SIASA

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), KUHUSU BAJETI YA WIZARA HIYO, KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2016
_________

1.0 UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb), naomba kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2016/17, pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Mheshimiwa Spika, kabla sijawasilisha maoni hayo, napenda kuchukua fursa hii, kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kunipa nguvu na maarifa zaidi ya kusonga mbele na kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Momba. Pili, napenda kutumia fursa hii kumshukuru, na pia kumpongeza Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb) ambaye ndiye Waziri Kivuli na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika wizara hii, kwa ushirikiano mkubwa anaonipa katika kutekeleza majukumu yangu kama Naibu wake. Kimsingi najivunia kufanya kazi na Waziri Kivuli mchapa kazi, msikivu na mwenye weledi, kama Mheshimiwa Halima Mdee.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika nitumie pia fursa hii kuishukuru Sektretarieti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa msaada wao katika kufanya utafiti wa kina ambao ndio umekuwa msingi wa maandalizi ya hotuba hii. Ninawatia moyo, waendelee kufanya kazi yao kwa weledi kwa manufaa ya taifa hili. 

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuungana na Watanzania wenzangu wote na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutoa pole kwa wazazi, familia na uongozi wa shule kwa wanafunzi 32, walimu na dereva wa Shule ya Lucky Vincent waliopoteza maisha mkoani Arusha mnamo tarehe 6 Mei, 2017 katika maeneo ya Rhotia Marera, wakiwa njiani kuelekea wilayani Karatu kwa ajili ya mitihani ya ujirani mwema kujipima uwezo na shule ya wenzao.

Mheshimiwa Spika, ninapomalizia utangulizi wangu napenda kila Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote kwa ujumla wafahamu kuwa Wizara hii ya fedha ndio inaweza kuwatoa Watanzania kwenye umasikini kama sio kuendelea kuwabakiza katika hali hiyo, kama alivyosema Mtaalamu wa masuala ya fedha na uchumi duniani Bw. Adam Smith  katika kitabu chake cha Wealth of Nations. Mtaalamu huyo alipata kusema kuwa, nitanukuu “no society can surely be flourishing and happy, of which the far greater part of the members are poor and miserable.”  Akimaanisha kuwa “hakuna jamii ambayo inaweza kuwa na uhakika wa furaha na kufanikiwa endapo sehemu kubwa ya watu wake ni masikini na walalahoi” Wizara hii ikitimiza majukumu yake kwa ufanisi, Watanzania walio wengi hawatakuwa masikini kama walivyo hivi leo!

2.0 MAJUKUMU YA WIZARA YA FEDHA

Mheshimiwa Spika, Kutokana na umuhimu wa wizara hii katika maendeleo ya nchi yetu, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inao wajibu wa kuwakumbusha wabunge majukumu ya wizara hii, ambayo ni: 
i) Kubuni na kusimamia utekelezaji  wa sera  za uchumi jumla, 
ii) Kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na nje ya nchi pamoja na matumizi yake, 
iii) Kuandaa na kusimamia  utekelezaji wa bajeti ya Serikali,
iv) Kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kupunguza umasikini katika sekta mbali mbali,
v) Kusimamia deni la Taifa, 
vi) Kusimamia upatikanaji wa rasilimali fedha zinazopatikana katika miradi ya ubia baina ya Serikali na sekta binafsi, 
vii) Kusimamia sera, sheria ,kanuni na taratibu  za uhasibu, ukaguzi wa ndani   na ununuzi wa Umma,
viii) Kusimamia Mali za Serikali,taasisi na mashirika ya Umma  (treasurer registrer),
ix) Kusimamia masuala ya Tume ya Pamoja ya fedha, 
x) Kuandaa na kulipa mishahara watumishi Serikalini,
xi) Kusimamia ulipaji wa mafao na pensheni ya wastaafu, 
xii) Kuthibiti  biashara ya fedha haramu pamoja na ufadhili wa ugaidi. 
Mheshimiwa Spika, kwa majukumu hayo ya wizara, ni dhahiri kwamba mafanikio ya mipango yote tunayopanga kama Taifa unategemea ufanisi katika wizara hii. 

3.0 MAONI YA NYUMA YA KAMBI YA UPINZANI

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Bunge la bajeti la mwaka 2012/13 na 2013/ 2014, kuna mambo ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza yafanyiwe kazi na Serikali ili kuleta tija na ufanisi katika utendaji wa wizara. Kuna ambayo yalifanyiwa kazi, kuna yanayoendelea kufanyiwa kazi na kuna ambayo hayajafanyiwa kazi kabisa.
Mambo ambayo hayajafanyiwa kazi kwa ufanisi ni pamoja na haya yafuatayo:

i. Kupunguza Misamaha ya Kodi hadi kufikia chini ya Asilimia 1 ya Pato la Taifa. 

Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua kadhaa za kupunguza misahama ya kodi. Hata hivyo, hatua husika bado haijafikia lengo la Taifa ambalo lilikuwa ni kukupunguza misamaha hiyo hadi kufikia chini ya asilimia 1 ya pato la Taifa. Kiasi kinachosamehewa kodi kwa mujibu wa ripoti ya CAG (Machi 2017) ni shilingi Trillion 1.1 tu, kiasi ambacho bado kinazidi asilimia 1 ya pato la taifa. Hivyo, bado Serikali inatakiwa kuendelea  kuchukua hatua zaidi . Ni rai ya kambi ya upinzani kwamba Serikali  itaendelea kupitia upya  motisha za kodi  zinazotolewa  kwa lengo la kupunguza  viwango  vya misamaha ya kodi  hadi kufikia 1% au pungufu ya hapo. 

Mheshimiwa Spika, halikadhalika bado kuna tatizo sugu katika udhibiti wa kodi ya mafuta   hususan kwenye kampuni za uchimbaji madini. Ripoti ya hivi karibuni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imebainisha kwamba, kuna kampuni ambazo zilipata msamaha wa kodi ya mafuta ambazo hazikustahili kupata misamaha hiyo. Mathalani ripoti hiyo inaonyesha kwamba,    lita  20,791,072 za mafuta katika  kipindi cha miezi 18  kuanzia mwezi Julai 2014  na Desemba 2015 yalisafirishwa kwenda  kwa mkandarasi  M/S Agreko  Company Limited  ambaye hakustahili  kupewa msahama wa kodi . Jumla ya tamani ya mafuta ilikuwa ni shilingi 10,174,646,166.

Mheshimiwa Spika, endapo pendekezo hili lingetekelezwa ipasavyo, mapato ya Serikali yangeongezeka. Pia,  ingesaidia kupunguza nakisi ya bajeti ya Serikali kwa kutegemea misaada na mikopo ya nje pamoja na mikopo ya ndani.

ii. Kufanya uchunguzi kupitia Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) kuhusu manunuzi ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ya kuzalisha umeme

Mheshimiwa Spika, pendekezo hili lilitokana na matumizi yenye mashaka ya shilingi bilioni 1.4 kila siku kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendesha mitambo hiyo. Katika pendekezo hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, tuliitaka Serikali kuleta taarifa ya uchunguzi huo Bungeni. Mpaka sasa, taarifa rasmi ya uchunguzi huo haijawahi kuletwa katika Bunge hili tukufu. Pia, ikumbukwe kuwa ni kwa kipindi kirefu sasa Serikali ilitoa ahadi ya kubadilisha mitambo ya IPTL itumie gesi badala ya mafuta yenye gharama kubwa, lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa. Kwa mujibu wa CAG moja ya sababu zinazoifanya Tanesco kuwa na Malimbikizo  makubwa  ya madeni   kunatokana na madeni  katika manunuzi ya umeme kutoka kwa wazalishaji huru wa nishati ( IPPs)  na wazalishaji wa dharura wa nishati  (EPPs) watano. Hii inatokana na Tanesco  kununua umeme kwa bei ya wastani wa shilingi  544.65 na kuuza shilingi  279.30 kwa kila unit hivyo  kusababisha hasara  ya shilingi  265.30 kwa kila unit. 

ii) Kuielekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye Maeneo yanayochochea Ukuaji wa Uchumi kama vile Reli na Bandari. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitoa pendekezo hili kwa kuwa uwekezaji wa mifuko hii ulikuwa umelenga kwenye ujenzi wa  majengo makubwa ya makazi  na biashara  ambao unatumia fedha nyingi ,huku mapato yanayopatikana (return on investment) yakiwa ni kidogo jambo linasababisha kuchukua kipindi kirefu kurudisha gharama( Payback period). Kutokana na kuwekeza katika eneo moja, na kumlenga mteja mmoja,   majengo mengi yalikosa  wapangaji na hivyo kufanya mradi mzima uwe ni wa hasara.  Pendekezo hili bado halijafanyiwa kazi na kwa sababu hiyo, bado Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  inaendelea na msimamo wake wa kuendelea kuitaka Serikali kuielekeza mifuko ya hifadhi za jamii kuwekeza kwenye miradi yenye faida ya haraka.
iii) Kutoa taarifa ya hesabu za robo mwaka za kila mfuko wa hifadhi ya Jamii kama ilivyo katika mabenki ili wanachama waweze kupata fursa za kuona utendaji wa mifuko wanakohifadhi fedha zao.

iv) Kuhamishia mifuko yote ya hifadhi ya Jamii kwenye Wizara ya Kazi na Ajira ambayo kimsingi ndiyo inayohusika na hifadhi ya jamii (Social Security).

Mheshimiwa Spika, pendekezo hili lilitokana na kwamba kwa hali ilivyo sasa mifuko hii iko katika wizara tofauti tofauti jambo ambalo linaleta ugumu katika kuidhibiti na kuisimamia. Hoja hiyo mpaka sasa haijatekelezwa.  Mamlaka ya Kusimamia mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) haijaweza kudhibiti kwa ufasaha mifuko yote ya hifadhi ya Jamii nchini. 

3.0 UPATIKANAJI WA FEDHA KUTOKA HAZINA

Mheshimiwa Spika, Kwa muda mrefu sasa Serikali kupitia wizara ya fedha imekuwa ama ikichelewa kupeleka fedha kwenye wizara na idara mbalimbali za Serikali au kutoa fedha pungufu na katika mazingira mengine kutokutoa fedha kabisa kama ambayo zimeidhinishwa na Bunge. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali kuandaa makisio yake ya mwaka, yanayoshabihiana na makusanyo ya mapato!!Kwa kufanya hivyo, inatarajiwa kwamba shughuli zilizopangwa zitatekelezwa kama zilivyopangwa. 

Mheshimiwa Spika, Kamati zako za kudumu za Bunge (Rejea Taarifa zote za Kamati, Bunge la Bajeti 2017),nazo zimeona tatizo hili kutokana  na ukweli kwamba katika wizara na idara za Serikali wanazozisimamia utoaji wa fedha za maendeleo umekuwa finyu sana! Hali hii inaondoa umuhimu wa  Bunge kukaa kwa gharma kubwa kupitisha bajeti ya Serikali ambayo haitekelezwi ipasavyo. Tofauti na awamu za utawala zilizotangulia, Serikali hii ya awamu ya nne ambayo imekuwa ikijigamba kwamba imefanikiwa kukusanya mapato kwa kiwango cha hali ya juu kuzidi makisio iliyoyaweka, kila mwezi imekuwa na hali mbaya zaidi  katika utekelezaji wa bajeti na hasa bajeti ya maendeleo kuliko awamu zilizopita.

 Mheshimiwa Spika, Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kwamba; hizo fedha amabazo Serikali inajisifu kukusanya kwa wingi zinakwenda wapi??  Au zinatumika vibaya – kwa maana ya matumizi ambayo hayajaidhinishwa na bunge? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili, ni kwa nini haikutoa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya maendeleo kwa takriban wizara zote, kwa kisingizio kwamba kulikuwa na upungufu wa fedha lakini wakati huo huo inautangazia umma kwamba imekusanya mapato mengi kuzidi lengo la makusanyo?

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mifano michache ya jinsi ambavyo Serikali haikutoa fedha za maendeleo kwa ukamilifu wake katika baadhi ya wizara ili tuweze kujipima kama tunasonga mbele kama taifa  kuiendea Tanzania ya viwanda au Serikali inawahadaa wananchi kama ilivyozoea. 
1. Ofisi ya Makamu wa Rais  ( Mazingira)

Mheshimiwa Spika, Kati  shilingi bilioni   10.9  za miradi ya Maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge,  ni shilingi  bilioni 1.2 tu  sawa na asilimia  11.3 ya fedha ya fedha hizo zilizotolewa na hazina kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa maneno mengine bajeti ya Maendeleo ya Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira haikutekelezwa kwa asilimia 88.7. Ikimbukwe kwamba fedha hizi ndizo hutumika kupambana na uharibifu wa mazingira yetu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa na athari kubwa sana kwa wananchi kama vile ukame, mafuriko, magonjwa ya mlipuko, njaa nk. Serikali kutotoa fedha za maendeleo katika Ofisi hii,  ili kulinda mazingira yasiharibiwe maana yake ni kubariki athari mbaya zinazotokana na uharibifu wa mazingira ziendelee kuwaangamiza wananchi. Ndio maana hatushangai kuona mkuu wetu akikataza  tuzungumzie habari za njaa, mafuriko au matetemeko kwa kuwa hana mpango nazo, na  ndio maana fedha hazitoki.

2. Tume ya kudhibiti Ukimwi 

Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni  10.1za miradi ya maendeleo  zilizoidhinishwa na Bunge, ni shilingi  bilioni  2.7 tu sawa na asilimia 27  ya bajeti  ndio zimetolewa. Kwa maneno mengine vita dhidi ya maambukizi ya UKIMWI hapa nchini si kipaumbele cha Serikali hii ya awamu ya tano.

3. Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi

Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni 897.6 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ni shilingi bilioni 500.4 sawa na asilimia 55 ndizo ambazo zilikuwa zimetolewa hadi kufikia Machi, 2017. Hata hivyo, mchanganuo wa fedha hizo ni kwamba, shilingi bilioni 427 (asilimia 48) zilikuwa ni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na shilingi bilioni 470 (asilimia52) zilikuwa ni kwa ajili ya kugharamia miradi halisi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo katika sekta ya elimu zinaonekana kuwa nyingi kwa kuwa zimechanganywa pamoja na fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwmba; ni muhimu tukatenganisha  kati ya miradi ‘halisi ya maendeleo’ na ‘ Mikopo ya wanafunzi’ ili kuweza  kupata picha halisi  ya nini hasa kinakwenda kutumika kutatua changamoto za uboreshaji/ upanuzi/ujenzi  wa miundombinu na shughuliza utafiti  katika sekta hiyo.

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye miradi halisi ya maendeleo, kati ya miradi 16 ambayo ilitengewa fedha  katika mwaka wa fedha  2016/17 Kamati ya Bunge ya Maendelelo na Huduma za Jamii  ilifanya  ukaguzi wa miradi 5 tu sawa na  na 12% ya miradi yote. Kati ya miradi hiyo  mitano , ni miwili tu iliyopatiwa fedha! Tena kwa kiwango kidogo sana. Ifuatayo ni Hali halisi ya miradi mitano iliyokaguliwa: 

i) Mradi wa upanuzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) – Mradi namba 6361. Bunge liliidhinisha  shilingi bilioni 4, hakuna fedha yoyote iliyopelekwa 
ii) Mradi wa ukarabati wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam  (Mradi namba 6350). Bunge iliidhinisha shilingi  bilioni 9.4, hakuna fedha yoote iliyopelekwa 

iii) Mradi wa Hospitali ya Mloganzila (Namba ya Mradi 6364).Chuo kiliomba shilingi 14,549,727,933 (BN. 14.5) hakuna fedha iliyopelekwa mpaka 13/Mei /2017 wakati wa hotuba ya bajeti ya wizara ya elimu inasomwa.

iv) Mradi wa Mfuko wa Utafiti na Maendeleo wa COSTECH (Namba ya Mradi 6345. Katika Malengo ambayo nchi  nchi imejiwekea , ni kutenga 1% ya Pato la Taifa. Hata hivyo, mfuko huu ulitengewa  kiasi cha shilingi  bilioni 12.8 tu  sawa na 0.012% ya pato la Taifa . Pamoja  na udogo huo , kiasi kilichotolewa ni shilingi  bilioni 4.07 tu (sawa na 31.7%). Kati ya hizo fedha Mfuko mkuu wa hazina uliotakiwa kutoa  bilioni 8 ilitoa  shilingi bilioni 1.5 tu na TCRA iliyotakiwa kutoa   shilingi  bilioni 4.8 ilitoa shilingi bilioni 2.57 tu.

v) Mradi wa ujenzi wa DIT teaching Tower (Namba ya Mradi 4384). Mradi huu una umri wa miaka 11 (2006- 2017)…bado unasuasua, hakuna pesa na Matokeo  yake gharama za mradi zimeongezeka  toka bilioni 5 mpaka bilioni 9.


4. Wizara ya Maji 
Tume ya Taifa ya umwagiliaji- Fungu 05:
Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni 35.3 za miradi ya maendeleo zilizodhinishwa na Bunge, ni shilingi bilioni 2.9 tu sawa na asilimia 8.4 zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji  wa miradi hiyo. Kwa upande wa usambazaji wa maji ,mijini na vijijini kati ya shilingi bilioni 915.1  zilizotengwa,  zilizotolewa ni shilingi bilioni 181.2 sawa na 19.8% ya fedha  zote za miradi ya Maendeleo ndizo zilizotolewa.  Kwa utekelezaji duni namna hii wa bajeti ya maendeleo katika sekta ya  maji ni matusi kwa watanzania ambao uhaba wa maji umewafanya waishi kama wanyama.  Ule usemi wa Serikali wa kumtua mama ndoo ya maji, kwa mazingira haya  ni dhihaka  kwa akina mama wote wa nchi hii ambao wanaendelea kusota  na kukumbana na kila aina ya kadhia katika kutafuta maji. Ikumbukwe kwamba hawa ndio mtaji mkubwa wa kura waliyoipa ushindi Serikali hii na sasa imeshindwa kutumiza ahadi yake ya kuwatuma akina mama ndoo za maji kwa kushindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo iliyodhinishwa na Bunge.

5. Wizara ya Viwanda:
Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni 42.1 zilizotengwa, wizara ilipokea shilingi bilioni 7.6 tu sawa na 18.6%. Kwa utekelezaji huo wa bajeti, ni aibu kwa Serikali kutumia Kauli mbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda’ kama kampeni ya kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia viwanda.

6. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa:
Mheshimiwa Spika, Wizara hii,  ambayo ni nyeti kwa usalama wan chi yetu, nayo ilikumbana na panga ambalo limezikumba wizara mbalimbali. Moja ya mradi muhimu sana  ni mradi wa  Defence Scheme ( mradi namba  6103) na kutekelezwa chini ya  Kifungu namba  2002- Military Research  na Development Fungu 57. Mradi huu, ulitengewa  jumla ya shilingi  bilioni 151.1. Mpaka mwezi Machi,2017 - ikiwa ni robo ya tatu ya mwaka  wizara ilikuwa imepokea shilingi  bilioni 30 tu sawa na 20%  tu! Mbali na mradi tajwa hapo juu  kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje  Ulinzi na Usalama   fedha za miradi ya maendeleo ziliwasilishwa ni 14.5% tu, yaani Bunge liliidhinisha shilingi   bilioni 230 , pesa zilizotolewa  hadi  Machi 2017 ni shilingi bilioni 33.9. Halafu tunaitangazia dunia kwamba tuna lengo la kuwa na jeshi dogo la kisasa lenye weledi- kwa bajeti ipi?

7. Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi: 
Mheshimiwa Spika, Kilimo kiliidhinishiwa shilingi 101,527,497,000 (bilioni 101). Kiasi kilichotolewa ni  shilingi 3,369,416,66 (bilioni. 3.369) sawa na  3.31%. Kwa upande wa mifugo na uvuvi, kiasi cha shilingi 15,873,215,000 (bilioni 15.8) kiasi kilichotolewa  ni bilioni 1.2. Sawa na 8% . Kwa maneno mengine, Kilimo ambacho tunasema kwamba ndio uti wa mngongo wa uchumi wa Tanzania, bajeti yake ya maendeleo haikutekelezwa kwa takriban  asilimia 97. Serikali inahubiri Uchumi wa Viwanda ikijua fika kwamba viwanda hivyo haviwezi kuendelea bila ukuaji katika sekta ya kilimo, lakini haitoi fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya Kilimo.  Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba;   ama Serikali imefilisika ila haitaka kukiri hivyo, au kuna tatizo kubwa la afya ya akili (mental health) miongoni mwa watendaji wa Serikali. Haingii akilini kwamba ile sekta ambayo inategemewa kuleta hayo mapinduzi ya viwanda haipewi fedha za kutosha, halafu Serikali inaendelea kuhubiri viwanda – vitatoka wapi?

8. Wizara ya Maliasili na Utalii , fedha za  ndani za miradi ya maendeleo  zilizotengwa ni shilingi  bilioni 2. Fedha zilizotolewa ni mil 156,688,000 sawa na 8%

9. Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi, fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa ni shilingi bilioni 25.30 . Fedha zilizotolewa mpaka sasa ni shilingi  bilioni 7.63 tu.

10. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano:

Mheshimiwa Spika, wizara hii ilitengewa  fedha za Maendeleo kwa mchanganuo ufuatao:

Ujenzi iliidhinishiwa shilingi trilioni 2.17 zilizotolewa ni shilingi trilioni 1.07 sawa na asiliia 58.7
Uchukuzi iliidhinishiwa shilingi trilioni 2.49 zilizotolewa ni shilingi bilioni 761.5 sawa na asilimia 30.5
Mheshimiwa Spika, Uchambuzi uliofanywa hapo juu unaonyesha wazi kwamba, ufanisi wa Serikali ya awamu ya tano katika utekelezaji bajeti ya Miradi ya maendeleo na mpango wa kuwaondolea umasikini watanzania  ni  kwa wastani wa  0%- 20%. Wizara pekee iliyoweza kuvuka 50% ni Wizara ya Ujenzi na inafahamika kwamba yapo ‘maslahi mapana’ yanayohitaji kulindwa katika wizara hiyo. . 
Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM katika vipindi mbalimbali , imekuwa ikituambia  kwamba Chama hicho kupitia  Dira  2025, na 2020 (SMZ), Mwelekeo  wa sera za CCM katika miaka 2000 -2010-2015 kimeelekeza  suluhisho la kuondokana na hali ya uchumi kuwa nyuma na tegemezi na kufanya modenaizesheni ya uchumi. Mchakato wa Modenization  ya uchumi na kuitoa  nchi  yenye uchumi tegemezi kuelekea uchumi wa kisasa utazingatia vipaumbele vifuatavyo:
i) Kutilia Mkazo katika matumizi ya maarifa ya kisasa (Sayansi na Teknolojia)
ii) Kuandaa rasilimali watu katika maarifa na mwelekeo
iii) Kufanya mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi
iv) Kufanya mapinduzi ya viwanda ambavyo ndivyo kiongozi wa uchumi wa kisasa
v) Mapinduzi  katika nishati na miundombinu ya kisasa

Mheshimiwa Spika, Suala la Msingi ambalo wabunge wa pande zote mbili tunapaswa kutafakari na kujiuliza, kutokana na uchambuzi uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hapo juu, hivi kweli itakapofika 2020 na 2025 malengo (i-v) yatatimia? Na kama nafsi zetu zinatuambia kwamba hayatatimia, tunajipanga vipi kutumia kipindi hiki cha bajeti KUJISAHIHISHA ili mwaka ujao wa fedha TUSIJIULIZE maswali hayahaya? !

4.0 OFISI YA MSAJILI WA HAZINA NA UHAI WA MASHIRIKA YA UMMA
Mheshimiwa Spika, Kulingana na Sheria ya Msajili wa Hazina na kifungu Na. 6 cha Sheria ya Mashirika ya Umma Na.16 ya mwaka 1992, Msajili wa Hazina ana majukumu ya kusimamia  uendeshaji wa shughuli za Mashirika na Taasisi nyinginezo za Umma kwa kushirikiana na Bodi za Wakurugenzi za Mashirika husika.  Hata hivyo, hali ya baadhi mashirika yetu sio ya kuridhisha, na kwa sababu hiyo,  hatua a haraka zinahitajika ili kuweza   kuyanusuru.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali imetaja baadhi ya mashirika ya umma pamoja na changamoto zinazoyakabili mashirika hayo na kushauri hatua za haraka zichuliwe ili kuyanusuru. Miongoni mwa Mashirika hayo ni kama ifuatavyo: 

i. TANESCO: 
Mheshimwa Spika, TANESCO inakabiliwa na Malimbikizo  makubwa  ya madeni yanayotokana na manunuzi ya umeme kutoka kwa wazalishaji huru wa nishati ( IPPs)  na wazalishaji wa dharura wa nishati  (EPPs). Hii inatokana na Tanesco  kununua umeme kwa bei ya wastani wa shilingi  544.65 na kuuza shilingi  279.30 kwa kila unit hivyo  kusababisha hasara  ya shilingi  265.30 kwa kila unit. Kwa Upande mwingine TANESCO inadai taasisi mbalimbali za Serikali fedha nyingi ambapo inashindwa kujiendesha kutokana na kutolipwa kwa fedha hizo. Mathalani TANESCO inaidai Wizara ya nishati na madini kodi ya pango  ya shilingi  bilioni 1.12  Kwa ujumla TANESCOinaidai Serikali  ( Mpaka tarehe 30 Juni 2016) shilingi  bilioni 144,854 sawa na 67.4% ya deni  lote la umeme. Deni lililobaki  kwa wateja binafsi  ni shilingi  bilioni 70 sawa na  asilimia 33

ii. Mifuko ya Hifadhi ya NSSF, PPF, PSPF na LAPF: 
Mheshimiwa Spika, Mifuko hii inakabiliwa na tatizo la kushuika kwa mapato ya uwekezaji kunakotokana na kutokuwepo kwa ufanisi wa menejiment  katika kusimamia mikopo  iliyotolewa. Aidha, kuna usimamizi hafifu wa kuratibu na kudhibiti madeni ya muda mrefu na kuchelewa kulipwa kwa madeni ambayo mifuko inaidai Serikali. Serikali imekuwa na tabia ya kutumia huduma au kukopa katika taasisi zake bila kufanya malipo.
iii. Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF)

Mheshimiwa Spika, NHIF ilitoa mkopo  wa shilingi  bilioni 44.29 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya  cha Chuo Kikuu cha Dodoma. Mkopo ulitolewa bila mkataba wala udhibitisho wa udhamini. Matokeo yake mpaka sasa haijulikani haki na wajibu wa kila upande ,utaratibu wa urejeshwaji wa mkopo halikadhalika ulipaji wa riba ya mkopo !hali hii inaisababishia  mfuko kupoteza fedha za wanachama  endapo mkopaji atashindwa kuwa mwaminifu(kama ambavyo viashiria vinavyojionyesha) na itakuwa ngumu  kupata haki mahakamani.

iv. Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF)

Mheshimiwa Spika, mfuko huu ni mhanga wa kurushwa fedha zake na Serikali.  Kutorejeshwa kwa gharama za uendeshaji za mfuko wa afya ya jamii (CHF) shilingi bilioni 1.20 kunaiweka CHF kwenye wakati mgumu kujiendesha.  Fedha hizi izilitakiwa ziwe zimerejeshwa na Serikali kutokana na gharama ilizotumia kwenye miradi ya CHF kama ilivyoainishwa kwenye hati ya makubaliano. Kutokulipwa kwa madeni haya na Serikali kunauongezea mfuko mzigo mkubwa wa kifedha hivyo kusababisha  kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na kushindwa kupanua  wigo wa shughuli zake.

v. Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)

Mheshimiwa Spika, shirika hili nalo lina changamoto ya kutolipwa deni na Serikali. TANAPA inaidai   Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki  jumla ya shilingi bilioni 2.4 ikiwa ni kodi ya pango ya ofisi za Wizara zilizopo katika jengo la TANAPA mkoani Arusha.

5.0 MSAJILI WA HAZINA KUTOKUWA NA UWEZO WA KUSIMAMIA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII

Mheshimiwa Spika, Ukirejea hotuba yetu ya Kambi Rasmi ya Upinzai Bungeni ya mwaka 2012/13 na 2013/2014 tulitoa ushauri kwa Serikali kufanya mambo yafuatayo kuhusu mifuko ya hifadhi za jamii kama ifuatavyo: 

Kwamba; Serikali ihamishie mifuko yote ya hifadhi ya Jamii kwenye Wizara ya Kazi na Ajira ambayo kimsingi ndiyo inayohusika na hifadhi ya jamii (Social Security). Pendekezo hili lilitokana na ukweli kwamba kwa hali ilivyo sasa mifuko hii iko katika Wizara tofauti tofauti jambo ambalo linaleta ugumu katika kuidhibiti na kuisimamia. Na ni ukweli usiopingika kwamba Mamlaka ya kusimamia mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imeshindwa kuisimamia mifuko kwa ufasaha.  
Na kwamba; Msajili wa Hazina awe na mamlaka ya kuisimamia kama anavyofanya kwenye Mashirika mengine ili kumwezesha  kufuatilia ipasavyo utendaji  na uwekezaji  unaofanywa na mifuko hiyo. Hoja hizi mpaka sasa hazijapatiwa majibu, hali ambayo inazidi kuhatarisha uhai wa mifuko yetu. 

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukosefu wa umakini katika kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii, yapo matukio ambayo kwa hali zote hayakuzingatia weledi jambo ambalo linaweza kusababisha hasara kubwa katika mifuko hiyo. Matukio  hayo ni pamoja na: 
Mkopo wa PSPF Shilingi Bilioni 58 kwa Bodi ya Mikopo na Marejesho ya Mikopo ya Wanafunzi Shilingi Bilioni 51.1 NSSF
Taarifa za fedha  za NSSF  zinaonyesha kwamba  waliwekeza kwenye  viwanja (Benki ya Ardhi) vyenye thamani ya shilingi bilioni 97.2 wakati kukiwa hakuna mipango na upembembuzi  yakinifu  kuhalalisha  sababu za kuwekeza  katika rasilimali  kinyume na aya 3.3  ya sera ya uwekezaji  ya mwaka 2012 inayoitaka  NSSF kuwekeza rasilimali zake  katika uwekezaji unaolipa  zaidi  ili kuweza kuleta  mafanikio kwa wanachama wake.
Shirika pia linakopesha taasisi ambazo hazikidhi vigezo na masharti kutokana na ukweli kwamba wakopeshwaji wanapaswa kuwa wanachama wa NSSF, lakini mikopo imekuwa ikitolewa  kwa watu ambao sio wanachama ! 
Mradi wa Tuangoma ambapo  mfuko uliingia mikataba mbalimbali yenye thamani  ya shilingi bilioni 165.4 kwa ajili ya kijiji cha setilaiti  katika shamba  la Dungu Tuangoma  Kigamboni pasipo kufanya upembuzi yakinifu…

Mheshimiwa Spika, mifano hiyo hapo juu inadhirisha kwamba Wizara ya Fedha haitimizi majukumu yake ipasavyo na haiko makini katika kuisimamia mifuko ya hifadhi ya Jamii.

6.0 RIPOTI YA MSAJILI WA HAZINA KUHUSU UTENDAJI  WA KAMPUNI YA NDEGE

Mheshimiwa Spika, Kampuni hii ilianzishwa mwaka 2002 kwa mujibu wa sheria ya Makampuni  sura 212 kama kampuni ya biashara ya usafiri wa anga. Mwezi Oktoba, 2016,  Serikali ilinunua ndege sita (mbili kati ya hizo zimeshafika na kuanza kazi). Kwa mujibu wa kitabu cha Mpango wa maendeleo 2017/18 , katika mwaka wa fedha 2017/18 zimetengwa shilingi bilioni 500 fedha za ndani kwa ajili ya kukamilisha malipo ya ndege 3 zilizosalia. Kwa lugha nyingine ndege zote sita zitaligharimu Taifa si pungufu ya shilingi bilioni 1000 (Trillion 1).

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya ofisi ya Msajili wa Hazina kwenda kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu ya tarehe 29 Machi 2017 inabainisha mambo yafuatayo:
i) Imekuwa vigumu  kwa  ofisi ya msajili  kufanya uchambuzi wa  kina wa utendaji  wa ATCL  kutokana na kutokuwepo kwa  taarifa za kutosha za kampuni.
ii) Mahesabu ya kampuni yaliyokamilika ni ya mwaka 2014/15. Mahesabu hayo  hayajatimizwa  na kupitishwa na bodi, hali ambayo  imemsababishia Msajili wa Hazina  kutoweza kuchambua  na kubainisha  hali halisi  ya uwekezaji  ilivyo sasa  hususani  madeni na mali za kampuni.
iii) Imekuwa vigumu kubaini hali halisi ya utendaji  na hali ya ukwasi (liquidity ratio) wa kampuni kwa kutumia viashiria vya utendaji  kutokana na kampuni kutokuwa na hesabu( financial statements) kwa muda mrefu.
iv) Uongozi  uulizwe  kueleza  mikakati  iliyonayo kuwezesha  kampuni  kujiendesha kwa faida na tija.
v) ATCL inatakiwa kuhakikisha inakuwa na hesabu zilizokaguliwa kila mwaka, mpango wa biashara, mpango au sera ya uwekezaji, mpango wa kurithisha utaalam. (Taarifa inaonyesha kwamba uongozi wa ATCL umeahidi kwamba ifikapo June 2017 mpango wa biashara na sera ya uwekezaji vitakuwa tayari).
vi) Kutokuwa na wataalam wa kutosha katika  masuala ya usafiri wa anga hususan marubani, wahandisi, wataalam wa uongozi na uendeshaji wa biashara ya suafiri wa anga  na waongoza ndege
vii) Kampuni inakabiliwa na madeni makubwa  ambayo yanachangia  ukuaji wa matumizi ya kampuni na hatimaye kushindwa kutekeleza baadhi ya shughuli zake za maendeleo!

Mheshimiwa Spika, Kwa maelezo hayo ya ofisi ya msajili wa hazina , Kambi ya upinzani  inataka  Serikali ilieleze Bunge hili tukufu ni kwa nini inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine ikiwa kampuni yetu ya ndege ina mapungufu makubwa namna hii? Je Serikali haioni kwamba kwa kuendelea na mpango wa kununua ndege ikiwa shirika la ndege lina matatizo makubwa namna hiyo ni kupoteza fedha za walipa kodi kwa kuwa kuna dalili zote shirika hilo kuanguka kama ilivyotokea awali?

7.0 MAFAO YA WASTAAFU (PENSHENI)

Mheshimiwa Spika, Mafao ya wastaafu katika nchi hii yameendelea kuzua migogoro mbalimbali na manung’uniko katika jamii. Kuna makundi mengi yenye malalamiko, kuanzia Wanajeshi, waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wastaafu waliokuwa watumishi wa Umma ambao wamebaguliwa na Sheria ya Mafao kwa Watumishi wa Umma, ya mwaka 1999 (The Public Service Retirement Benefits Act, Cap. 371, R.E. 2002). 

7.1 SHERIA YA MAFAO YA UTUMISHI WA UMMA

 Mheshimiwa Spika, Sheria hii, pamoja na kufuta Sheria ya Pensheni ya mwaka 1954 (The Pensions Ordinance of 1954, Cap. 371 of the Laws of Tanzania), bado ilibakiza matumizi ya Sheria hiyo kwa watumishi wa umma waliokuwa wakipokea mafao yao kwa Sheria na kanuni za Sheria iliyofutwa. Hali hii inajidhihirisha kwenye kifungu cha 73 na 84 cha Sheria ya mwaka 1999.

Mheshimiwa Spika, Kwa sasa asilimia kubwa ya watumishi hao wanalipwa mafao yasiyoendana na hali halisi ya maisha. Wako kwenye hali ngumu ya udhalilishwaji na umaskini uliopindukia. Wengi wao hupewa shilingi elfu ishirini (Sh. 20,000/=) tu kwa mwezi! Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za Binadamu na aibu kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza yafanywe mabadiliko ya Sheria zote zinazohusu mafao kwa wafanyakazi katika sekta zote za ajira nchini. Pia, kipaumbele kiwekwe kwenye marekebisho ya Sheria ya Pensheni ya mwaka 1999 na kuwafanya wale wote waliokuwa wakistahili kupewa pensheni zao kwa mujibu wa Sheria ya Pensheni ya mwaka 1954 wanapewa pensheni hizo kwa kuzingatia viwango vipya vinavyokidhi mahitaji ya msingi ya Binadamu na Utu, siyo viwango vya mwaka 1954.

7.2 DHULUMA DHIDI KWA WALIOKUWA WAFANYAKAZI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Spika, Tarehe 24/02/2016 wawakilishi wa  wafanyakazi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki  walimwandikia  barua   Mheshimiwa John Pombe  Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  wakimtaka aingilie kati dhuluma waliofanyiwa na Serikali ya CCM kwa kutokulipwa stahiki zao kikamilifu baada ya Jumuiya kuvunjika na kila nchi kupewa mgao wake kwa malipo ya wafanyakazi  wa Jumuiya wanaotoka katika nchi zao! 

Mheshimiwa Spika, Mwaka mmoja na miezi minne imepita, Wastaafu hawa hawajapata majibu,  Kambi Rasmi ya Upinzani ni sauti ya wasio na sauti, ikiwa ni miaka 40 toka Jumuiya hiyo ivunjike inalileta suala hili mbele ya Bunge lako tukufu ili Serikali  itoe ufafanuzi wa madai ya watanzania hawa  wanaodai kwamba bado hawajaaalipwa  kikamilifu stahiki zao  zilizotokana na ajira zao kwa kuzingatia  kumbukumbu,taratibu  na Sharia za ajira zao ambazo zilihitimishwa  kwa nguvu  ya Mkataba  wa East African Community Mediation Agreement 1984 ulioidhinishwa  na kutiwa saini  na Mamlaka (The Authority ) ambao  ni marais wa Afrika Mashariki wakati huo. Pamoja na Mkataba huo kulitayarishwa  pia Acturial Report  ya 1986  iliyotoa ufafanuzi wa malipo hayo.

Mheshimiwa Spika, Viashiria vya wizi na dhuluma dhidi ya watanzania hawa vilianza  mwaka 1987 pale Mkataba wa The East African Community Mediation Agreement 1984 (Ulioidhinishwa  na kusainiwa  na Marais wa nchi wanachama, akiwemo hayati Julius Kambarage Nyerere)  ulipoletwa kwenye Bunge ili upate uthibitisho  kama sheria rasmi ya nchi . Katika hali ya kushangaza Serikali ilinyofoa  baadhi ya vipengele muhimu vya Mkataba mama ( Article 1,2,6,13,16,17 na 18)  kabla ya kuupeleka Bungeni  kwa uthibitisho. Tendo hili la Serikali lilikuwa ni kinyume kabisa  na mwongozo wa Article 95 ya Mkataba wa Jumuiya ya Africa Mashariki (The Treaty for East African Co-operation) . 

Mheshimiwa Spika, Kitendo hichi cha dhuluma kilichofanywa na Serikali ya CCM kilipunguza  nguvu nna thamani ya mafao ya watanzania hawa  na hususani kifungu cha 1(n) ambacho kiliweka  bayana  kwa kutoa  maagizo na mwongozo  uliotakiwa kufuatwa  katika ukokotoaji  na ulipaji wa mafao. Hatua hii ya Serikali kwa kiwango kikubwa imekuwa ikiathiri wazee wetu hawa kwani Mahakama zetu zimekuwa zikitoa  uamuzi wake  kwa kutumia Mkataba wa ndani uliochakachuliwa !

Mheshimiwa Spika, Swala la wazee hawa ( Watanzania zaidi ya 28,831) halitofautiani  sana migogoro ya mirathi , hasa pale baba mkubwa  anapoteuliwa kusimamia mirathi  ya marehemi  ndugu yake  ambae aliacha  mali na watoto wadogo. Mara nyingi ndugu hawa wa baba hugeuka wakatili , hunyanyasa na kuwadhulumu  au mara nyingine kuwapunja  haki mayatima  hao pale wanapoanza kudai mali zao kwa kisingizio eti waliwalea na kuwasomesha! Hichi ndicho kilichowakuta wafanyakazi wa Jumuiya mbele ya baba yao Mlezi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano!  

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2005 iliundwa Kamati ya muafaka baada ya Serikali kuomba suala limalizwe nje ya Mahakama. Kwa ridhaa ya Mahakama Kuu, Kamati husikwa iliundwa na watu 10 toka Serikali Kuu ikiongozwa na Bwn. Ramadhani Khija (ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muafaka na baadae alikuwa Katibu Mkuu Hazina. Na watu 10 wakiwakilishwa upande wa  wastaafu wakiongozwa  na Ndugu  Alfred Kinyondo  kama Mwenyekiti wa Wastaaafu. Baada ya majadiliano ya  ya miezi mitatu  Muafaka ulifikiwa  na kupelekwa kwa Waziri wa Fedha , wakati huo Bwana Basil  Mramba. Makubaliano yakiwa Serikali itawalipa  jumla ya shilingi billion 450 kwa wastaafu 28,831

Mheshimiwa Spika, Makubaliano haya yalithibitishwa na kauli ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin Mkapa  katika kilele cha sherehe  za wafanyakazi  za Mei Mosi  tarehe 1/05/2005 Songea, alitamka rasmi  kwamba Serikali yake imeridhai  kulipa Tshs. 419 bilioni  ikiwa ni malipo ya wastaafu  wa Jumuiya hiyo na mashirika yake japo kwa awamu  na alimuagiza Waziri wa Fedha wakati huo ndugu Basil Mramba  kutekeleza maamuzi hayo kwa haraka ( Kiambatanisho)!

Mheshimiwa Spika, Katika hali ile ile ya dhuluma kama ilivyotokea katika uchakachuaji wa Mkataba  kama nilivyoainisha hapo juu, Serikali hiyo hiyo iliyoingia makubaliano katika Kamati ya mwafaka, ikaandaa Deed of Settlement yenye kuonyesha kwamba  kiasi cha shilingi bilioni 117 zitalipwa kwa wastaafu 31,831, kutoa shinikizo kwa wastaafu kupitia wakili wa ndugu Lukwaro wasaini. Mkataba ulisainiwa Kwa shinikizo (21/09/2005) Mahakama ikatoa hukumu siku hiyo hiyo!..Siku ya pili 22/09/2005 Serikali ikachapisha majina ya wastaafu 28,831 na kuagiza wakachukue malipo yao  kuanzia tarehe hiyo hiyo 22/09/2005!!

Mheshimiwa Spika, Swali la kujiuliza hapa ni kwa miujiza gani Serikali iliweza kukokotoa ndani ya siku moja  stahiki za watumishi wote 28,831 ambao wako kada tofauti na waliohudumu kwa muda , mishahara na vyeo tofauti ndani ya nusu siku/siku moja??
Serikali ikijua kwamba inafanya hila ilifanya  siri sana katika ‘kukokotoa mahesabu’  bila hata kuwashirikisha wawakilishi wa wastaafu, ni pale tu Mstaafu alipofika  kuchukua hundi yake  na kuona payment voucher , ndipo alipoweza tambua kuwa alicholipwa  hakiendani na stahihi yake! 

Mheshimiwa Spika, Dhuluma kama hii hatuwezi kuacha iendelee kutafuna Taifa letu kudhulumu wazee waliolitumikia Taifa na Jumuiya ni laana kubwa, laana ambayo haturuhusiwi kuiacha kama Taifa! Hivi kwa nini hatujiulizi kwa nini hawa wazee wetu kwa miaka yote wamekuwa wakisisitiza kwamba wamedhulumiwa?? Kwa nini nafsi yao hairudi nyuma licha ya vitisho mbalimbali wanavyokabiliana navyo?? Kwa nini ni wastaafu hawa tu kati ya wengi ambao hawachoki kuililia Serikali yao (baba yao Mlezi) iwape urithi halali walioachiwa na baba yao (Jumuiya) wakati anafariki?? 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali, kupitia Waziri wa Fedha ambaye Hazina iko chini yake, ilieleze Bunge hili tukufu ni lini Serikali itafanyia kazi kwa usahihi na haki madai ya wastaafu hawa?? 

8.0 HALI YA UCHUMI WA NCHI 

2.1 Kuendelea Kupanda kwa Mfumuko wa Bei

Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei umeendelea kupanda siku hadi siku kutokana na sera mbovu za Serikali ya CCM jambo linalopelekea wananchi wengi wenye kipato duni kuumia.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu (Monthly Economic Review) iliyotolewa mwezi Aprili, 2017 mfumuko wa bei umepanda kutoka asilimia 5.4  mwezi Machi, 2016 mpaka kufikia asilima 6.4 mwezi Machi, 2017.

Mheshimiwa Spika, kupanda huku kwa mfumuko wa bei kumeathiri kupanda kwa bei za chakula kama vile mahindi, mihogo, mtama, mchele, ndizi, dagaa wakavu, sukari na mboga za majani.  Gazeti la kila siku, Mwananchi, limeripoti tarehe 3 Aprili, 2017 kupitia uchunguzi uliofanywa katika masoko mbalimbali na kubaini kuwa bei za mazao zimepanda sana. Kwa mfano bei ya maharage imepanda kutoka shilingi 1,800 kwa kilogramu 1, mpaka kufikia kati ya shilingi 2,700 mpaka 3,000.

Mheshimiwa Spika, mazao mengine yaliyopanda bei kwa ukubwa usiokuwa wa kawaida ni pamoja na Sukari kutoka bei elekezi ya Serikali shilingi 1,800 kwa kilogramu 1, mpaka kufikia shilingi 2,500. Mchele nao umepanda kutoka 1,200 kwa kilogramu 1 mpaka kufikia 2,600.  Unga wa Sembe nao umepanda kutoka shilingi 1,200 kwa kilogramu 1 mpaka kufikia shilingi 2,000.  

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako tukufu juu ya hatua stahiki zinachokuliwa ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei nchini. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa majibu ndani ya Bunge lako tukufu kuwa ni lini itabadilisha sera zake za fedha na matumizi ya Serikali ili kudhibiti mfumuko wa bei unaofanya maisha ya wananchi wa Tanzania kuwa duni na kushindwa kumudu gharama za maisha. 

8.2 Uwepo wa Njaa na Hifadhi Duni ya Chakula

Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani njaa imeendelea kuiathiri nchi kwa kiwango cha kutisha. Serikali ya Rais Kikwete katika awamu ya nne ilipofika mwezi Machi, 2015 iliacha hifadhi ya chakula katika Ghala la Taifa jumla ya tani 452,054. 

Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano, haina mpango wa kununua chakula cha hifadhi, ilipofika Mwezi Machi, 2016 miezi mitano tu baada ya Rais Magufuli kuapishwa, hifadhi ya chakula katika ghala la Taifa ikashuka kwa asilimia 85 mpaka kufikia kiasi cha tani 68,727. 

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni sera ya Serikali ya awamu ya tano kutonunua chakula cha kutosha kwa ajili ya akiba katika ghala la Taifa. Ilipofika mwezi Machi, 2017 akiba ya chakula katika ghala la Taifa la hifadhi ya chakula ilikuwa ni tani 86,444

Mheshimiwa Spika, ripoti ya Benki Kuu (Monthly Economic Review) iliyotolewa mwezi Aprili, 2017 imeonesha kuwa Serikali ya awamu ya tano haijanunua chakula chochote wala kuuza ndani ya mwezi Machi, 2017. 

Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali ya awamu ya tano kutonunua hifadhi ya chakula ni hatua ya kuwatia kitanzi na kufanikiwa kuwanyonga kiuchumi Watanzania zaidi ya asilimia 70 ambao kazi yao kubwa ni kulima mazao ya chakula na kuuza katika ghala la hifadhi la Taifa. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali itoe majibu mbele ya Bunge lako tukufu na mbele ya Watanzania wote, kuwa ni kwanini Serikali hainunui tena chakula kwa ajili ya kuweka akiba na kuwainua wananchi wake kiuchumi kutokana na wengi wao kutegemea kilimo kama chanzo cha mapato yao. 

8.3 Mzunguko wa fedha, Riba na Hali ya Mikopo

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu (Monthly Economic Review) iliyotolewa mwezi Aprili, 2016 na Aprili, 2017 ilipofika  mwezi Machi, 2016 mikopo ya Benki za Kibiashara kwa sekta binafsi ilishuhudia ukuaji wa asilimia 23.6 kwa mwaka, na ilipofika mwezi Machi, 2017 ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ukapungua kwa kasi ya ajabu mpaka kufikia asilima 3.7 kwa mwaka. 

Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Benki Kuu inasema kuwa upunguaji huo wa mikopo kwa sekta binafsi unapunguza ukuaji wa mzunguko wa fedha. Sehemu ya ripoti hiyo ukurasa wa 3 inasema kuwa “This development mirrors the slowdown in the growth of money supply”

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha inaboresha sera za Benki kuu juu ya uratibu madhubuti ya mzunguko wa fedha ili kuzuia anguko la kiuchumi litakalotokana na sekta binafsi kutopata fedha za mikopo zinazotarajiwa kutumiwa katika usisimuaji wa uchumi kutokana na shughuli za kiuchumi kuongezeka. 

Mheshimiwa Spika, Kinachoendelea hivi sasa kwa sekta binafsi kukosa mikopo ya kibiashara na mikopo binafsi kunaathiri ukuaji wa pato la mwananchi mmoja mmoja hivyo kuongeza mzigo wa ugumu wa maisha kwa wananchi. 

Mheshimiwa Spika, hata hivyo kutokana na sera zisizotabirika za Serikali ya awamu ya tano, sekta ya mikopo hususani katika riba ya mikopo imeendelea kuathirika. Ripoti ya Benki kuu imendelea kusema kuwa kiwango cha riba ya mikopo (lending rate) kiliendelea kupanda kutoka asilimia 16.26 mwezi Machi, 2016 mpaka kufikia asilima 17.58  mwezi Machi, 2017. 

Mheshimiwa Spika, Kiwango kikubwa cha riba kinachotozwa nchini kinarudisha nyuma juhudi za kuwakwamua Watanzania kiuchumi, hivyo basi, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ya awamu ya tano, kuhakikisha inatoa majibu ya haraka iwezekanavyo juu ya hatua inazozichukua kuhakikisha kiwango cha riba za mikopo kinapungua ili kurahisisha ongezeko la wakopaji miongoni mwa Watanzania wenye nia ya kukopa na uwezo wa kurudisha unaozuiliwa na kiwango kikubwa cha riba ya mikopo. 


8.4 Tafrani ya Sera ya Serikali kuweka Fedha BoT

Mheshimiwa Spika, haijaeleweka (uncertainties) mpaka sasa endapo Serikali ya awamu ya tano inafuata falsafa ipi katika ujenzi wa uchumi wa nchi kutokana na Sera yake ya kuzuia mashirika ya Serikali kutunza fedha katika mabenki ya kibiashara, kuondoa jumla ya bilioni 5 kutoka mabenki ya biashara na kuzitunza katika akaunti za Benki Kuu (BoT).

Mheshimiwa Spika, hata ongezeko la riba za mikopo katika benki za biashara linatokana na uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano kuondoa fedha katika mabenki ya biashara jambo lililopunguza kiasi cha fedha ‘liquidity’ na kupelekea kupungua kwa amana katika benki hizo jambo linalolazimisha benki za biashara kuongeza kiwango cha riba ili kujipatia unafuu wa kibiashara.

Mheshimiwa Spika, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya uchumi, wameonya kuwa kitendo cha Serikali kukosa falsafa inayoisimamia katika ujenzi wa uchumi na kitendo cha Serikali kufanya maamuzi yasiyotabirika (uncertainities) kunatuma ‘signal’ kwa wawekezaji kusita kuwekeza fedha zao ndani ya uchumi wa Tanzania kutokana na hofu zinazotokana na Serikali ya awamu ya tano kuibuka na sera zisizoshirikishi kila mara. 

Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Serikali kuondoa fedha katika mabenki ya biashara ni hatua ya kuamua kuiangamiza sekta binafsi ambayo inauhusiano wa moja kwa moja na ukuaji wa pato la kila Mtanzania na pia ukuaji wa pato la Taifa. 

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Benki kadhaa za kibiashara zimerekodi hasara katika hesabu zao kutokana na uamuzi huo. Gazeti la The Citizen, tarehe 11 mwezi Agosti, 2016   liliripoti kuwa uamuzi wa Serikali kuhamisha fedha kwenye mabenki ya biashara kumesababisha benki kadhaa kupata hasara. Benki zilizorekodi hasara ni pamoja na Barclays Bank Tanzania (hasara ya Shilingi bilioni 8.2), TBI Development Bank (hasara ya Shilingi bilioni 6.27), Stanbic Bank Tanzania (hasara ya shilingi bilioni 2.40)

Mheshimiwa Spika, Gazeti hilo hilo la The Citizen, tarehe 31 mwezi Oktoba, 2016  liliripoti benki kadhaa kuendelea kupata hasara iliyopelekewa na uamuzi wa Serikali kuondoa fedha katika mabenki ya biashara. Benki zilizorekodi hasara ni pamoja na CRDB Bank (hasara ya shilingi bilioni 1.9) na Amana Bank (hasara ya milioni 195)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ikubaliane na hoja ya kuamua kuwa na falsafa moja ya ujenzi wa uchumi na kuacha kutoeleweka kuwa inasimamia mfumo upi wa uchumi. Falsafa hii itajenga misingi itakayozuia viongozi wa kisiasa wasio na ujuzi wala weledi na taaluma ya uchumi kuacha kuibuka na matamko yanayopelekea anguko la uchumi wan chi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kukubaliana na ukweli kuwa kuzipeleka fedha za mashirika ya Serikali kutunza katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu sio suluhisho la kuzuia matumizi mabaya ya fedha wala sio njia ya kuzuia wizi na ubadhirifu wa fedha za umma. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Ramsi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ya awamu ya tano kuelewa kuwa njia salama ya Serikali kuzuia wizi wa fedha za umma  sio kuzificha fedha katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu; kwa kuwa kwa vyovyote vile lazima zitatolewa ili zitatumike kugharamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya umma, njia sahihi ya kuzuia wizi ni kuimarisha usimamizi wa fedha (finance management) ndani ya mashirika ya umma na Serikali, kuimarisha sera za matumizi ya fedha kwenye miradi ya kimkakati na kuziba mianya ya rushwa katika mifumo rasmi ya matumizi ya fedha za umma. 

Mheshimiwa Spika, baada ya kuanza kuzitunza fehda za umma kwenye akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu, sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulielezea Bunge lako tukufu kuwa ni hatua zipi inazozichukua ili kuhakikisha mifumo ya matumizi ya fedha za umma katika mashirika ya umma na Serikali kuu inaimarishwa ili kuziba mianya ya rushwa kubwa kubwa za kimfumo zinazowanufaisha ‘PEP’ (Political Exposed Personalities) kama vile Wakurugenzi, Makatibu wakuu, na Mawaziri. 

Mheshimiwa Spika, Mtindo unaotumiwa na Serikali ya awamu ya tano kutuza fedha za umma Benki Kuu badala ya kuziweka kwenye benki za biashara ili zisisimue uchumi wa nchi na kuimarisha sekta binafsi na kukuza biashara nchini ni njia za kizamani (traditional methods), zimepitwa na wakati na hazina tofauti na baba wa nyumba anayeficha fedha kwenye kibubu chini ya uvungu wa kitanda wakati angeweza kwenda kuzihifadhi katika amana za benki ili ziingizwe katika mfumo rasmi wa mzunguko wa fedha. 

9.0 TUME YA PAMOJA YA FEDHA (FUNGU 10)

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 133 inatambua uwepo wa  Tume ya Pamoja ya Fedha na Ibara ya 134 inaelezea majukumu ya Tume kuwa ni yafuatayo:
a) Kuchambua mapato na matumizi yanayotokana na, au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano na kutoa  mapendekezo kwa Serikali mbili kuhusu mchango na mgao wa kila mojawapo ya Serikali hizo;
b) Kuchunguza kwa wakati wote mfumo wa  shughuli za fedha wa Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali mbili;
c) Kutekeleza majukumu mengine ambayo Rais  ataipatia Tume au kama Rais atakavyoagiza, na kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Kifungu cha 18(3) cha Sheria ya Tume (The Joint Finance Commission Act) ya mwaka 1996, Sura ya 140, Tume itawasilisha mapendekezo yake au ushauri unaohusiana na kazi yake Serikalini kupitia kwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano wa Tanzania. 

Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia Kifungu cha 18 cha Sheria, Tume imekuwa inawasilisha mapendekezo yake Serikalini kupitia Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano wa Tanzania, ambaye humpatia mapendekezo hayo Waziri mwenye dhamana ya Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya hapo kila upande hupeleka mapendekezo hayo kwenye Baraza la Mawaziri kwa kupitia utaratibu wa kawaida wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kilio kikubwa toka upande wa pili wa muungano kuhusu Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu, 

9.1. KANUNI (FORMULA) YA KUCHANGIA GHARAMA ZA MUUNGANO 

Mheshimiwa Spika, Kumbukumbu zinaonyesha kuwepo kwa makubaliano kati ya Mawaziri wa Fedha na SMT na SMZ ikionyesha kima cha mchango wa Zanzibar kuwa ni wastani wa shilingi milioni 12 kwa mwaka kuanzia mwaka wa 1964/65 mpaka machi, 1977. Kiwango hiki kilikatwa kutokana na pato la Ushuru wa Forodha na kodi ya Mapato iliyokuwa inakusanywa na SMT kutoka upande wa Zanzibar. Kufuatia agizo la Halmashauri Kuu ya CCM kuwa mapato ya kila upande yaingie kwenye Hazina ya SMT kwa Tanzania Bara na Hazina ya SMZ kwa Tanzania Zanzibar, yalifikiwa makubaliano kwamba kila upande uchangie gharama za mambo ya Muungano kwa msingi (fomula) wa uwiano wa idadi ya watu na pato la Taifa. Hata hivyo, kumekuwa na changamoto kadhaa kuhusu uchangiaji wa gharama zikiwemo zifuatazo;

Mheshimiwa Spika, SMZ inatoa hoja kwamba “formula” hiyo inaelekea kuchangisha kila Mtanzania wa Tanzania Zanzibar kiasi kikubwa zaidi ya kiwango anachochangishwa kila Mtanzania wa Tanzania Bara. 
2) SMZ inatoa hoja kuwa baadhi ya shughuli ambazo zimehusishwa katika mambo ya kuchangia kimuungano siyo mambo ya Muungano na hivyo kutaka yafanyiwe mchanganuo na ufafanuzi zaidi ili kufikia maelewano. Maeneo hayo ni pamoja na yanayohusisha gharama ya; 

(i) Michango kwa mikataba ya kimataifa (External Contributions) ambayo imeridhiwa na Jamhuri ya Muungano kama vile ILO, GATT, PTA, SADC, WHO, UNEP, UNIDO, UNDP, CCC na IBRD. 
(ii) Pensheni za Viongozi wa kisiasa. 
(iii) Pensheni za marupurupu ya viongozi wa Kitaifa. 
(iv) Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano hususani Usalama wa Taifa. 
(v) Mahakama ya Rufani na sikukuu za kitaifa. 
(vi) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya SMT; na 
(vii) Mambo mengine ya kimuungano ambayo hayakuorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. 
3) SMZ kutokuwa na mapato ya kutosheleza mahitaji ya bajeti yake. 
4) SMZ inatoa hoja kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 114 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni lazima mchango wa SMZ utolewe baada ya SMZ kukubali ushauri na mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha iliyoundwa na Katiba ya Muungano Ibara ya 133. Hadi sasa wajumbe wa Tume hiyo hawajateuliwa na Sheria ya kuiwezesha kutekeleza kazi zake haijatungwa. 

9.2. MAPENDEKEZO KWA MUJIBU WA UTAFITI WA TUME YA MAREKEBISHO YA KATIBA

Mheshimiwa Spika, Katika uchambuzi wa Masuala ya Fedha yanayohusu Mambo ya Muungano masuala mbalimbali yamejitokeza ambayo yanahitaji kupatiwa ufumbuzi; 
(i) Ugumu wa kubaini mapato na matumizi ya Muungano yasiyotokana na kodi 

(ii) Kutoanzishwa kwa Akaunti ya Fedha ya Pamoja 
Kutokuanzishwa kwa Akaunti ya Fedha ya Pamoja1, kunasababisha kutokuwekwa pamoja mapato ya Muungano kwenye Akaunti hiyo ambayo ni mchango wa Serikali mbili (SMT na SMZ) kwa ajili ya kugharamia Mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa mrejesho ni kwanini hadi sasa akaunti ya pamoja ya fedha kati ya Serikali hizi mbili haijafunguliwa na ni hatua gani hadi sasa zinatumika kubaini matumizi halali ya Muungano na matumizi ambayo siyo ya muungano?

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 tume ya pamoja ya fedha ilitengewa bil 1.374 lakini hadi feb 2017 Tume ilikuwa imepatiwa mil 686 sawa na 50%. Mhe Spika mwenendo wa upelekaji wa fedha kidogo imegeuka kuwa tabia ya serikali kwenye kila fungu. Kwa mwenendo huu hali ya nchi ni itaendelea kudumaa kila kukicha. Pamoja na umuhimu wa tume kusimamia masuala ya fedha za muungano lakini bado serikali haioni umuhimu wa kitengo hichi mana sera tuliyojiwekea ya mgawanyo bado ni kitendawili kikubwa. 

Mheshimiwa Spika, kama taifa tunapaswa kuheshimu makubaliano yetu ili tuweze kuulinda muungano wetu kwa vitendo. Maana kwa  mwenendo wa sasa wa magawanyo serikali ya mapinduzi Zanzibar inapaswa kupokea 21% na serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania 79%, hii ni kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri anayesimamia masuala ya Muungano aliyoitoa Bungeni tarehe 24/04/2017. Pamoja na umuhimu wa makubaliano bado serikali haiyafuati kabisa.

Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali ilieleze bunge lako tukufu ni kwa nini mgawanyo wa fedha wenye lengo la kudumisha muungano na kusaidia usawa wa kimaendeleo haufuatwi? Na kwa nini fedha zinazotengwa kwa ajili ya Tume hii haziendi kama zilizotengwa?
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2017/18 Tume inaliomba Bunge kuwapatia shilingi bilioni  1.286 kiwango hiki kikiwa pungufu kwa asilimia 6 ya fedha zilizotengwa kwa mwaka 2016/17. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kufahamu kupungua huku kwa bajeti hasa ni kutokana na nini?

10.0 OFISI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

Mheshimiwa Spika, Majukumu ya kisheria ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yameainishwa Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama ilivyorekebishwa)  na kufafanuliwa na Sheria ya Ukaguzi ya Umma, Na. 11 ya mwaka 2008 (kama ilivyorekebishwa) na kufafanuliwa na Kanuni za Ukaguzi wa Umma za mwaka 2009.

Mheshimiwa Spika, licha ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuanzishwa na Katiba ya Nchi, na majukumu yake kuainishwa na Katiba pamoja na sheria ya ukaguzi ya Umma, Ofisi hii imekuwa haitendewi haki kibajeti. Katika mwaka wa fedha 2016/17 bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya ofisi ya CAG jumla ya shilingi bilioni 44.7 zilitengwa. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 13.8 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi bilioni 18.5 fedha za matumizi mengineyo na shilingi bilioni 12.2 ni fedha za maendeleo. Hata hivyo fedha zilizopokelewa  kutoka hazina hadi mwezi februari 2017, ni shilingi bilioni 31.699 sawa na asilimia 54.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kushindwa kupeleka fedha kama inavyotakiwa kwa ofisi hii ya Mkaguzi, kumepelekea ofisi hii kukumbana na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kushindwa kufanya ukaguzi katika maeneo yafuatayo;
a. Sekretariat ya SADC 
b. Vyama vya siasa
c. Ofisi za Mahakama katika mikoa 21(Mahakama za mwanzo, mahakama za wilaya na mahakama kuu)
d. Kaguzi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika halmashauri 105
e. Wakala za Serikali (GPSA, TIA, TIRA,SELF na PPAA)
f. Ukaguzi wa mafuta yanayo safirishwa kwenda nchi jirani
Pia ofisi hiyo imeshindwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa vyombo vya kusimamia  fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina fahamu kwamba Ofisi ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali ndiyo imeokoa fedha nyingi za Serikali kutokana na matumizi au ubadhirifu unaofanywa na watendaji wasio waaminifu. Hivyo basi, kitendo cha kutokuipatia fedha kiukamilifu maana yake ni kutoa mwanya kwa matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inadhani kutokuipatia fedha ofisi hii ni kitendo cha makusudi kutokana na ukweli kwamba matumizi mengi ya serikali ya awamu ya tano hayafuati taratibu za kiuhasibu. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali kulieleza Bunge hili kwa nini haikutoa fedha za kutosha kwa CAG na pia ilileze Bunge nini madhara ya kufanya ukaguzi katika taasisi zilizotajwa.


11. MPANGO WA MATOKEO MAKUBWA SASA (BRN)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na utaratibu wa mpango wa matokeo makubwa sasa, mpango huu ulitoka nchini Malaysia ambapo Serikali ya awamu ya Nne ilikwenda huko na kuja nao hapa kwetu, na kitendo hicho kikawa chini ya kitengo cha “Presidential Delivery Bureau. Tatizo kuwa ni kwamba  “copy and paste”  haikuangalia ni mazingira gani wenzetu wa Malaysia wanaifanyia kazi hiyo BRN kwenye sekta mbalimbali, Mfano kwenye sekta ya elimu Malyasia ilikuwa na mkakati kama nchi kusomesha wanafunzi 10,000 nje ya nchi kila mwaka. Tanzania ilichotoka nacho ni kuongeza ufaulu wa sekondari kwa kushusha alama za ufaulu, maana yake ni kuongeza watu wasiokuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira. 

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kitengo hicho ambacho kilikuwa chini ya ofisi ya Rais hakikufanya kazi yake vyema na hivyo Serikali ya awamu ya tano ikaamua kukivunja. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuleta Bungeni utendaji wa miradi yote iliyokuwa inatekelezwa chini na BRN.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa  kuanzishwa kwa BRN ulikuwa ni maanuzi ya baraza la Mawaziri kama ilivyokuwa uamuzi wa kuuzwa kwa nyumba za Serikali umamuzi ambao hadi leo umelitia hasara kubwa Taifa letu na kuleta kashfa mbaya kwa viongozi wetu wakuu wa nchi. 

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mpango wa Matokeo makubwa sasa ulitumia fedha nyingi za walipa kodi,
Na kwa kuwa Mpango huo umeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa;
Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuleta mchanganuo wa matumizi ya fedha zilizotumika kutekeleza mpango huo ambao umeshindwa na kulieleza Bunge hili namna itakavyotekeleza yale malengo ya mpango huo.

10.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia hotuba yangu kwa kumnukuu mtaalam wa masuala ya fedha Bw. Adam Smith aliyesema:“  A man whose whole life is spent in performing a few simple operations, of which the effects are perhaps always the same, or very nearly the same, has no occasion to exert his understanding or to exercise his invention in finding out expedients for removing difficulties which never occur. He naturally loses, therefore, the habit of such exertion, and generally becomes as stupid and ignorant as it is possible for a human creature to become.”

Kwa tafsiri isiyo rasmi alisema kuwa “Mtu ambaye maisha yake yote yanatumika kufanya mambo machache marahisi ambayo labda kila mara huwa yale yale, anakosa muda wa kuongeza ufahamu wake au kutumia ubunifu wake kutafuta njia za mafanikio ambayo katu hayawezi kutokea. Mtu huyo mara zote hushindwa, na hivyo juhdi zake zote hugeuka kuwa ujinga na upumbavu kama ambavyo ni rahisi kwa mwanadamu kuwa hivyo”

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itimize wajibu wake ipasavyo katika kusimamia masuala ya fedha, ili isije ikaingia katika kundi hili analozungumzia Adam Smith. 

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.________
David Ernest Silinde (Mb)
K.n.y MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI KATIKA
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
31 Mei, 2017

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.