Friday, September 16, 2016

STORY SITA KUBWA KUTOKA POLISI DAR ES SALAAM LEO ZISIKUPITE


 KUKAMATWA KWA MAJAMBAZI WATANO, WAKUTWA NA SILAHA AINA YA SHOTGUN, BASTOLA 03 NA RISASI 49

Kikosi Maalum cha Kupambana na ujambazi wa kutumia silaha cha Polisi Kanda Maalum ya Dar Es salaam kimefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano kwa makosa ya ujambazi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es salaam.

Katika tukio la kwanza mnamo tarehe 14/09/2016 Askari Polisi wakiwa katika ufuatiliaji maeneo ya Goba Wilaya ya kipolisi Kawe Mkoa wa Kinondoni  walimkamata mwanamke mmoja mkazi wa Goba, baada ya kupata taarifa kuwa anawafahamu majambazi wanaojihusisha na uvamizi kwenye maduka makubwa.


Katika mahojiano aliwataja washirika wake watano  ambao walifuatiliwa na kukamatwa katika upekuzi walipatikana na silaha moja Bastola aina ya Browning TZCAR No.87881 ikiwa na risasi 17.

Katika mahojiano zaidi watu hao walikiri kufanya matukio ya ujambazi wa kutumia silaha jijin DSM na mmoja wao alitaja silaha  nyingine amezifichwa kwenye majaruba ya Chumvi maeneo ya Ununio na kuwaongoza askari hadi kwenye eneo husika. walipofika maeneo hayo mtuhumiwa alianza kukimbia kuelekea kichakani ndipo Askari walirusha risasi iliyompata mguu wa kushoto  na kufanikiwa kumkamata.

Hata hivyo mtuhumiwa alifariki akiwa njiani kuelekea hosptalini kutokana na kuvuja damu nyingi kutokana na jeraha la risasi.

Aidha kati ya watuhumiwa wengine waliobaki mmoja aliwaongoza askari hadi eneo la gongolamboto anakoishi ambapo katika upekuzi
alipatikana silaha nyingine aina ya Shotgun Pump action ambayo imefutwa namba za usajili, msumeno mmoja na tupa moja  ya kunolea misumeno na visu.
Watuhumiwa wote wanne wanaendelea kuhojiwa mara ya upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Katika tukio lingine Polisi kanda Maalum Dar es salaam mnamo tarehe 05/09/2016 majira ya saa 08:00 usiku  huko magomeni mtaa wa makumbusho  askari wakiwa doria  waliwatilia mashaka watu wawili wakiwa wamepakizana kwenye Pikipiki na begi dogo mgongoni ndipo askari waliwasimamisha hawakutii amri hiyo, Polisi walifuatilia ili kuwahoji  lakini watu hao baada ya kugundua kuwa Polisi wanawafuatilia walianza kukimbia kwa kasi mara wakatupa begi hilo, askari waliliokota baada ya  kulipekua begi hilo walikuta Bastola mbili aina ya Browning No, NE984517CAT5802  Ikiwa na risasi 11 na nyigine yenye No. CZ 2075 aina ya RAMI ikiwa na risasi 21 na magazine mbili iliyotengenezwa CZECH REPUBLIC jitihada ya kuwasaka watu hao zinaendelea.

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM DSM LATOA WITO KWA VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA KUIMARISHA ULINZI KATIKA MAENEO YAO

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam anatoa wito kwa Wenyeviti wa serikali za mitaa kupitia kamati za ulinzi na usalama za mitaa kuimarisha ulinzi na usalama  katika maeneo yao na kutimiza wajibu wao, amewataka wamiliki wote wa nyumba jijini kuhakikisha kuwa wanaweka kipengele cha kuwepo na picha katika mikataba ya kupangisha nyumba zao kutokana na uwepo wa wimbi la uhalifu jijini.

Aidha amewataka kufuatilia jambo hilo kwa ukaribu ikiwa ni pamoja na wao kuwa na picha za wapangaji wa nyumba hizo, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuweza kuwabaini wahalifu mbalimbali katika maeneo yao, atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kupelekwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Ibara ya 146(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, serikali za mitaa zitakuwa na majukumu ya fuatayo:
1. Kutekeleza kazi za Serikali za Mitaa katika eneo lake
2. Kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi
3. Kuimarisha demokrasia katika eneo lake na kuitumia demokrasia
kuharakisha maendeleo ya wananchi.

KUPATIKANA KWA MAGARI 04 YA WIZI, HATI ZA MAGARI NA WATUHUMIWA WAWILI

Kikosi Maalum cha Kupambana na wezi wa magari cha Polisi Kanda Maalum Dar Es Salaam mnamo tarehe 03/09/2016 majira ya saa nne asubuhi lilipokea taarifa toka kwa raia mwema kuwa kuna gari aina ya Toyota Carina T 289 DFL imeibiwa jijini DSM maeneo ya Kimara na kupelekwa mafichoni Mjini Mbeya. Baada ya taarifa hizo kupokelewa ndipo ufuatiliaji ulianza na  mtuhumiwa MZAWARI AHAMAD (29) mkazi wa mwananyamala alikamatwa jijini MBEYA akiwa na wenzake  wawili na alikiri kuhusika na tukio hilo.

Katika tukio lingine mnamo tarehe 11/09/2016 asubuhi zilipokelewa taarifa toka kwa raia mwema kwamba huko Mkoa wa Kilimanjaro kuna gari nyingine aina ya Suzuki Carry T234 DAJ ambayo iliibwa maeneo ya Tandale jijini DSM mali ya NURDIN MPELEMBE. Askari walisafiri mkoa tajwa tarehe 05/09/2016 na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa SERAFIN VALERIAN (46), mfanyabiashara, mkazi wa Himo Kilimanjaro akiwa na magari  matatu ya wizi nyumbani kwake. Magari hayo ni:  SUZUKI CARRY T935 CPC rangi nyeupe namba zake halisi ni T139 DEK mmiliki ni BRAYAN LYIMO wa Ilala mtaa wa Arusha Dsm, gari nyingine ni TOYOTA RAV 4 rangi ya silver T732 CHP ambayo iliibwa kimara jijini Dsm tarehe 11/01/2016 nyumbani kwa CECULAR JAMES LAURICH namba halisi ni T440CAW.

Kadhalika mtuhumiwa  baada ya kupekuliwa alipatikana na hati mbalimbali za magari na pikipiki ambazo ni: kadi za bajaji, bima za magari mbalimbali yaliyopata ajali na kulipwa, plate namba za pikipiki, motorvehicle licence na TIN namba zenye majina mbalimbali.

watuhumiwa wote wakiwemo madalali wa magari haya ya wizi wanaendelea kutafutwa na mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa mahojiano mara upelelezi utakapokamilika atapelekwa mahakamani.

POLISI KANDA MAALUM D’SALAAM YAKUSANYA MILIONI TSH 882,570,000/= TOZO ZA MAKOSA YA USALAMA BARABARANI KUANZIA TAREH E 06/09/2016 HADI TAREHE 16.09.2016.
Taarifa  ya Kikosi cha Usalama barabarani Kanda Maalum ya D’salaam ya ukamataji wa makosa ya Usalama  Barabarani kwa kipindi cha kuanzia tarehe 06.09.2016  hadi tarehe 16.09.2016 ni kama ifuatavyo:-

1.  Idadi ya magari yaliyokamatwa                     - 26,363
2.  Idadi ya Pikipiki zilizokamatwa                     - 3,056       
3.  Daladala zilizokamatwa                        - 7,523
4.  Magari mengine (binafsi na malori)      - 18,840
5.  Bodaboda waliofikishwa Mahakamani
kwa makosa ya kutovaa helmet na
kupakia mishkaki                                       -  53
6.  Jumla ya Makosa yaliyokamatwa               - 29,419
JumlaFedha za Tozo zilizopatikana    TSH    882,570,000/=

 MAADHIMISHO YA WIKI YA NENDA KWA USALAMA JIJINI DSM
Taarifa ya Kikosi cha Usalama barabarani Kanda Maalum  D’salaam kitaendelea na ukamataji wa makosa ya Usalama  Barabarani
Aidha zoezi la ukaguzi wa magari ya wiki ya Nenda kwa usalama kwa mkoa wa D’salaam limeanza leo 16.09.2016 katika Vituo vyote vya Usalama Barabarani pamoja na vituo vikuu vya mabasi ya abiria, ambapo ukaguzi ukifanyika na gari kukidhi viwango itatolewa sticker kwa gari husika kwa viwango. Wakaguzi wa magari waliopo vituoni ndio watatoa sticker hizo baada ya ukaguzi, kwa viwango vya Tsh 5,000/= kwa magari makubwa na ya biashara, Tsh 3,000/= magari madogo binafsi, Tsh 1,000/=  Bajaji na pikipiki zoezi hili kwa kanda ya Dar es salaam litaendelea hadi mwezi wa kumi na mbili.
Kauli mbiu ya maadhimisho 2016. “HATUTAKI AJALI, TUNATAKA KUISHI SALAMA.

ONYO KWA WANAOTUMIA SIMU ZA DHARURA 111 NA 112 VIBAYA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm linatoa onyo kali kwa wananchi wanaotumia  vibaya simu za dharura 111 NA 112  kwa kutoa taarifa za uongo na kupiga simu kuwapa watoto wadogo waongee au kuweka muziki jambo ambalo hupunguza utendaji wa kazi ya askari. wananchi wote wa jiji la DSM watambue kuwa kutoa taarifa za uongo ni kosa la jinai, Aidha Polisi tutaanza kuwafuatilia wote kupitia mitandao yetu General Packet Radio Service (GPRS) inayoonyesha maeneo walipo na simu wanazotumia ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Pia tunapenda kuwafahamisha wananchi wote watumie simu zetu kutoa taarifa zenye ukweli na zitafanyiwa kazi kwa wakati na kuona matokeo ya muda mfupi pale wanapoona viashiria vya uhalifu ama tukio lolote linaloleta uvunjifu wa amani.


S.N.SIRRO - CP
 KAMISHNA WA POLISI
KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

No comments: