Friday, June 23, 2017

FANYA YAFUATAYO KUNOGESHA SIKUKUU YA EID-AL-FITR


Na Jumia Travel Tanzania

Ni siku chache zimebakia kabla ya waumini wa dini ya kiislamu nchini na duniani kote kumaliza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr. Zipo namna tofauti za kusherehekea sikukuu hii kulingana na sehemu watu walipo.

Jumia Travel ingependa kukushirikisha mambo yafuatayo ambayo yanaweza kuifanya sikukuu hii kuwa ya tofauti na kipekee tofauti na unavyosherehekea kila mwaka.   
 
Fanya maandalizi pamoja na familia. Katika kuhakikisha kwamba kila mtu anafurahia sikukuu basi ni vema ukawashirikisha kwenye maandalizi yake. Kama baba au mama wa familia na una watoto au ndugu unaishi nao litakuwa ni jambo zuri kama mtafanya hata kikao kidogo na kujadili. Kwa mfano, shughuli zote zitakazofanyika kipindi cha sikukuu, chakula kitakachopikwa, vinywaji, zawadi, wapi kwa kusherehekea, wageni gani wa kuwaalika, kupamba nyumba nakadhalika. Hii itasaidia siku hiyo ikifika kila mtu anafurahia na sio kufanya mambo ambayo yatakufurahisha wewe tu kuwaacha baadhi ya wengine kunung’unika.

Sherehekea pamoja na familia na majirani. Mara nyingi sikukuu hupendeza pale zinaposherehekewa kwa pamoja na ndugu na jamaa. Haijalishi familia uliyonayo ina ukubwa gani, kujumuika kwa pamoja kunaleta furaha na muunganiko zaidi miongoni mwa watu. Pia, hata kama una familia ndogo ni vema ukawashirikisha majirani zako. Unaweza ukapika chakula cha kutosha na ukaamua kuwaalika au kuwagawia lengo ni kuifanya iwe na shamrashamra zaidi.
 
Sherekea pamoja na watu wenye mahitaji maalum. Sio kila mtu huwa anapata fursa au kuwa na uwezo wa kusherehekea sikukuu. Na kwa sababu sikukuu ya Eid al-Fitr husherehekewa kwa siku mbili mpaka tatu (kwa sehemu zingine), unaweza ukapanga kwamba sikukuu ya moja au mbili ukasherehekea na familia yako na nyingine ukajumuika pamoja na watu wenye mahitaji maalumu kama vile watoto wa mitaani, watoto wa mitaani, wagonjwa mahospitalini, wazee, wafungwa na wengineo.

Wasimulie watoto kuhusu maisha ya Mtume na namna waislamu wa wakati walivyokuwa wakisherehekea sikukuu ya Eid-al-Fitr. Sio siku zote watoto wakishamaliza kupata chakula cha pamoja na familia wakaenda kutembea. Unaweza kuitumia siku hiyo kwa muda mchache tu ukawakusanya watoto na kuwasomea hadithi za Mtume Mohammad na namna waislamu wa kipindi hiko walikuwa wanasherehekea vipi sikukuu hii.  Hii itawafanya si tu kufurahia kwa kuwaongezea maarifa lakini pia kuelewa ni nini maana zaidi ya siku hii.
 
Safiri pamoja na familia. Unaweza ukaamua kusherehekea sikukuu hii kwa kusafiri mahali tofauti na nyumbani. Mnaweza kutumia gari binafsi kama usafiri, mkawa mnapumzika kwenye vituo kadhaa kwa ajili ya chakula na kuswali mpaka mkafika mahali muendapo.

Toa zawadi kwa ndugu, jamaa na marafiki. Kipindi cha Ramadhan mbali tu na kuwa ni kipindi cha kufanya toba na kumuomba Mwenyezi Mungu kukupunguzia dhambi zako lakini pia kutoa zawadi kunaweza kuwa ni njia mojawapo ya kukuongezea thawabu. Kutoa zawadi ni jambo jema kumfanyia mtu hususani unapolifanya kwa moyo mkunjufu. Basi kama utakuwa na uwezo unaweza kununua zawadi kadhaa na kuwapatia ndugu na majirani zako.

Badili muonekano wa nyumba yako. Itapendeza kama siku ya sikukuu mtaisherehekea kwenye nyumba yenye muonekano tofauti. Unaweza kufanya hivi kwa kushirikiana na familia yako ili kupata mwonekano utakaovutia. Mambo yanayoweza kubadili mwonekano wa zamani ni kama vile kupaka rangi mpya, kubadili samani za ndani, kununua mapambo, kufanya usafi au hata mpangilio wa vitu ndani ya nyumba.

Valia mavazi nadhifu. Tumezoea kwamba linapokuja suala la kuvaa nguo mpya siku za sikukuu huwa ni watoto pekee wanaopenda kufanya hivyo. Kwenye familia nyingi imekuwa ni kawaida wazazi kuweka kipaumbele kwa kuwanunulia watoto nguo mpya. Kutokana na desturi hiyo kuzoeleka miongoni mwa watu wengi, imewafanya watu wazima kupuuzia kuvaa nguo mpya kipindi cha sikukuu. Hiyo ni dhana na mawazo ya watu tu na wala isikufanye ujisikie vibaya kuvaa nguo mpya siku ya sikukuu. Unastahili kuutendea vema mwili wako kwa kuuvika na mavazi mapya na nadhifu siku hiyo, kama una uwezo lakini.   

Dhumuni la kukupatia dondoo hizi ni kuifanya sikukuu hiyo iwe na upekee tofauti na unavyosherehekea kila mwaka. Jaribu kufanya baadhi ya mambo hayo na utagundua utofauti mkubwa. Sio lazima ufanye yote yaliyoorodheshwa kwenye makala haya, machache tu yanatosha. Tofauti na hapo, Jumia Travel ingependa kukutakia maandalizi na mapumziko mema ya sikukuu ya Eid al-Fitr!

No comments: