LHRC NAO WAMVAA MAKONDA WAKEMEA UDHALILISHAJI NA UKIUKWAJI WA MISINGI YA KISHERIA NA HAKI ZA BINADAMU


 Ndugu Wanahabari,

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la kiserikali ambalo si la kisiasa wala kibiashara lenye kujibidiisha katika kutetea, kulinda na kuendeleza haki za binadamu na utawala bora nchini. Kituo kimekuwa kikifuatilia mwenendo wa serikali na taasisi zake ili kuhakikisha utendaji wa serikali unafuata misingi ya sheria na haki za Binadamu kwa lengo la kuhakikisha kuwa utendaji wa serikali unakuwa na tija kwa wananchi wake.

Ndugu Wanahabari,
Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, takribani mwaka mmoja sasa, kumekuwa na jitihada za lazima za serikali yenyewe katika kupambana dhidi ya rushwa na ubadhirifu,nakuimarisha uwajibikaji  vitu ambavyo  ni vichocheo muhimu katika ustawina maendeleo ya  nchi.Kwa upande mwingine kumekuwa na ongezeko la uwazi katika utekelezaji wa baadhi ya shuguli za serikali jambo ambalo kwa mapana yake ni zuri pia.

Hata hivyo jitihada hizo zimekuwa na kasoro mbali mbali za kiutendaji , kiufundi na kisheria ambazo zimekuwa zikitajwa mara kadhaa na wadau mbalimbali ikiwemo Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu. Kikubwa zaidi katika haya yote ni ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu katika matamko na,hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kuanzia ngazi ya serikali za mitaa mpaka serikali kuu. Mambo haya ambayo kwa nadharia yanaonekana ni mepesi ni hatari zaidi katika ustawi wa nchi ya kidemokrasia na sisi kama watetezi wa haki za Binadamu hatutaacha kuyakemea vikali ili kujenga jamii yenye haki na usawa.

vitendo hivyo ambavyo serikali imeendelea kuvifumbia macho.
Ndugu Wanahabari,
Ninyi mmekuwa mashahidi kwani ni mara nyingi tumetoa matamko kukemea kauli zisizo afya kwa ustawi wa utawala wa sheria na Haki za Binadamu, lakini viongozi wa serikali wameendelea kuziba masikio na kuendelea kuvunja sheria na kukiuka haki za Binadamu, ili hali wakiongoza kama miungu watu.


Sote tumeshuhudia kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa katika ziara ya kuzungumza na wananchi huko Kinondoni. Ndugu Makonda amemshambulia kwa maneno mtumishi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Rehema Mwinuka baada ya kumtolea matamshi ya kejeli na kumnyima haki yake ya asili ya kusikilizwa na hata kujieleza. Makonda alinukuliwa akimfokea Bi.Mwinuka “hawa ndio vichaa tunaohangaika nao, toka hapa”.

Ndugu wanahabari,
Tanzania ni nchi inayoheshimu utawala wa sheria kwa mujibu wa Katiba ya waka 1977. Hivyo serikali yetu kwa mujibu wa katiba hiyo ina mihimili mitatu  ambayo ni Serikali yenyewe, Bunge na mahakama . Katika utendaji chombo kilichopewa mamlaka kusimamia haki na tafsiri ya sheria ni mahakama pekee. Licha ya misingi hii ya kikatiba kuwepo viongozi wa serikali wamekuwa wakichukua nafasi ya Mahakama na kuhukumu na kuwahesabu watuhumiwa kuwa na hatia moja kwa moja  pasipo kujua wanakiuka misingi ya katiba waliyo apa kuilinda. Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania pamoja na mambo mengine inasema “ Mtu hata hesabiwa kuwa na hatia mpaka Itakapo thibitishwa na Mahakama yenye mamlaka” Kitendo cha kuwahukumu watu mbele ya hadhara na kuwataja majina kama wezi , wajinga, wasiokuwa na akili timamu na lugha zingine zisizo na staha ni kudhalilisha utu wa mtu na kuvunja misingi ya Katiba.
Ndugu wanahabari,

Tunasikitika kuwa mbali na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kukemea kwa nguvu uvunjwaji huu wa sheria na ukiukwaji wa Haki za Binadamu unaofanywa na viongozi bado viongozi wetu wameendelea kuwa wakaidi na kusahau kuwa dhamana waliyo nayo iko kwa mujibu wa sheria na badala yake wanajiona miungu watu kama alivyojifafanua Mhe. 

Makonda kwa kusema “huna wa kukutetea mimi nikisimama mahala Mungu amesimama”.Aina hii ya kauli haitarajiwi kutumika kwa viongozi wa serikali ya Kidemokrasia . Kauli hizi ni aina ya kauli mbazo zimekuwa zikitumika katika serikali zilizofuata mifumo ya kifashisti. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 13(1) “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.”   Ibara hii ya katiba inatushangaza kuona ni wapi viongozi wetu wanatoa mamlaka ya kujitangaza wao ni Mungu na waliopo chini yao hawana haki ya utetezi.

Tunapenda kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa katiba Ibara ya 8 (1) inatanabaisha kuwa;
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo - 
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii;”

Hivyo tunapenda kumkumbusha mkuu wa mkoa Makonda kuwa yeye amepewa dhaman tu na wananchi na hivyo yeye si Mungu kama anavyodhani.

Kanuni za utumishi wa Umma za mwaka 2014, Kanuni 107(1) na (2) zinaeleza bayana kama ifuatavyo: “107 (1) Mtumishi wa umma anapofanya kosa kuhusiana na kazi yake, Katibu Mkuu au Mkuu wa Taasisi au Mkuu wa Idara husika atapaswa kuzingatia kama kosa hilo ni la jinai au ni la uvunjaji wa nidhamu za kazi au aina zote mbili.

(2) Iwapo mtumishi atafanya kosa la kinidhamu, Katibu Mkuu au Mkuu wa Taasisi au Mkuu wa Idara atampa taarifa ya dai hilo mtumishi husika na kupewa nafasi ya kujieleza na baadae kuchukuliwa hatua muafaka. Taarifa ya mtumishi huyo itawasilishwa kwa maandishi kwa Katibu wa chama cha wafanyakazi au mwakilishi wa wafanyakazi aliyomo katika Kamati ya Uongozi.”

Kifungu hiki kinatanabaisha wazi kwamba Mh. Makonda amekuwa  akikiuka taratibu za kisheria za uwajibishaji wa  watumishi wa serikali walio chini yake.
Hata hivyo kauli hiyo ya matusi pia ni udhalilishaji mkubwa wa kijinsia ukizingatia Dunia inaadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Ndugu Wanahabari,

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaendelea kuwasihi viongozi wa serikali kutopuuza misingi ya utawala wa sheria kwani kwa kufanya hivyo wanavunja haki za wengine na kukiuka misingi ya utawala wa sharia na utawala bora.

Tunaamini kwamba  kuna watanzania wengi wanateseka huko mitaani na wanahitaji msaada. Nia ya serikali kufanya ziara katika maeneo mbalimbali inaweza kuwa ni njema sana katika kukuza uwajibikaji isipo kuwa tu kama taratibu za kisheria na misingi ya utawala bora itazingatiwa katika zoezi hilo. Ziara hizi zingetumika zaidi kugundua maeneo dhaifu na kupanga mikakati ya kuboresha kuliko kugeuka kuwa mahaka za wazi ambazo zinaweza kuwa chombo kikuu cha uvunjaji wa haki za binadamu   na ukiukwaji wa misingi ya katiba yetu.

Hata hivyo tunamtaka Ndugu Paul Makonda kumwomba radhi Bi. Rehema Mwinuka kwa kumdhalilisha kwa matusi tena mbele ya hadhara. Tunaamini kwamba serikali inaweza kutimiza azma zake bila kukiuka utawala wa sheria kwani kuongoza bila kufuata katiba si ruhusa katika mfumo wa kidemokrasia.

Imetolewa na Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.