SIASA

ACT YAHOJI KANUNI EALA


Katika Gazeti la Serikali Toleo Namba 11 la tarehe 17 Machi 2017, Katibu wa Bunge alitangaza rasmi Uchaguzi tajwa hapo juu. Katika Tangazo hilo yaliambatanishwa Masharti ya Uteuzi wa Wagombea. Tangazo hilo ambalo kimsingi ni Sheria limeweka sharti kwamba Vyama vyenye Haki ya kuteua Wagombea ni vile vyenye Uwakilishi Bungeni. 

Kila Chama cha Siasa kilitakiwa kuteua Wagombea 3 kwa kila nafasi inayogombewa isipokuwa tu kwa Kundi C ambapo Chama Cha Mapinduzi hakiruhusiwi kuweka Mgombea.

Vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni vimefanya mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa mujibu wa Kanuni na Tangazo hilo. 

Chama ambacho mimi ni Mbunge wake ( ACT Wazalendo ) pia kimefanya mchakato wake wa Uteuzi.
1.    Wakati Mchakato wa uteuzi unaendelea na kabla ya siku ya uteuzi nimejulishwa kuwa Spika wa Bunge ametoa maagizo kwamba nafasi zinazogombewa ZITAGAWIWA kwa Vyama vya Siasa kulingana na uwiano wa uwakilishi wao Bungeni na hivyo hapatakuwa na uchaguzi bali uteuzi ( allotment of seats instead of election ). 

Uamuzi huu wa Spika unakwenda kinyume na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (ibara ya 50) na vile vile Kanuni za Bunge na Tangazo la Uchaguzi lililotolewa na GN iliyotajwa hapo juu. Uamuzi huu pia unakwenda kinyume na nia ya kanuni ya 12 ya Kanuni za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inasisitiza kuwa ‘kadiri inavyowezekana’ vyama vyote Bungeni viwakilishwe katika Bunge la Afrika Mashariki.

2.    Uamuzi wa Spika pia umeacha kuzingatia ukweli wa HAKI kwamba Chama chochote cha siasa kinaweza kugombea nafasi yeyote katika makundi yote isipokuwa kwamba CCM haiwezi kugombea nafasi ya kundi C peke yake. Tangazo la Uchaguzi linaruhusu Chama cha ACT Wazalendo kugombea makundi yote manne yaliyoainishwa na hivyo uamuzi wa Spika ni kuvunja Kanuni za Bunge. 

Maamuzi ya Mahakama pia yanatamka wazi kwamba Mkataba unataka UCHAGUZI na sio UTEUZI ( Rejea Kesi ya Antony Komu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ). Uamuzi wa Spika unafanya zoezi hili kuwa ni uteuzi ( allotment of seats ) badala ya Uchaguzi.

3.    Vile vile Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge inatumia mgawanyo wa viti kwa makundi yaliyoundwa miaka 15 iliyopita na hivyo kutozingatia mgawanyo wa Jinsia na pande za Muungano kwa makundi mengine. 

Kwa mfano ni CCM peke yake ambayo inalazimishwa na Kanuni kuzingatia uwiano wa Kijinsia na pande za Muungano na hivyo kutokana na kupungua kwa nafasi za CCM katika Bunge la Afrika Mashariki, sura ya Muungano na usawa wa kijinsia kwa uwakilishi wa Tanzania kwenye Bunge hilo inapungua na hivyo kwenda kinyume na Mkataba wa Afrika Mashariki.

Kwa kuzingatia madhara makubwa ya Uamuzi wa Spika kwa kuzuia haki ya vyama vyenye uwakilishi Bungeni kushiriki uchaguzi wa wawakilishi wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki na kwa kupelekea kupunguza sura ya Muungano wa Tanzania na usawa wa jinsia kwa wawakilishi wetu; Na kwa Kuzingatia kuwa Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge inapaswa kubadilishwa na Maamuzi ya Bunge zima (kifungu cha 18 cha Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge );

Naleta kwako Ombi rasmi la kutaka Kamati ya Kanuni za Bunge ikutane mara moja kujadili Maamuzi ya Spika kukiuka Kanuni za Bunge na Tangazo la Uchaguzi. Katika kikao hicho pia Kamati ya Kanuni itazame upya mgawanyo wa Makundi kwa mujibu wa Nyongeza ya Tatu ya Kanuzi za Bunge na kuzingatia uwiano wa pande za Muungano, jinsia na haki za vyama vyenye uwakilishi mdogo zaidi ndani ya Bunge kushiriki katika chaguzi za uwakilishi wa Nchi yetu kwenye Mabunge ya Kimataifa na Kikanda.

Ikumbukwe kwamba tunafanya uchaguzi wa uwakilishi wa NCHI na sio uwakilishi wa Vyama, kazi ya Bunge ni kupeleka watu makini wenye uwezo kutetea maslahi ya Nchi yetu bila kujali udogo au ukubwa wa vyama vya Siasa.

Nawasilisha kwa hatua za haraka kwa maslahi ya Tanzania.

Kabwe Zuberi Ruyagwa Kabwe, MB
Kigoma Mjini

Nakala 

Mnadhimu Mkuu wa Serikali Bungeni 
Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni

About HABARI24 TV

Powered by Blogger.