Tuesday, June 20, 2017

WALEMAVU WAIANGUKIA SERIKALI

Mwenyekiti wa Chama cha watu wenye ulemavu kwa Mkoa wa Dar es Salaam Ahmad Abdallah Komboza ameiomba serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji kuwatengea vituo vya kushushia na kupakia abiria ili kuondoa sintofahamu baina yao na jeshi la polisi.
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa jeshi la polisi limekuwa likiwakamata kwa kosa la kutokuwa na vituo maalum vya abiria na kuwatoza kiasi kikubwa cha fedha mpaka kufikia elfu 90 jambo ambalo linawarudisha nyuma kimaendeleo.
Pia amelaani kitendo kilichotokea Juni 16 kwa jeshi la polisi kuzuia maandamano yao ya amani kwa madai ya kutokuwa halali kisheria na kudaiwa kuwapiga na kuwajeruhi baadhi ya walemavu wapatao 40 na kuwapeleka katika vituo vya polisi huku bajaji 76 zikikamatwa, hivyo ameomba walipwe fidia na jeshi la polisi liombe radhi kwa tukio hilo na iwe mwisho wa matukio hayo.
Huku akisisitiza kuwa walipanga kwenda kwa Mkurugenzi kusisitiza madai yao ya vituo vya abiria, ndipo polisi wakaja na kuzuia maandamano hayo.
Kwa upande wake Charles Temba Katibu wa Umoja wa Waendesha Bajiji Mkoa wa Dar es Salaam ameeleza kuwa suala la vituo vya abiria wametuma maombi kwa serikali tangu mwaka 20tano na waliainisha baadhi ya maeneo 20 ambayo walipendekeza yawe rasmi kwa waendesha bajaji walemavu ikiwemo Feri, Mnazi Mmoja, Upanga, Shule ya Uhuru lakini mpaka sasa hakuna kilichoshughulikiwa.
"Tulitoa mpaka nakala na kuziwasilisha ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Meya wa Jiji na Mkurugenzi ambapo tuliainisha mapendekezo ya vituo 20 vya abiria lakini mpaka sasa ombi letu halijashughulikiwa na tunazidi kutozwa kwa kosa la kutokuwa na vituo maalum vya kupaki abiria"
Katika hatua nyingine Mwendesha bajaji Fatuma Amrani Abdallah amelomba jeshi la polisi kutotumia nguvu kwa watu wenye ulemavu kwani wao ni kundi maalum linalohitaji kuangaliwa kwa upekee, vitendo vya kuwapiga na kuwatolea lugha chafu havifai , hivyo mamlaka husika inabidi ichukue hatua stahiki, kwani Tanzania ni nchi inayosifika kwa amani.

No comments: