Friday, September 16, 2016

Kubwa leo--Taarifa nzima ya walinzi wa Lipumba Kufanya jaribio la kuteka Viongozi wa CUF leo Asubuhi

WALINZI WA PROF LIPUMBA WAANZA UTEKAJI WA VIONGOZI WA CUF.
Leo majira ya 2:30 asubuhi vijana wa Prof Lipumba wamefanya jaribio la kutaka kumteka MKURUGENZI WA UCHUMI NA FEDHA WA CUF ambaye ni K/NAIBU MKUU CUF BARA Mhe. Joran Bashange wakati akitoka nyumbani kwake eneo la Buguruni. Watekeji hao wakiwa na gari aina ya Noah yenye namba ya Usajili T 760 CEX (pichani).
Baada ya jaribio la kumteka, walifanikiwa kumuingiza katika gari hiyo ya NOAH iliyokuwa na vioo TINTED. Bashange alipambana na kuomba msaada kwa kuita watu waliojirani kwa yowee la kuita "Majambazi" ndipo wananchi wakalizingira gari hilo na kuweka mawe na magogo na Polisi wakaitwa.

Polisi walipofika wakawakagua vijana hao na kuwakuta na pingu na silaha kadhaa na kitambulisho feki cha polisi.
Vijana watatu wamekamatwa na mmoja amefanikiwa kukimbia. 

Mmoja kati ya vijana waliokamatwa ni mlinzi wa karibu wa Prof. Lipumba aitwaye HAJI "Mrangi" ambaye ni maarufu anajulikana kwa ushiriki wake wa vitendo vya kihuni na kiharamia kama hivi.
Katika mahojiano ya awali mmoja wa vijana hao ametoa ushirikiano na kueleza kuwa wametumwa na Abdul Kambaya na kuwa anayeongoza oparesheni yao hiyo ni mtu aitwaye Athumani (Mganga wa Kienyeji na Mwalimu wa mafunzo ya Kareti) aishiye Ilala akisaidiwa na watu wengine wanaojulikana Abubakar Fambo, Mohamed Ibrahim na Hassan Kingwele ( Mlinzi wa Magdalena Sakaya (MB).

Vijana hao waliokamatwa wanakiri kuwa mipango yote hiyo Prof. Lipumba anaijua kama vile walivyoongoza mpango wa kuhujumu Mkutano Mkuu Maalumu wa CUF ulioahirishwa pale Blue Pearl Hotel, Ubungo Plaza.

Mhe. Joran Bashange ameumizwa maeneo kadhaa ya mwili na anaendelea na matibabu na taarifa za ndani zinaonesha kuwa wahusika walielekezwa kumshambulia vibaya na kumuua ikiwa wangelifanikiwa kuondoka naye. Tukio hili linafanana na matukio kadhaa yaliyotokea huko nyuma na mfano utekwaji wa Dr. Ulimboka, Absalom Kibanda , Salma SaidKubenea na wengine.
Vijana waliohusika na utekaji huo na gari lao wanashikiliwa na Polisi katika Kituo cha Polisi Buguruni.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) kinalaani sana kitendo hicho na kinachukua hatua stahiki. Chama kinaamini kuwa kwa sasa Prof. 

Lipumba na watu wake wamekusudia kuendesha HUJUMA za wazi na kuvuka mipaka ya ushindani wa kisiasa za ndani ya Chama na kujivika joho la 'Uintarahamwe na Umungiki' wa wazi dhidi ya Chama na kuhatarisha na kutishia usalama wa maisha ya viongozi wa Chama.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma. 
16 Septemba 2016.

No comments: