Friday, January 27, 2017

UWANJA WA TAIFA MPYA RUKSA KUTUMIKA,TFF WAMSHUKURU RAIS MAGUFULI


TFF YAMSHUKURU RAIS DK. MAGUFULI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kuridhia kufunguliwa tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kadhalika, TFF inamshukuru Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kwa juhudi zake na kwamba namna aliyoonesha ushirikiano kufanikisha suala la kufunguliwa uwanja huo uliofungiwa matumizi yake na Serikali, Oktoba mwaka uliopita.

TFF inachukua nafasi hii kuahidi kuwa itasimamia matumizi mazuri ya uwanja huo kwa kutoa elimu kwa wadau ili kuutumia uwanja huo vema ikitambua kuwa ni hazina ambayo imetokana na nguvu na gharama kubwa za Serikali kuujenga uwanja huo.

TFF inatahadharisha mashabiki wa mpira wa miguu kwamba uwanja huo umejengwa kwa gharama kubwa hivyo ni jukumu letu kuutuza na kuutumia vema kwa sababu ni hazina kubwa tuliyonayo na ni miongoni mwa urithi bora kwa vizazi vijavyo.

Kwa sasa tumetuma maombi yetu Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuomba kuutumia uwanja huo kwenye mchezo wa kesho Jumamosi Januari 28, mwaka huu kati Simba na Azam utapigwa kwenye uwanja huo wa Taifa, Dar es Salaam kadhalika keshokutwa katika mchezo kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na Mwadui ya Shinyanga.

Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inaonesha kuwa ligi hiyo huko Mbeya kutakuwa na ‘derby’ kwa maana ya mchezo wa upinzani baina ya timu zinazotoka mkoa mmoja wa Mbeya ambazo ni Tanzania Prisons na Mbeya City utakaochezwa na Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Keshokutwa Jumapili Januari 29, mwaka huu kutakuwa na mchezo mwingine ambao Young Africans itacheza na Mwadui jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Majimaji ya Songea itasafiri hadi Mtwara kucheza na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Jumatatu Januari 30, 2017 kutakuwa na mchezo mwingine kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

..…………………………………………………………………………........................
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: