TAARIFA KWA UMMA
MAAMUZI YA KIKAO CHA KAMATI YA UONGOZI JUU YA UENYEKITI WA CHAMA CHA ACT Wazalendo
Tarehe 3 Juni, 2017 Mwenyekiti wa chama chetu cha ACT Wazalendo, Mama Anna Elisha Mghwira aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Kufuatia uteuzi huu, Kamati ya Uongozi wa Chama ilikutana leo tarehe 7, Juni 2017 kutafakari juu ya matokeo ya uteuzi huu katika utekelezaji wa majukumu yake ya Uenyekiti na mustakabali wa siasa za Chama chetu na mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi nchini kwetu. Katika tafakari yake, Kamati ya Uongozi imezingatia yafuatayo:
- Kama Chama hatuna kipingamizi kwa Mama Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa, wala kumzuia ndugu Rais kumteua mtanzania yoyote na haswa mwana ACT Wazalendo kutumikia Taifa letu. ACT Wazalendo ni chama cha siasa na azma yake ni kutumikia Taifa.
- Kamati ya Uongozi inampongeza Rais kwa kuvunja miiko ya siasa za Tanzania kwa kuanza kuteua wapinzani katika utumishi wa umma. Uteuzi wa mara ya pili wa ndugu Rais kwa wanachama na viongozi wa ACT Wazalendo ni kielelezo kuwa chama chetu kinao watu makini na wanaofaa kuongoza. Ni uthibitisho kuwa ACT inapaswa kupewa nafasi ya kuongoza nchi katika uchaguzi ujao. Tunapenda kumhakikishia ndugu Rais kuwa tunao watu waadilifu na wazalendo wengine wengi ndani ya ACT kama jina la chama chetu linavyojipambanua yaani ACT- Wazalendo. Asichoke na asisite kuja kuvuna na wengine maana tumeonyesha uwezo wa kutengeneza wengi wa aina hiyo. Muhimu zaidi, Chama chake cha CCM kijifunze kutoka kwetu namna ya kuchagua na kuvutia viongozi waadilifu na wazalendo katika chama chao.
- Kamati ya Uongozi inashauri Rais au mamlaka yoyote ile ya uteuzi kuweka mfumo bora wa kuazima watu kutoka vyama vingine kumsaidia kazi za Maendeleo ya Nchi Kwa kufanya Mashauriano na Vyama husika ili kuepuka migongano isiyo ya lazima ndani ya vyama na katika jamii. Pamoja na kwamba Rais kama Mkuu wa Nchi anayo mamlaka ya kuteua yeyote amtakaye, lakini ni Afya na hekima teuzi hizo kufanywa kwa kushauriana na Viongozi wa Vyama husika ambavyo anachukua wanachama wake. Hii haitakuwa kuingilia mamlaka yake ya Kikatiba bali kuimarisha Umoja wa Kitaifa na hata Mfumo wa Vyama Vyama vingi nchini. Kuteua bila ya mashauriano kunaleta wasiwasi wa dhamira mbaya na kuathiri taswira ya vyama vya upinzani ambavyo Rais anachukua wanachama wake.
Kwa hiyo basi;
a. Kamati ya Uongozi imempongeza Mama Anna Elisha Mghwira Kwa kutambuliwa na hatimaye kuteuliwa na Rais kushika nafasi muhimu ya Mkuu wa Mkoa.
b. Kufuatia uteuzi wake kuwa Mkuu wa Mkoa, Kamati ya Uongozi imezingatia kuwa kutakuwa na mgongano wa moja kwa moja wa kiutendaji na kitaswira kati ya majukumu ya Uenyekiti wa chama na majukumu yake mapya, jambo linaloweza kuathiri Ufanisi wa moja wa nafasi hizi mbili.
c. Kwa mujibu wa Ibara ya 17(1)(iii) ya Katiba ya ACT Wazalendo na kutokana na mashauriano kati ya Mama Anna Mghwira na viongozi wenzake wakuu wa Chama, Mama Anna Mghwira amekoma kuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo. Ibara ya 17(1)(iii) ya Katiba ya ACT inamfanya Kiongozi wa Chama kukoma kushika nafasi yake iwapo atashindwa kutekeleza majukumu yake. Ni dhahiri kuwa kwa kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Mkoa, Mama Anna Mghwira hawezi tena kutekeleza kwa ufanisi wajibu huu.
d. ACT Wazalendo, inamshukuru Mama Mghwira kwa muda, mchango, nguvu, busara na hekima zake alizozitumia katika muda wote wa Uenyekiti wake, na tunamtakia kila la kheri katika kutumikia nafasi yake mpya.
e. Mwisho, Kamati ya Uongozi (Kwa mujibu wa Ibara za 29(24) ya Katiba ya ACT Wazalendo imemteua Ndugu Yeremia Kulwa Maganja kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Chama Taifa hadi uchaguzi Mkuu utapoitishwa Mwezi Machi 2018.
Ahsanteni Sana.
Samson Maingu Mwigamba
Kaimu Kiongozi wa Chama
Juni 7, 2017
Dar es salaam
Aliyekaimu nafasi yake--Yeremia Kulwa Maganja |
No comments:
Post a Comment