Tuesday, April 11, 2017

ZITTO KABWE-Taifa Limegawanyika, Viongozi Wakuu Hawaliunganishi Taifa


Mheshimiwa Spika,


Katika mwaka 2016 tumeshuhudia mahusiano ya Vyama vya siasa yakiwa mabaya zaidi kuliko wakati wowote tangu mfumo wa vyama vingi uingie nchini. Wakati Mfumo wa Vyama vingi ulipoanza, Miaka ile ya 90, tuliwahi kushuhudia Kiongozi Mkuu wa ngazi ya Waziri Mkuu wa wakati ule, ndugu Sumaye akisema kuwa ili mambo yako (mfanyabiashara) yaende vizuri lazima uwe CCM.

Kauli yake hii ilipingwa nchi nzima, Sumaye alikemewa, akakumbushwa kuwa huo si Utanzania. Sisi wananchi tukayasahau hayo ya miaka ya 90, tukaamini kuwa Vyama na Itikadi tofauti za Kisiasa ni fursa tu ya kupata mawazo, mbinu, nyenzo na namna bora mbalimbali za kuliendeleza Taifa, kwamba sote tuna dhamira njema ya kuleta Tanzanianjema, tukitofautiana tu njia za kuifikia hiyo Tanzanianjema, kwamba sote ni watanzania, na kwamba hatutofautishwi kwa vyama vya siasa, dini, kipato ama makabila mbalimbali yoliyoko nchini. 

Mwaka huu mmoja wa awamu ya tano tumerudishwa miaka ile ya Uwaziri Mkuu wa Sumaye, miaka ile ya kuanza kwa siasa za vyama vingi nchini, miaka ile ya uhasama. Viongozi wetu, waliopaswa kutuweka pamoja, wakiongozwa na Rais, ndio vinara wa kutugawa watanzania kutokana na vyama vyetu na itikadi zetu za kisiasa. Hotuba za Rais akiwa Unguja na Pemba, ni mfano hai juu ya hili, akizidisha pia mpasuko wa kisiasa ulioko Zanzibar. Jambo hili si la Kitanzania.

Sasa hivi Rais wa nchi amezuia kabisa mikutano ya Vyama vya siasa, kinyume na sheria. Katika ibara ya 17 ya hotuba ya Waziri Mkuu, anatutaka "kujenga utamaduni wa masikilizano na kuendesha siasa za Maendeleo badala ya siasa za malumbano, siasa za kuunganisha watu badala ya siasa za kuwagawa na siasa za uwajibikaji badala ya siasa za mazoea".

Hizi anazopendekeza Waziri Mkuu ndio siasa wengi wetu tumekuwa tukihubiri miaka na miaka. Lakini unafanyaje siasa hizi wakati Vyama vya siasa vimezuiwa kufanya mikutano Kwa amri ya Rais? Unahamasishaje maendeleo ya wananchi kama uruhusiwi kufanya mikutano? Unahamasishaje Uwajibikaji kwa wananchi kama unazuiwa kukutana nao? Unafanyaje siasa za masikizano kama Viongozi wa Serikali mnanadi uhasama na mpasuko wa Taifa? Katiba inaruhusu mikutano ya hadhara, sheria inaruhusu, utamaduni na desturi yetu Watanzania inaruhusu, lakini Rais hataki. 

Waziri Mkuu anataka Siasa gani za uwajibikaji wakati Katiba inasiginywa na Serikali anayoiongoza? Kuna Uwajibikaji mkubwa kama kulinda Katiba na Kiapo cha kulinda Katiba na Sheria? Nani Ana uthubutu wa kumwambia Rais kuwa amri zake zinavunja katiba? Amri hii ya Rais iondolewe ili vyama vya siasa viwe na haki ya kufanya mikutano ya hadhara kuchochea Maendeleo, kuwajibisha na kuunganisha Watanzania.

Miaka ya nyuma Vyama vya Upinzani ndio vilikuwa vinalaumiwa kwa siasa za kugawa watu. Leo Viongozi wa Serikali ndio wanaongoza kutoa kauli za kuwagawa Watanzania Kwa vyama vyao vya siasa. Nchi gani tunajenga? Demokrasia gani ya uwajibikaji tunaijenga? 

Leo chombo cha habari kinavamiwa na walinzi wa Rais usiku wa manane. Askari wa Usalama wa Taifa anatoa bastola hadharani kumtishia mbunge. Waziri wa Usalama wa Taifa yupo kimya. Serikali nzima ipo kimya kana kwamba lile ni jambo la kawaida kabisa. Tunajenga nchi ya namna gani? Mambo haya yanadhalilisha sana taasisi ya Urais, jambo ambalo ni kosa la kikatiba.

Nimuombe Waziri Mkuu, ushauri wake huu mwema aupeleke pia ndani ya Serikali anayoiongoza, inauhutaji zaidi. Tunaligawa Taifa, ni wakati sasa wa kuliweka Taifa pamoja.


Hali ya Uchumi ni Mbaya, Watanzania Wamepoteza Matumaini

[Semehu ya 1 ya Hotuba ya ndugu Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (MB) kuhusu Mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kwa mwaka 2017/18]

Mheshimiwa Spika, 

Tangu mwezi Novemba mwaka 2015 nchi yetu ilipata Serikali mpya iliyoanza kazi kwa kasi kubwa haswa katika maeneo ya kupambana na rushwa, ufisadi na kuongeza mapato ya Serikali. Wananchi walikuwa na matumaini makubwa sana kutokana na mwanzo huu, na hata ufanisi katika utendaji wa kazi Serikalini ulianza kuboreka. 

Bahati mbaya, leo tunapokutana kujadili utendaji wa Serikali wa mwaka uliopita na kupanga Bajeti ya mwaka unaofuata wa fedha matumaini hayapo tena, kuna hali kubwa ya kukata tamaa miongoni mwa wananchi. 

Maeneo mengi ya nchi kuna uhaba mkubwa wa chakula na badala ya Serikali na hasa Rais kuwa matumaini Kwa wananchi akiwa Comforter In Chief, kumekuwa na maneno makali ya kuwakatisha tamaa wananchi. Bei za vyakula nchini zimepanda mno kiasi cha wananchi kushindwa kumudu chakula ili waweze kufanya kazi na kukuza Uchumi. 

Taarifa za Serikali kupitia ripoti za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake juu ya hali ya Uchumi ya nchi yetu (Quartely Economic Review na Monthly Economic Review) kwa mwezi wa Disemba 2016 zinaonesha kuwa kuna mfumuko mkubwa mno wa bei za Vyakula, hasa Chakula Kikuu kwa Watanzania - Mahindi, ambapo bei ya chakula hicho kikuu nchini imepanda kwa zaidi ya 30% na kupandisha mno gharama za maisha za wananchi wote nchi nzima.

Leo bei ya kilo moja ya mahindi nchini iko sawa au ni zaidi ya bei ya kilo moja ya mchele kwenye miji mbalimbali nchini, sukari bei juu, mafuta ya kula bei juu nk. Kwa wakati wa mjini hata bei ya gesi kwaajili ya kupikia majumbani imepanda, wananchi wamerudia matumizi ya mkaa, tujiandae na uharibifu wa misitu nchini.

Jana Ofisi ya takwimu ya Taifa imetoa Taarifa ya kuonyesha kuwa Mfumuko wa Bei umepanda kwa kasi na sasa umefika asilimia 6.4 Kwa mwaka unaoishia Machi, 2017. Ibara ya 20 ya Hotuba ya Waziri Mkuu iliyosomwa bungeni inaonyesha mfumuko wa bei wa asilimia 5.2 kwani wametumia takwimu za mwezi Desemba, 2016. 

Ukuaji wa sekta binafsi umedorora na kushuhudia biashara maelfu kwa maelfu zikifungwa na kusababisha ajira nyingi kupotea na ajira chache kutengenezwa. Katka Ibara ya 26 ya Hotuba ya Waziri Mkuu inaonekana kuwa ajira 418,000 zilizalishwa mwaka 2016/17. Lakini Waziri Mkuu hakulieleza Taifa kuwa Hivi sasa Watanzania 1.6m wanaingia kwenye soko la Ajira kila mwaka. Pia Waziri Mkuu hakueleza Taifa ni ajira ngapi zimepotea Kwa viwanda kufungwa au kupunguza uzalishaji na biashara kufungwa. Manispaa ya Ilala peke yake imefunga biashara 2900 na hivyo kupoteza chanzo cha mapato ya Manispaa. Lakini hata mikopo ya Kibenki kwa sekta binafsi imepungua mno, ikiwa ni kiashiria cha mdororo wa sekta binafsi.

Matamko ya viongozi wakuu wa Serikali kuhusu mwelekeo wa Uchumi yanatuma ujumbe hasi kuhusu uwekezaji wa mitaji nchini, na hivi sasa kila mwekezaji kwenye macho ya Serikali anaonekana mpiga dili. Juhudi zote za kuhamasisha uwekaji wa mitaji nchini zilizofanywa tangu Serikali ya awamu ya tatu, zimefutwa katika mwaka Mmoja tu wa Serikali ya awamu ya tano. Hali ni ya kusikitisha sana.

Tatizo jengine kubwa ni suala la ajira, ukiondoa ajira zilizopotea kwa mdororo wa sekta binafsi, lakini pia hakuna ajira mpya serikalini tangu awamu ya tano iingie madarakani. Vijana mbalimbali waliomaliza masomo yao ya Ualimu, Utabibu, Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvivu bado wako mtaani bila ajira kwa mwaka sasa. Hata walioajiriwa mwanzoni ajira zilisitishwa kwa kisingizio cha uhakiki wa watumishi wa Umma.

Yote hayo yana athari kwenye uchumi wa nchi, yamepunguza kipato cha wananchi, yamechangia ugumu wa maisha. Yamefuta matumaini waliyokuwa nayo watanzania na yamewakatisha tamaa. Bunge letu lina wajibu wa kuhakikisha Serikali inarelebisha hayo.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Bungeni Dodoma
April 11, 2017

No comments: