Wednesday, February 15, 2017

Mwakyembe atembelewa na Uongozi wa TLS


Serikali imekiasa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) kibaki kuwa chombo cha kitaaluma cha kulinda weledi, viwango na maslahi mapana ya uanasheria na kisikubali kuyumbishwa na mihemko ya uanaharakati wa kisiasa isiyo na tija kitaaluma.

Akiongea na ujumbe wa TLS kwenye ofisi yake ndogo ya Dar es Salaam leo  (15/2/17), Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk.  Harrison Mwakyembe amesema TLS ibakie njia kuu kama ilivyo kwa vyama vingine vya kitaaluma nchini, isighilibiwe na michepuko.

Amesema uanzishaji na uendeshaji wa TLS kwa sheria ya Bunge umesukumwa miaka yote na dhamira njema ya Serikali ya kutaka kuilinda na kuilea taaluma ya uanasheria ili ikue na ijenge weledi stahili na hivyo itoe mchango bora katika ujenzi na uendeshaji wa utawala wa sheria nchini.

"Ikiwa TLS sasa inajiona imekua kiasi cha kutosha na sasa inataka iingie  kwenye majukumu ya ziada ya uanaharakati wa kisiasa, Serikali haitasita kuifuta sheria iliyoanzisha TLS ili chama hicho kijisajili chini ya Sheria ya Vyama kama NGOs zingine nchini au ikiwezekana chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa kama vyama vingine vya siasa nchini".

Ameongeza kusema harakati zinazoendelea ndani ya TLS zenye mwelekeo wa kisiasa, zimeifanya ofisi yangu isimame kidogo kukamilisha marekebisho kadhaa ya sheria ya TLS maana hatma ya TLS haieleweki, "it remains in the balance".

Awali, waziri huyo aliueleza ujumbe huo wa TLS ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wa TLS, Wakili Lameck Calleb, kuwa Serikali imefarijika sana kwa ushirikiano mkubwa uliotolewa na chama hicho katika maandalizi ya muswada wa sheria ya huduma ya msaada wa kisheria ambayo imepitishwa na Bunge na sasa unasubiri saini ya Rais wa Nchi kuwa sheria.

Aliongeza kuwa Wizara inaitegemea sana ushirikiano wa TLS hata katika utungaji wa Kanuni za sheria hiyo mpya, mchakato wake ambao tayari umeanza.

No comments: