Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe jana alisababisha taharuki katika kikao cha Bunge baada ya kuzusha tuhuma za rushwa kwa wabunge wa CCM katika kipindi cha maswali na majibu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Ingawa swali lake hilo lenye tuhuma lilizuiwa kujibiwa na Naibu Spika, Dk Tulia Akson kwa kuwa halikuwa swali la kisera, hoja iliibuliwa tena na wabunge wengine wakati wa kuingia kipindi cha majadiliano, kama miongozo.
Mbowe katika swali lake kwa Waziri Mkuu alituhumu wabunge wa CCM, kupewa rushwa ya Sh milioni 10 kila mmoja na serikali ya chama hicho ili kuupitisha Muswada wa Huduma za Habari unaowasilishwa bungeni leo.
Aidha alidai rushwa hiyo, pia imetolewa kupitisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18. Pamoja na tuhuma hizo kutojibiwa na Waziri Mkuu kutokana na muundo wa maswali ya papo kwa hapo kugusa sera, Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema) aliomba mwongozo wa Spika huku akitaka kuundwe Tume Huru ya Kimahakama ya Bunge, kuchunguza tuhuma hizo.
Naye Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) alisimama na kuomba mwongozo, na kumtaka Mbowe athibitishe tuhuma hizo au achukuliwe hatua.
Nkamia alisema yeye akiwa Mbunge wa CCM, hajapata rushwa hiyo wala hakuiona na kuhoji kwa nini Mbowe ahoji wakati yeye si Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), hivyo akitaka Mbowe athibitishe tuhuma hizo na akishindwa, alitaka mwongozo ni hatua gani Bunge itamchukulia.
Akijibu hoja zote hizo za wabunge, Naibu Spika alimtaka Mbowe kupeleka tuhuma zake kwa vyombo husika ili vichukuliwe hatua stahiki.
Akifafanua zaidi, Naibu Spika katika majibu yake ya miongozo hiyo alisema :“Wabunge tuwe makini, ukisema kuna rushwa ujue kuna vyombo vyake maalumu vya kushughulikia hilo, Bunge haliwezi kusikiliza kesi hizo, Bunge na Waziri Mkuu hawana mamlaka kwa mambo yasiyohusiana nayo, nashauri suala hilo lipelekwe kwenye vyombo husika.”
Kuhusu mwongozo wa Nkamia, alisema kwamba hatomtaka Mbowe athibitishe kwani alimzuia kuliongelea, lakini mwenye uthibitisho apeleke kwenye chombo kinachohusika na rushwa ili kifanye kazi yake.
Mbowe aitisha mkutano
Baada ya tafrani hiyo kuzuka bungeni na kumalizwa na Naibu Spika kwa kutoruhusu mjadala wake, Mbowe aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Bunge mjini hapa, akiwa na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu na viongozi wengine wa Chama cha Wananchi (CUF).
Katika mkutano huo, Mbowe alimtaka Rais Magufuli kumtumbua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kile alichoeleza kuwa yeye (Majaliwa) pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana walihusika kutoa kwa wabunge hao wa CCM 272 fedha hizo.
Alisema pia kuwa, wanamuandikia barua Rais kutaka aunde Tume ya Kimahakama ya Uchunguzi, kuchunguza suala hilo kwa kuwa linawahusu wabunge, na Bunge haliwezi kujichunguza lenyewe.
Akifafanua kuhusu fedha hizo, Mbowe alisema taarifa walizonazo, zinathibitisha kuwa katika kikao cha wabunge wa CCM cha Oktoba 25, mwaka huu, Majaliwa na Kinana waligawa fedha Sh milioni 10 kwa kila mbunge wa CCM ili kuwapooza kuhusu hali ya mdororo wa uchumi.
Alisema pia kuwa fedha hizo, zilizoanza kutolewa Oktoba 26, zililenga pia kuwashawishi wabunge hao wa CCM, kupitisha Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18, ambao mapendekezo yake yamewasilishwa bungeni.
Mbowe alisema tuhuma hizo ni nzito na Bunge haliwezi kujichunguza lenyewe, hivyo ni lazima iundwe tume huru ya kimahakama kuchunguza jambo hilo. Mbowe alisema ushahidi wa kutosha wanao na watautoa mbele ya tume hiyo.
Mbowe alisema walimshangaa Naibu Spika, Dk Akson kwa kuwazuia kutoa ushahidi ndani ya Bunge, kama walivyoombewa mwongozo na Nkamia. Alieleza kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa upinzani, kuzuiwa kutoa ushahidi kwa jambo, ambapo linaonekana kama ni uongo.
Lisu naye azungumza
Kwa upande wake, Lissu alisema watamuandikia Rais Magufuli barua rasmi kueleza kilichofanywa na viongozi wake, na kumtaka achukue hatua kuhusu suala hilo.
“Magufuli amejinadi yeye anapambana na ufisadi, mtihani wa pili aufanye na aufaulu ni huu. Magufuli amtumbue Kassim Majaliwa kutoka kwenye nafasi hiyo ya uwaziri mkuu,” alisema Lissu.
Lissu alisema Sheria ya Tume za Uchunguzi, inampa Rais mamlaka ya kuunda tume ya uchunguzi kwenye jambo kubwa na muhimu, linalohusu mambo ya umma.
“Katika barua hiyo tunamgusia Tulia Ackson. Kwa maoni yangu kisheria, kiongozi wa kuteuliwa anaondolewa na mamlaka ya uteuzi, Rais amuondoe huyu mama bungeni, hafai,” alisema Lissu.
Viongozi wa CUF waliokuwa katika mkutano huo ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Mngwali.
Awali, ndani ya Bunge baada ya Naibu Spika kuzuia swali hilo kwa kuwa si la kisera, Mbowe akinukuu Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma ya mwaka 1995 na Sheria ya Rushwa ya mwaka 2007, alisema masuala ya rushwa ni ya kisera.
Hata hivyo, Dk Akson alimtaka Mbowe kuheshimu kiti na kanuni, na kusisitiza kuwa, yeye (Naibu Spika) anaongozwa kwa kanuni na kanuni zinaeleza kuwa swali hilo si la kisera.
No comments:
Post a Comment