Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunasikitishwa
na mlolongo wa matukio ya uvunjifu wa amani yanayoshamiri siku hadi siku. Kituo
tunashitushwa na matukio hayo yanayodunisha amani na kumomonyoa misingi ya
demokrasia nchini Tanzania.
Tukio la uvamizi katika mkutano wa ndani wa
Chama cha Wananchi (CUF) uliopelekea kupigwa na kujeruhiwa kwa wanachama na waandishi
wa habari huko Mabibo, Ubungo, Dar es Salaam limezidi kuzua mjadala katika
jamii juu ya hatma ya hali ya usalama kwa taifa. Tunatoa
pole kwa waandishi wa habari, viongozi na wanachama wa Chama cha Wananchi
(CUF).
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaona
kuwa huu ni ukiukwaji mkubwa wa misingi ya demokrasia kwa kuzingatia aina ya
shughuli iliyokuwa ikiendelea. Pia tukio hilo limezua hofu juu ya usalama wa
wanahabari wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo
linazorotesha haki ya kupata taarifa.
Tunaitaka serikali kutofumbia macho matukio
haya yanayoota mizizi kwani kwa kufanya hivyo ni kuhalalisha vitendo vya kihuni
na kuruhusu uvunjwaji wa sheria kiholela.
Kwa kuzingatia umuhimu wa uhuru wa kujieleza
na uhuru wa kukusanyika kituo cha sheria na haki za Binadamu tunapendekeza
yafuatayo;
1. Msajili wa vyama vya siasa kuhakikisha ustawi
mzuri wa vyama vya siasa kwa kutatua migogoro iliyopo ndani na baina ya vyama
vya siasa ili kuepusha matukio ya uvunjifu wa amani na kudumisha ustawi wa
demokrasia.
2. Serikali kuhakikisha usalama kwa raia
wanapokuwa kwenye shughuli zao ili kuepusha hofu kwa wananchi.
3. Vyama vya siasa kutumia uhuru wao kwa mujibu
wa sheria ya vyama vya siasa bila kusababisha uvunjifu wa amani.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
tunataamali jamii yenye kuheshimu na kulinda haki za binadamu.
Imetolewa na:
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji
No comments:
Post a Comment