Monday, June 5, 2017

Hotuba ya ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto katika Mazishi ya Mbunge Mstaafu na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro Mzee Philemon Ndesamburo Kiwelu

Tangulia Mbunge wa watu, Tangulia Jabari la Demokrasia yetu 
Ndugu Mwenyekiti Taifa CHADEMA, 
Ndugu Edward Lowasa, WM Mstaafu,
Ndugu Fredrick Tluwai Sumaye, WM Mstaafu, 
Ndugu Mashinji, Katibu Mkuu CHADEMA
Ndugu James Mbatia, Mwenyekiti Taifa NCCR-M,
Ndugu Severine Mwijage, Mwakilishi wa Chama cha CUF
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa 
Ndugu Wabunge, 
Mama Ndesamburo
Ndugu Lucy Owenya, pamoja na Kaka na wadogo zako wote, 
Ndugu wananchi wa Moshi Mjini,
Ndugu, Jamaa na Marafiki,
Ndugu zangu Watanzania,

Leo tuna shughuli maalumu, ya kumuaga mzee wetu, baba yetu, kiongozi mwenzetu, ndugu Philemon Ndesamburo Kiwelu.  Nami nimepewa nafasi niseme maneno machache juu ya muagwa wetu huyu.

Mzee Ndesamburo anayo mengi, lakini Tanzania itamkumbuka kama mtu aliyepambana kuboresha hali ya Demokrasia yetu na hali ya nchi yetu kwa ujumla. Yeye ni shujaa wa wote wanaoamini katika mfumo madhubuti wa vyama vingi nchini, akiwa ni Mwanasiasa aliyepanda na kubakia kileleni daima katika mapambano ya kidemokrasia.

Kwa maneno machache naweza kusema kuwa Mzee Ndesamburo ni taswira ya mkoa wake wa Kilimanjaro, Mwanamageuzi kindakindaki na pia Mbunge wa mioyo ya watu wa jimboni kwake, hapa Moshi mjini. Hakika Nchi yetu imepoteza mmoja wa majabari wa harakati za ujenzi wa Demokrasia. 

Umati huu uliopo leo hapa kwenye viwanja vya Majengo, manispaa ya Moshi, ni uthibitisho wa wazi juu ya mapenzi makubwa ambayo wananchi walikuwa nayo kwa Mzee Ndesamburo. 

Mzee Ndesamburo Ulikuwa Baba mlezi. Ulikuwa Mume mwema. Ulikuwa Babu na Kiongozi wa Umma. Leo sote tuna majonzi makubwa kwa kuondoka kwako, umeliunganisha Taifa na Manispaa ya Moshi katika ibada hii ya kukukumbuka ewe Mbunge wa Wananchi, Philemon Ndesamburo Kiwelu. 

Ulikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro na kwa muda mrefu mjumbe wa Kamati Kuu wa CHADEMA. Hakika wanachama wa Chama hiki wamepoteza jabari katika uimarishaji wa Chama. Hata hivyo hujaondoka tu bali umeacha 'legacy'. Legacy yako ni kuimarika madhubuti kabisa kwa Chama hicho mkoani mwako. Umeondoka kuwa kwa heshima na ni wajibu kwa wanaobakia kulinda heshima hiyo na kuiendeleza. 

Philemon Ndesamburo, uliipenda sana Kilimanjaro. Hukujali kuunganisha nguvu na yoyote, bila kujali itikadi za vyama vya siasa, linapokuja suala la Maendeleo ya mkoa wako. Nakumbuka siku moja Mwaka 2012, ulikusanya wabunge wote wa mkoa wa Kilimanjaro kufuatia Bajeti ya Mkoa kukatwa panga. Hukutaka kuona mkoa wako unabaguliwa na kuachwa nyuma Kwa sababu zozote zile. Nilijifunza jambo kubwa sana kutoka kwenye ujasiri ule wa mzee wetu. Mafunzo ambayo ninayatumia mpaka sasa. Ulifanya Yote haya kutilia nguvu umuhimu wa maendeleo ya mkoa wako.

Tuendeleze Jahazi.

Philemon Ndesamburo anakwenda kwenye nyumba yake ya milele akiongozwa na imani yake kubwa kwa Mungu na uzalendo wake usio na mawaa kwa nchi yake Tanzania. Angalau bado ataendelea kuwa nasi kwa kutuachia mafundisho makubwa kutokana na Maisha yake, mambo mema aliyoyafanya kwa nchi yetu, Kwa wanaMoshi, ndoto aliyoiishi ya Tanzania imara na yenye Demokrasia, heshima, na malezi kwa viongozi wengi vijana aliowafunda na kuwalea kiuongozi.

Ni dhahiri umeishi maisha yako Babu Ndesamburo Kama isemavyo biblia;

2 Timotheo 4:7 "Nimepigana Vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda". 

Tangulia Mbunge wa Watu wa Moshi. Tangulia Mzee Philemon Ndesamburo Kiwelu.

Mola akulaze pema.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Juni 5, 2017
Moshi Mjini
Kilimanjaro

No comments: