Tuesday, June 20, 2017

Kinondoni leo imezindua ukarabati wa barabara zenye urefu wa Kilomita 148

Wilaya ya Kinondoni leo imezindua ukarabati wa barabara zenye urefu wa Kilomita 148 ambazo zimeharibiwa na mvua zilizonyesha katika msimu uliopita hali iliyosababisha adha ya usumbufu na foleni kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi ameeleza hayo wakati akizindua matengenezo hayo na kumkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni ambaye pia ni mhandisi wa manispaa hiyo Abdul Digaga mitambo ya ujenzi wa barabara na lita 10,000 za dizeli.
Mafuta na mitambo hiyo inatokana na juhudi za Mkuu huyo wa Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na wadau wa kampuni za TOTAL TANZANIA na kampuni ya ujenzi GRAND TECH zilizotoa mitambo na mafuta ya dizeli kama sehemu ya mchango wao kwa DC Hapi kwa juhudi zake na za serikali ya awamu ya tano kwa ujumla katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Kinondoni.
Barabara zitakazofanyiwa ukarabati ni barabara zote korofi na zilizoharibiwa na mvua katika kata zote 20 za manispaa ya Kinondoni.
Aidha, DC Hapi ametembelea ujenzi wa barabara ya Nzasa KM 1.2 kwa kiwango cha lami unaofanywa na kampuni ya Esteem chini ya mradi wa Uboreshaji jiji la Dar es salaam (DMDP) ambapo chini ya mradi huo wilaya ya Kinondoni itanufaika na kiasi cha bilioni 22 huku Mfuko wa barabara ikiwa na bilioni 6 zilizoruhusiwa kutumika kukamilisha miradi iliyosimamishwa ya 2016/2017.
"Mbali na juhudi hizi za wadau waliojitolea kunisaidia mafuta na mitambo ya kutengenezea barabara, tunazo bilioni 6 za Mfuko wa barabara na tutanufaika na bilioni 22 za mradi wa Uboreshaji wa jiji la Dar es Salaam.Hivyo wananchi msiwe na wasiwasi, mwaka huu ujao wa fedha ni mwaka wa barabara kwa Kinondoni." Alisema Hapi.
DC Hapi aliwaomba wananchi waliojitokeza kuendelea kumuombea Rais Dr. John Magufuli na wasaidizi wake wote kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo nchini.
Uzinduzi wa ukarabati huo wa barabara umefanyika katika kata ya Kijitonyama na kuhudhuriwa na wananchi wa eneo hilo.

No comments: