Saturday, November 12, 2016

Kiungo Mshambuiliaji hatari kutoka Ghana Agyei asaini miaka mitatu Azam FC

 UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, unayofuraha kuwaataarifu wapenzi wa soka kuwa jioni ya leo umefanikiwa kuingia mkataba wa miaka mitatu na kiungo mshambuliaji kutoka Ghana, Enock Atta Agyei.


Agosti mwaka huu, Azam FC tuliingia makubaliano maalumu na Medeama ya Ghana juu ya kumsajili kinda huyo anayetimiza umri wa miaka 18 mwakani baada ya benchi la ufundi kuridhishwa na uwezo wake na sasa amejiunga rasmi kwenye viunga vya Azam Complex.
Agyei anasaini mkataba tayari kabisa kuanza kuitumikia Azam FC katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) mwakani pamoja na michuano mingine ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika.

Tunaamini ya kuwa ujio wa nyota huyo wa timu ya Taifa ya Vijana ya Ghana chini ya miaka 17, utazidi kuipa nguvu timu yetu kuelekea kwenye michuano inayotukabili mbeleni, hivyo tunapenda kumtakia mafanikio mema kwa kipindi chote atakachokuwa akiipigania jezi ya Azam FC.


Azam FC tunapenda kuwafahamisha mashabiki wetu kuwa tutaendelea kukifanyia marekebisho kikosi chetu kuelekea usajili wa dirisha dogo, lengo ni kukipa nguvu kikosi hicho ili kifanye vizuri zaidi katika michuano ya hapa nchini pamoja na ile ya Kimataifa.
Lengo kubwa la Azam FC ni kuendelea kuwafurahisha mashabiki wetu kwa kupata matokeo bora uwanjani, na tunaamini ya kuwa, benchi zuri la ufundi tulilokuwa nalo, wachezaji wazuri walioko kikosini na wengine watakaokuja kuongeza nguvu, wote kwa pamoja wataweza kutuvusha kuelekea safari ya mafanikio msimu huu.

Hivyo, tunawaomba mashabiki wetu kuvuta subira na kuendelea kuisapoti timu kwani tunaamini ya kuwa nyie ndio nguzo muhimu ya 12 uwanjani katika kuwapa hamasa wachezaji ya kupata matokeo bora pamoja na kuijenga timu kiujumla.   

Wakati huo huo, leo tumewapokea wachezaji saba waliokuja kwenye majaribio ya kujiunga na Azam FC, ambao ni mabeki wa kati Mbimbe Aaron Nkot (Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Ivory Coast), kiungo mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Cameroon),

Wengine ni washambuliaji Yaya Awaba Joel (Cameroon), Samuel Afful, Benard Ofori (wote Ghana) na Konan Oussou kutoka Ivory Coast.  

Imetolewa na Uongozi Azam FC

No comments: