RUSHWA YATAJWA KUCHOCHEA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI TANZANIA

Wanajamii mbalimbali kutoka mashirika ya kiraia nchini pamoja na maafisa kutoka serikalini pamoja na wadau wa ardhi wakimsikiliza kwa makini Magdalena Rwebangira ambaye alikuwa mwezeshaji wa semina hiyo ya kupitia kwa kina maswala mbalimbali yanayohusu ardhi pamoja na kutoa mapendekezo juu ya sera mpya ya ardhi nchini ambayo inatengenezwa kwa sasa
 Imeelezwa kuwa Rushwa kwa viongozi wa serikali za vijiji na maeneo mengine ndiyo imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro mingi ya ardhi nchini Tanzania ambayo imekuwa ikiibuka katika maeneo mengi na kusababisha matatizo makubwa yakiwemo vifo na uharibifu wa mali.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam katika warsha maalum iliyoandaliwa na serikali kupitia wizara ya ardhi ambao wamewapa nafasi Shirika lisilo la kiserikali la TGNP-MTANDAO kuwakutanisha wanajamii mbalimbali kujadili kwa pamoja sera mpya ya ardhi ambayo inatengenezwa nchini kwa sasa na pia kupitia kwa pamoja sera zilizopo ili kuona ni jinsi gani wanaweza kurekebisha maswala mbalimbali kwenye sera mpya ambayo inatengenezwa kwa sasa.
Mwezeshaji Magdalena Rwebangira akitoa mada katika Warsha Hiyo iliyofanyika Jijini Dar es salaam 
Akizungumza katika warsha hiyo Mwezeshaji wa leo ambaye ni Magdalena Rwebangira amesema kuwa baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa na vijiji wamekuwa wakitumia nafasi zao kuuza mashamba mara mbili mbili kwa watu tofauti tofauti jambo ambalo limekuwa likianzisha migogoro mingi kutokana na shamba moja kukutwa na wamiliki Zaidi ya mmoja.
Amesema kuwa moja ya maswala ambayo wanayajadili katika semina hiyo ni pamoja na kuona ni jinsi gani wanaweza kuishauri serikali kutengeneza sera ambayo itakuwa na uwezo wa kuondoa migogoro mingi ya ardhi nchini ambayo imekuwa ikisababisha matatizo makubwa.


Aidha katika mjadala huo pia wamejadili kwa kina swala la umiliki wa ardhi nchini Tanzania ambapo imeonekana kuwa bado watanzania walio wengi hususani wanawake na wajane wa vijijini wamekuwa wakikosa Fursa ya kumiki ardhi kutokana na Imani walizowekewa kuwa ardhi itamikiwa na wanaume tu jambo ambalo mwezeshaji huyo amelikataa na kusema kuwa hata katika Rasimu mpya ya katiba swala la umiliki wa ardhi nchini limeonyeshwa kuwa ni la kila mtanzania na sio kundi moja la watu.
Nyangi Marwa mwanamama kutoka mkoani Mara Akizungumza na wanahabari
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanawake kutoka mikoani mmoja wapo akiwa ni Nyangi Marwa mwanamama kutoka mkoani Mara ambapo akizungumza na mtandao huu amekiri kuwa wanawake wengi wa Tanzania wamekuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu maswala ya umiliki wa ardhi na sera zinazotuongoza jambo ambalo limezidi kuwafanya kuwa chini ya wanaume katika umiliki wa ardhi nchini
Grace Kisetu kutoka mtandao wa TGNP
Naye Grace Kisetu kutoka mtandao wa TGNP nchini Tanzania ambao ndio walikuwa wenyeji wa mkutano huo amesema kuwa mkutano huo umeandaliwa na Serikali kwa lengo la kuwapa nafasi wananchi kupitia Mtandao wao kutoa maoni juu ya Rasimu ya sera ya ardhi ambayo inatangenezwa kwa sasa nchini Tanzania pamoja na kupitia Sera nyingine ikiwepo ile inayotumika ya mwaka 1995 ili kuona kama kuna mambo ambayo yanafaa kuwepo katika sera mpya nchini.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria kutoka wizara ya ardhi pamoja na maafisa mbalimbali wa ardhi na wadau kutoka mashirika mbalimbali ya kiraia nchini

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.