Thursday, October 13, 2016

RC Arusha Mrisho Gambo Arejesha fedha zaidi ya shilingi milioni 1.3 alizokuwa amelipwa kwa ajili ya kuhudhuria kilele cha Mwenge.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo leo ametekeleza agizo la Rais Magufuli la kusitisha safari ya kwenda Mkoani Simiyu kwenye sherehe za kuhitimisha kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru kwa kurejesha kiasi cha Jumla ya Shilingi 1,389,300.

Fedha hizo yalikuwa ni malipo kwa ajili ya Mkuu wa Mkoa, Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa , Dereva wa Mkuu wa Mkoa na gharama za mafuta.

Akiongea na mwandishi huyu ofisini kwake leo, mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha amesema wakati agizo hilo linatolewa yeye alikuwa bado hajaanza safari ya kuelekea mkoani Simiyu, na kwamba amelipokea bila kinyongo na mara moja akaamua kurejesha posho hiyo, akionesha stakabadhi ya kuthibitisha hilo.

Kwa mujibu wa mchakato wa malipo ya posho kwa safari hiyo ya kwenda mkoani Simiyu kwa siku tatu, posho ya RC ilikuwa ni Sh 360,000, Msaidizi wa RC Sh 240,000, posho ya dereva 24,000 na Sh 549,300 kwa ajili ya Mafuta ya gari.

Pia RC Gambo ameahidi kusimamia zoezi hilo kwa wahusika wote mkoani Arusha na kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo kwa wakati na fedha hizo zielekezwe kwenye ujenzi wa madarasa kama sehemu ya maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na darasa la awali kwa mwaka 2017.

No comments: