Monday, May 8, 2017

NI KILIO TAIFA NZIMA-MKUSANYIKO WA TUKIO NZIMA LA KUWAAGA WANAFUNZI WA AJALI ARUSHA,

Miili ya watu 32 wakiwemo wanafunzi 29 wa Lucky Vicent waliopata ajali ya gari May 6, 2017 imeagwa leo May 8, 2017 ambapo Makamu wa Rais Samia Suluhu aliwaongoza watanzania kuiaga miili hiyo katika Uwanja wa Kumbukumbuku ya Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Kutoka katika Uwanja wa Kumbukumbuku ya Sheikh Amri Abeid millardayo.com imezipata picha za baadhi ya matukio uwanjani hapo.

Watu wa Huduma ya Kwanza wakimpatia huduma mmoja wa wazazi walioondokewa na watoto wao, Arusha

Majeneza yaliyohifadhi miili ya marehemu wakati wa tukio la kuwaga, Arusha

Mzazi akipatiwa msaada wa huduma ya kwanza

Waombolezaji wakiwa ndani ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, Arusha


Unavyoonekana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid ukiwa umejaa waombolezaji
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan leo tarehe 8-May-2017 ameongoza mamia ya wananchi wa mkoa wa Arusha na Mikoa ya Jirani katika kuaga miili ya wanafunzi 32,walimu Wawili na pamoja na Dereva Mmoja wa shule ya Lucky Vicent katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha waliopata ajali katika eneo la Rhotia wilayani Karatu mkoani Arusha.

Katika hotuba yake kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi katika tukio la kuaga miili hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewahakikishia waombolezaji kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na chenye majonzi mazito kwa kuondokewa na wapendwa wao.

Amehimiza wananchi kote nchini kuungana katika msiba uliotokea kwa kuwafiriji wafiwa katika kipindi hiki kigumu na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali peponi.

Makamu wa Rais pia ameiagiza Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Jeshi la Polisi nchini,walimu, wazazi na walezi wawe makini katika kuhakikisha kuwa sheria za usalama barabarani zinazingatiwa kwa kuchukua hatua stahiki za kulinda watoto hasa wanapotumia vyombo vya moto kwenye shughuli zao za kimasomo.

Amesema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuepusha matukio ya ajali ambayo yanaweza kuzuilika kote nchini.

Makamu wa Rais amewataka madereva nchini kuzingatia sheria za usalama barabarani na waache kutumia pombe na dawa za kulevya ili kuepukana na ajali ambazo zinagharimu maisha ya wananchi.

Makamu wa Rais pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta na Wakenya kwa ujumla kwa kuungana na Wananchi wa Tanzania katika msiba uliotokea.

Katika kuaga miili ya wanafunzi, walimu na dereva katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha, Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta amewakilishwa na Waziri wa Elimu wa nchi hiyo Fred Matiang’i.

Ibada na Dua ya kuaga miili hiyo, imehudhuriwa na Mawaziri mbalimbali ikiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mohammed Aboud,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene, Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, Viongozi wa vyama vya siasa na Viongozi wa Dini.
Maelfu ya wananchi wa ndani na nje ya mkoa wa Arusha wamejitokeza kuwaaga wanafunzi,walimu na dereva wa shule ya Lucky Vicent waliofariki katika ajali ya gari juzi. Mageti ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid yamelazimika kufungwa kutokana na idadi kubwa ya waombolezaji huku wengine wakiendelea kuwasili.Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali wamehudhuria zoezi hilo wakiongozwa na Makamu wa rais Samia Suluhu

TAZAMA VIDEO HAPA CHINI
Maelfu ya wananchi waliojitokeza uwanjani

MIILI YA WANAFUNZI WALIOFARIKI KWENYE AJALI IKISHUSHWA UWANJANI


TAZAMA PICHA



No comments: