Monday, June 26, 2017

SHEIKH JALALA ALAANI VIKALI MAUAJI YANAYOENDELEA KIBITI MKOANI PWANI..

Sheikh Mkuu wa Dhehebu SHIA Ithna Shariya Hemed Jalala amewaomba viongozi wa dini nchini kuungana kwa pamoja bila kujali itikadi zao za kimadhehebu na kukemea, kutoa elimu ya kuwaelimisha umma juu ya mauaji yanayoendelea Mkoa wa Pwani katika wilaya za Kibiti na Mkuranga.
Sheikh Jalala ameyasema hayo leo katika swala ya Eid iliyoswaliwa katika msikiti wa AL GHADIR uliopo Kigogo wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Sheikh Jalala ameeleza kuwa yanayoendelea Kibiti yanalitia aibu taifa kwani siyo utamaduni wa watanzania hivyo viongozi wa dini wanafursa kubwa ya kunasihi waumini wao ili yanaendelea yafikie ukomo.
Sheikh Jalala amesema akili inapowekwa kando katika kufanya maamuzi ya mambo mbalimbali kunahatari kubwa inaweza kulikumba taifa ikiwemo kutokuwepo kwa maamuzi yenye busara na hekima ambayo hupelekea taifa katika vitendo vya kikatili na ugaidi.
Huku akitolea mfano kwa yanayoendelea nchini Palestina kuwa ni kuiweka akili kando kwani akili ikiwekwa kando mambo yote yanafanyika kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu.
Hivyo amewasihi waislamu wafanye matendo yao kwa kuzingatia akili, kwani kwa kufanya hivyo kutapelekea kutokubaguana kwa dini, kabila na kupelekea kuwa na Taifa bora lenye kuhurumiana na kusaidiana.

No comments: