TAARIFA
KWA UMMA
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinasikitishwa kuona kiwango
cha vifo vitokanavyo na ajali za barabarani nchini Tanzania kinazidi kupanda
kulinganisha na nchi ambazo zipo salama zaidi na zenye magari mengi duniani.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ambazo huchapishwa kila mwaka inakadiriwa
kuwa watu 3,000 hupoteza maisha na 30,000 wanajeruhiwa vibaya barabarani kila
siku duniani, huku kiwango kikubwa zikiripotiwa kutoka nchi zenye uchumi wa
kati na wa chini ikiwemo Tanzania. Tatizo
la ajali za barabarani limekua tatizo kubwa la kiafya duniani kote, nchini
Tanzania ajali za barabarani ni chanzo namba mbili cha jumla vifo vya watu
ikiongozwa na ugonjwa wa malaria.
Mwenendo wa Takwimu za vifo vitokanavyo na ajali za
barabarani sio wa kuridhisha hata kidogo, mwaka 2009 iliripotiwa jumla ya ajali
3,406 zilizosababisha vifo vya watu 502, mwaka 2010 kulikua na jumla ya ajali
4,363 zilizosababisha vifo vya watu 683, kwa kipindi chote hadi kufikia mwaka
2015 idadi ya vifo kwa mwaka imepanda kufikia vifo vya watu 3, 468 katika jumla
ya ajali 8,337 kwa mwaka huo. Mwaka 2016 jumla ya watu 3,256 walipoteza maisha
kwenye jumla ya ajali zote zilizotokea nchini. Idadi hiyo imepungua kwa jumla
ya vifo vya watu 212 ukilinganisha na mwaka jana.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kupitia tafiti zake za
kila mwaka huainisha sababu zinazochangia kukithiri kwa ajali za barabarani
pamoja na kutoa mapendekezo kwa serikali kukabili tatizo la ajali za
barabarani.
Hatua mbali mbali zimechukuliwa kimataifa kwa
kupitisha mikataba inayoweka vigezo vya kiusalama ili kupunguza tatizo la ajali
za barabarani, kwa mujibu wa ibara 6(3)
ya Mkataba juu ya Usafirishaji, Mawasiliano na Hali ya Hewa katika Kanda ya
Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, 1996 ili inchi iweze
kuyafikia malengo ya usalama barabarani nchi wanachama zilikubaliana kuanzisha
sera itakayolenga kuoanisha sheria za usalama barabarani, kuchukua hatua za
udhibiti kuhusiana na magari, madereva, na shuguli za barabarani pia kuonanisha
na kutekeleza viwango husika vya utaalamu.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binaadamu kinatoa rai kwa serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupita Wizara ya Mambo ya Ndani kuangalia
upya na kufanya tathimini ya makubaliano ya mkataba huo kwa kuangalia Sheria,
Sera na Kanuni za usalama barabarani ili kupunguza idadi ya vifo vinavyoendelea kukithiri kutokana na
ajali za barabarani.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinaendelea kusisitiza
Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani kusimamia misingi ya
usalama wa magari pamoja na vyombo vingine vinavyotumia barabara kuzingatia
kanuni za usalama barabarani.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa
mapendekezo yafuatayo kwa Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani;
·
Kusimamia kanuni zinazoainisha idadi salama
ya abiria kulingana na uwezo wa gari husika. Kwa mfano, ajali ya
iliyotokea Arusha ilihusisha zaidi ya watu 30 kwenye gari aina ya coaster
ambalo halina uwezo wa kubeba idadi hiyo kiusalama.
·
Kusimamia kanuni zinazotaka abiria na
dereva kufunga mikanda ya usalama ndani ya gari.
·
Kutoa tahadhari za kiusalama wa mfumo wa
usafirishaji kwa kuzingatia taarifa ya hali ya hewa. Ikiwemo kuzuia baadhi ya
magari kusafiri kipindi ambacho hakuna uhakika na usalama wa barabara kwa
sababu za hali ya hewa.
·
Kuhakikisha magari ya watu binafsi na ya
abiria yanafuata taratibu za kuwa na bima ili kuweza kufidia abiria yanapotokea
majanga ya ajali.
·
Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara
kuhakiki ubora na usalama wa magari.
·
Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara
kuhakiki weledi wa madereva wa magari.
·
Kusimamia kanuni zinazoweka taratibu za
udhibiti wa mwendo kasi.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito kwa
Kamishna wa Bima kutengeneza hifadhi ya kanzidata kwa mambo yanayohusu bima za
magari na kuanzisha mfuko wa kuwalipa fidia waathirika wa magari yasiyokatiwa
bima.
Pia, serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kuboresha mifumo ya usafirishaji ikiwemo barabara kwa kuweka alama
za tahadhari kwenye maeneo hatarishi. Maeneo hayo yanahusisha maeneo yenye kona
kali, maeneo yenye miinuko mikali, maeneo yenye matuta ya barabarani, maeneo
yenye madaraja, na maeneo yenye barabara mbovu au zinazoendelea kutengenezwa
pamoja na maeneo yote hatarishi kwa usafirishaji wa abiria na mizigo.
Kupitia msiba huu mzito kwa taifa LHRC inaendelea
kuungana na wananchi wote kwa kutoa pole kwa waathirika (majeruhi) wa ajali,
familia, ndugu na Taifa kwa ujumla kwa ajali iliyotokea na zilizotokea kabla na
baada ya ajali ya Arusha ndani ya kipindi hiki.
Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
Amina
Imetolewa
leo tarehe 08/05/2017 na,
Anna
Henga,
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji
Kituo
cha Sheria na Haki za Binaadamu
No comments:
Post a Comment