SIASA

ACT WAMKANA ALIYEPOKELEWA CCM MBELE YA RAIS MAGUFULI,WAMVAA POLEPOLE AACHE PROPAGANDA

HALI YA MAISHA NI NGUMU Pole Pole AACHE PROPAGANDA ZA KITOTO DHIDI YA ACT Wazalendo

Juzi tarehe 21Juni,2017 akihutubia wananchi kwenye viwanja vya Bwawani, Kibaha Mjini, Mwenyekiti wa CCM, ndugu John Magufuli alitumia fursa hiyo kumruhusu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama chake, ndugu Humphrey Polepole kumwingiza CCM mtu mmoja aliyesemwa kuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Pwani.

Kama Chama umekuwa msimamo wetu wa siku nyingi kutowajibu watu wanaohama Chama chetu au kuwapa mkazo mkubwa watu wanaohamia Chama chetu.

Tangu kuasisiwa kwa siasa za mageuzi hapa nchini, imekuwa ni kawaida kwa watu kutoka Chama kimoja kwenda kingine, Utitiri wa watu wamefanya hivyo kwa muda mrefu. Si jambo linalostaajabisha hata kidogo.

Lakini, leo tumelazimika kulitolea ufafanuzi tukio la Kibaha kwa sababu liligubikwa na uwongo wa dhahiri, hadaa, na propaganda za kitoto za Polepole.

 Mtu aliyesemwa kuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Pwani, Isihaka Juma Karanda,si tu kwamba mtu huyo si Mwenyekiti bali hana nafasi yeyote katika Kamati ya Uongozi ya Mkoa wa Pwani na si mwanachama kabisa wa Chama chetu.

Mwenyekiti Chama cha ACT Wazalendo, Mkoa wa Pwani ni Mimi hapa mbele yenu Mrisho Swagara. Katibu wangu ni ndugu Amina Batash. Kamati yetu ya uongozi ya Mkoa wa Pwani imeshangazwa sana na propaganda hizi za Polepole na chama chake, ambazo ziliendeshwa kwa kutumia kodi zetu wananchi.

Jambo hili la propaganda za kitoto za CCM   dhidi ya ACT Wazalendo ni mwendelezo wa harakati za Chama hicho kuwahadaa watanzania wasizungumzie hali mbaya ya chakula na usalama, pamoja na ugumu wa maisha, masuala ambayo chama chetu kimejikita katika kuyasemea.

Katika wakati ambao uchumi wa nchi unaanguka, hali mbaya ya usalama mkoani Pwani, kukiwa na mfumuko wa bei wa bidhaa wa kutisha, hasa vyakula, ingetarajiwa kuwa chama makini kingejikita kuisimamia Serikali yake irekebishe masuala hayo. Lakini kwa masikitiko kabisa CCM wamejikita kwenye propaganda za kitoto kabisa dhidi ya Chama pekee kinachosimamia mambo ya wananchi, chama cha ACT Wazalendo. Hili ni jambo la aibu sana.

Kwaniaba ya Chama changu, Viongozi wenzangu wa Mkoa wa Pwani, nawaasa Watanzania wenzangu wazipuuze propaganda hizo za CCM zinazofanywa kwa gharama kubwa ya kodi zetu.

 Ni muhimu Watanzania tuutumie muda huu kuhoji juu ya masuala muhimu yanayotugusa sisi wananchi, uhaba wa madawa hospitalini, hali ngumu ya maisha, kukosekana ajira kwa vijana, pamoja na kupanda kwa gharama za bidhaa kulikotokana na mfumuko mkubwa wa bei.

Uongo huo wa viongozi wa CCM unadhihirisha namna chama hicho kilivyo cha hovyo na kinavyoweza kufanya mambo ya hovyo kwa ajili ya kumfurahisha mwenyekiti wao

Kiusalama ni muhimu kwa wasaidizi wa Mwenyekiti wa CCM Kujiridhisha juu ya masuala mbali mbali yanayofikishwa mbele ya Rais ili wasimshushie hadhi kiongozi huyo wa nchi kwa ajili ya wachache kutaka sifa za kuonekana ni wachapakazi wanaokubaliwa katika maeneo yao.


Mrisho Swagara
Mwenyekiti wa Mkoa wa Pwani - ACT Wazalendo

Juni 22, 2017

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.