Friday, June 2, 2017

TAIFA STARS: MWENDO WA DAKIKA 1,500 KWA SIKU 8

Mshambuliaji wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbaraka Yussuf Abeid (katikati) ‘anaposepa’ na kijiji yaani kuhama au kuondoka na idadi kubwa ya watu/mabeki waliomzunguka wakiwamo Salum Mbonde, Shomari Kapombe na Kiungo Aboubakar Salum katika mazoezi ya timu yanayofanyika Uwanja wa mazoezi wa Kituo cha michezo cha Tolip (Tolip Sports City) hapa Alexandria, Misri. Taifa Stars  inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti kutoka Kampuni ya Bia ya SBL inajiandaa kucheza na Lesotho Juni 10, 2017 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon. Picha na Alfred Lucas wa TFF.

Mpaka leo asubuhi Juni 2, mwaka huu, Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga pamoja na wenzake katika benchi la ufundi, wamekinoa kikosi hicho kwa dakika 420 ndani ya Uwanja wa mazoezi wa Kituo cha michezo cha Tolip yaani Tolip Sports City hapa Alexandria, Misri.

Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mayanga, Taifa Stars  inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti kutoka Kampuni ya Bia ya SBL itafanya mazoezi yasiyopungua dakika 1,500 katika kambi iliyoanza Mei 31, 2017 usiku na kufikia kikomo Juni 7, mwaka.

Siku ya kwanza ya kambi Mei 31, mwaka huu Kocha Mayanga alianza na dakika 120 za mwanzo baada ya kusafiri salama kutoka Tanzania hadi hapa Misri.

Kila siku Taifa Stars ina programu mbili ambako asubuhi timu inafundishwa kwa dakika 90 uwanjani kwa mazoezi mbalimbali na kwa programu ya usiku ni dakika 120 ambako huanza saa 3.00 (saa 2100) usiku na kumaliza saa 5.00 (saa 2300) usiku kwa saa za hapa Misri.

Kwa msingi huo, Kocha Mayanga kwa kusaidiana na benchi lake la ufiundi, anakionoa kikosi hicho kwa takribani saa 25 kwa wiki, kabla ya kurejea nyumbani. Timu itarudi Tanzania usiku wa kuamkia Juni 8, mwaka huu.

Ikiwa nyumbani Tanzania, Mayanga atawanoa tena kwa dakika nyingine 180 tayari kabisa kuivaa Lesotho Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mchezo huo umepangwa kuanza saa 2.00 usiku.

Mchezo dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.

Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.

Akizungumza mwenendo wa mazoezi kwa saa 300 za mwanzo, Kocha Mayanga amesema: “Nafarajika vijana wangu wameendelea kufunguka. Hapa hawana usumbufu wo wote, ni mazoezi na kupumzika kulingana na ratiba na chakula.”

Mazoezi ya Mayanga hayathiri maendeleo ya mwili wa binadamu kadhalika nguzo ya funga kwa wale ambao wako kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwani ratiba huonyesha huanza kunolewa kuanzia saa 12.00 alfajiri - saa mbili baadaye baada ya daku (Uhudumiwa daku kabla ya saa 11.00 alfajiri), lakini pia saa 3.00 usiku ikiwa ni saa mbili baada ya kufuturu (Futari ni saa 12.45 jioni).

Ikiwa hapa kambini, timu hupata huduma zote kwa upande wa chakula na wachezaji wana faraja ya kizalendo kuitumikia timu yao ambayo ina mtihani dhidi ya Lesotho wakijenga imani kabisa kwamba watafanikiwa.


Maelezo ya picha/captions.


……………………………………………………………………..……………..……
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments: