Juzi tarehe 27 Aprili
2017, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora) Mh. Angela Kairuki
alikabidhi rasmi Ripoti ya zoezi la Uhakiki wa Vyeti ambapo iliripotiwa kuwa
jumla ya watumishi 9932 wanatumia vyeti feki.
Chama cha ACT
Wazalendo kinaunga mkono uamuzi wa serikali kuwachukulia hatua watumishi wote
wa umma waliobainika kutumia vyeti feki ikiwemo kuwafukuza kazi na kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria.
Bila shaka hatua hii itapanda mbegu ya uwajibikaji,
kuchochea uadilifu na kuhakikisha uweledi kwenye utumishi wa umma.
Mbali na kupongeza,
yapo masuala kadhaa yaliyoibuka kwenye zoezi hilo ambayo tunadhani hayakwenda
sawasawa na hivyo basi sisi kwa nafasi yetu tunao wajibu wa kuyakemea ili
kuufanya mchakato huu uende kwa haki:
Mosi, kauli ya Mh.
Rais kuwasamehe wale wataojiondosha kazini wenyewe na kuwafikisha kwenye vyombo
vya sheria na wale wataoendelea kubaki kwenye nafasi zao ni kinyume cha sheria
na katiba ya nchi.
Kisheria Rais hana mamlaka ya kumsamehe mtu
anayetuhumiwa kufanya kosa la jinai iwapo mtu huyo hajafikishwa kwenye vyombo
vya sheria na kuhukumiwa.
Madaraka pekee
aliyonayo . Rais ni kutoa Msamaha kwa wafungwa wanaotumikia kifungo
(President's Prerogative of Mercy) kama alivyofanya hivi karibuni kwenye
Sherehe za Muungano.
Iwapo tutaacha hulka ya viongozi kuchukua
hatua wapendavyo hata kama kwa kusigina sheria za nchi basi tujue wazi tunalipeleka
taifa kwenye "Utawala wa Mtu Binafsi" badala ya "Utawala wa
Sheria".
Pili, madai ya Waziri
Kairuki kuwa mchakato wa uhakiki wa vyeti haujawagusa wanasiasa na wateule wa
Mh. Rais kwa sababu cheti si sifa ya kupatikana kwao unapotosha mantiki ya
zoezi zima na kuweka upendeleo wa dhahiri.
Ikumbukwe kuwa msingi
wa zoezi hili ni kuhakikisha kuwa taifa linabaki na watumishi wenye sifa.
Waziri Kairuki anasema kuwa sifa pekee ya Kikatiba ya Viongozi wa kisiasa ni
kuwa wajue kusoma na kuandika. Jambo ambalo Waziri Kairuki hakutaka kujiuliza
ni kuwa iwapo viongozi wa kisiasa watathibitika kughushi vyeti ambalo ni kosa
la jinai haitawaondolea sifa yao ya uongozi.
Kama Waziri mwenye dhamana ya utawala bora
hakuona kuwa uhakiki wa vyeti kwa viongozi wa kisiasa na wateule wa . Rais kama
vile Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kungehakikisha kuwa viongozi hao
wanakwenda sambamba na viapo na matakwa ya kimaadili?
Uamuzi huu wa
kutowagusa viongozi wa kisiasa katika zoezi hili la uhakiki wa vyeti ni
ushahidi wa dhahiri kabisa wa jinsi serikali inavyohaha kuwalinda baadhi ya
wateule wa Mh. Rais na wanasiasa ambao wametuhumiwa na umma kwa makosa ya
kughushi vyeti.
ACT Wazalendo tunatoa
rai kwa serikali kutanua mawanda ya zoezi hili liguse viongozi wa kisiasa
wa CCM na vyama vya upinzani.
Ado Shaibu,
Katibu wa Itikadi,
Uenezi na Mawasiliano.
30 Aprili 2017
No comments:
Post a Comment