga marufuku maandamano hayo kwa lengo la kutaka amani ya nchi idumishwe na kuelekeza mikutano ya hadhara ya wabunge walioshinda ifanywe kwenye majimbo yao.

No comments: