Friday, November 11, 2016

Hii ndiyo Hotuba ya Zitto Kabwe aliyoisoma muda mchache uliopita bungeni wakati wa kumuaga Sitta


Tangulia Spika wa Mioyo ya Wananchi

Hotuba ya ndg. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, mbunge wa Kigoma Mjini katika Kikao Maalumu cha Bunge cha Mazishi ya Spika Mstaafu Samwel John Sitta
Ndugu Spika, Ndugu Wabunge, Mama Magreth Sitta na Watoto wote wa Mzee Samwel John Sitta, ndugu jamaa na marafiki.

"Leo kikao maalumu cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wake wa Tano kinamuaga mtoto wa Mzee John Sitta na Hajjat Zuwena Said Fundikira. Tanzania itamkumbuka mtoto wa wazee hawa kama mtu aliyejaribu kuboresha kila alichokabidhiwa kama jukumu; shujaa wa wote wanaomini katika Uwajibikaji wa kitaasisi;

Mwanasiasa aliyepanda na kushuka na kupanda kubakia kileleni;taswira ya mkoa wake wa Tabora; sio tu mdhamini wa klabu ya Simba, bali pia Mwanasimba aliyeipeleka klabu Brazil na kuwezesha kuifunga Yanga mabao mengi zaidi ambayo hayajapata kulipwa hata kwa kuunga kuunga; mwanamageuzi wa Bunge na Spika wa mioyo ya Watanzania.

Hata katika kifo chake, Samwel John Sitta ameweka rekodi nyengine kwa Bunge kufanya kikao maalumu kuenzi mmoja wa wajumbe wake mahiri kati ya mwaka 1975 – 2015 isipokuwa tu kwa kipindi cha 1995-2005. Rekodi hii itaendelea kwa wengine wote watakaofuata. Ni mtu wa namna gani wewe Samwel Sitta, Spika wa Kasi na Viwango, unayeweka rekodi hata ukiwa umelala ndani ya Jeneza lako lililopambwa na Bendera ya Taifa letu ukielekea nyumbani kwako Urambo kwenye nyumba yako ya milele. Ulikuwa hushindwi ukiwa hai, umeonyesha umahiri wako hata ukiwa kwenye umauti. Kweli wewe ni Spika wa Watu ( The Peoples Speaker ).

Tuliokupenda tunajua. Ulikuwa baba mlezi. Ulikuwa mume mwema. Ulikuwa Babu. Ulikuwa Kiongozi. Nadhani hata kwa uliokwaruzana nao hapa na pale wanajua hilo. Leo sote tuna majonzi makubwa. Umeliunganisha Taifa kukumbuka ewe Spika wa Watu. Ulikuwa na vyeo vingi; Mbunge, Naibu Waziri, Waziri, Mkuu wa Mkoa, Waziri tena, Mkurugenzi Mtendaji, Spika, Waziri tena na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. Lakini, wala, tunakuita Spika Sitta tu. Kwanini? Kwa sababu ‘legacy’ yako ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sio kwamba umeanzisha Bunge wewe, la hasha. Lakini ulipopokea uliboresha, uliwezesha kutunga kanuni mpya, uliimarisha Mhimili huu na kuuweka katika nafasi yake ya Kikatiba. Nakumbuka siku moja ulimwomba Rais wa Jamhuri aongee na baadhi yetu, ilikuwa mwaka 2006.

 Mimi nikiwa nina miaka 29 tu. Tukakutana na Rais ukumbi wa Msekwa. Baada ya kikao kilichofanikiwa kumshawishi Rais kuhusu mabadiliko uliyoyataka uliniambia  “Babu, mimi sasa alasiri, ninyi ndio  saa nne asubuhi. Nawawekea misingi tu na kuliweka Bunge katika nafasi yake ya kikatiba”. Kilichofuata ni mabadiliko makubwa ya Kanuni za Bunge, kuandikwa upya kwa Sheria ya Bunge ( National Assembly Administration Act, 2008) na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Majimbo ( Constituencies Development Catalyst Fund ( CDCF). 

Wabunge, mnataka kumuenzi Spika wa Watu Samwel John Sitta? Basi hakuna kumuenzi bora zaidi kama kuimarisha uhuru wa Bunge na heshima ya Bunge.
Samwel Sitta, bado tunasikia mwangwi wa sauti yako nene kutoka kwenye kiti cha Spika ukiwataka Mawaziri wajibu maswali kwa ufasaha. Ukiona kuna swali linaloruhusu Tabora hukusita kuwaambia mawaziri wajibu vizuri ( haswa kuhusu barabara ) au ukiamsha jeshi la akina Lumambo Selelii wakisema “ mheshimiwa Spika, wewe leo ukipata dharura Urambo unafikaje”! hukuisahau Tabora yako.

 Damu ya kichifu wa Unyanyembe ya Fundikira kutoka mama yako Zuwena ilikusambaa kwenye mishipa yako. Ulitoa nafasi kwa wabunge wote wa kambi zote ndani ya Bunge. Hatusemi hukubagua, la hasha, uCCM wako ulikuwa pale pale. Lakini walio wengi walishinda na walio wachache walisikika. Ndio Demokrasia hiyo.

Nakumbuka siku ile unamwomba radhi Mzee John Momose Cheyo katika kamati ya Uongozi, eti msongo wa mawazo ulikujaa kwani watu wanapitapita Jimboni. Lakini uliwashinda. Unyenyekevu wako wa kuomba radhi unapokosea ni somo kubwa sana kwa Viongozi wengine waliobakia.
Tuendeleze Jahazi.

Samwel Sitta anakwenda kwenye nyumba yake ya milele akiongozwa na imani yake kubwa kwa Mungu na uzalendo wake usio na mawaa kwa nchi yake Tanzania. Angalau bado ataendelea kuwa nasi kwa kutuachia mafundisho makubwa kutokana na Maisha yake; mambo mema aliyoyafanya kwa nchi yetu; ndoto aliyoiishi ya Tanzania imara na yenye heshima; na malezi kwa viongozi wengi vijana aliowafunda na kuwalea kiuongozi.

Ni dhahiri umeishi maisha yako Babu. Kama isemavyo biblia, 2 Timotheo 4:7 “ Nimepigana vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda”. Tangulia Spika wa Watu ( The Peoples’ Speaker) Samwel John Sitta.


No comments: