Tuesday, July 4, 2017

MANJI AWASILISHA MAOMBI MAHAKAMA KUU YA KUACHIWA KWA KUWA WAMEKAMATWA ISIVYO HALALI

Mfanyabiashara maarufu na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga Yusuf Manjina wenzake wawili wamefungua kwa hati ya dharura maombi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya DSM wakiomba waachiwe kwa sababu wamekamatwa isivyo halali.

Mbali na Yusuf Manji katika maombi hayo yaliyowasilishwa jana July 4, 2017 na kupangiwa mbele ya Jaji Lugano Mwandambo, walalamikaji wengine ni Deogratius Kisinda na Thobias Fwere ambapo wamefungua maombi hayo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, IGP Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi Kanda ya DSM.
Kwa mujibu hati ya kiapo ambayo imewasilishwa na Wakili Gudson Ndusyepo, Manji na wenzake wanaiomba Mahakama Kuu iwaachie kutokana na kukamatwa isivyo halali huku wakiiomba Mahakama hiyo kutoa amri ya kuwataka walalamikiwa wawafikishe Mahakamani ili washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
Katika hati hiyo, Wakili Ndusyepo amebainisha kuwa Manji na wenzake walikamatwa nyakati tofauti tofauti ambapo mlalamikaji Kisinda alikamatwa June 30, 2017 saa 10 jioni wakati Manji na Fwere walimatwa July 1, 2017 saa 5 asubuhi katika Jengo la Quality Center Barabara ya Pugu, DSM.
Manji na wenzake walikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na sare za Jeshi katika ghala laQuality Motors Group ambapo kupitia hati hiyo ya kiapo, Wakili Ndusyepo amebainisha kuwa kukamatwa kwa walalamikaji sio halali kwa sababu kosa linalodaiwa dhidi yao linahusiana na masuala ya Kampuni ya Quality Motors ambayo inaongozwa na Wakurugenzi wake na Manji.
Mara baada ya kukamatwa kwa walalamikaji hao waliombewa dhamana lakini ilikataliwa kwa sababu zisizojulikana:>>>”Kama Wakili wa waombaji nimefuatilia suala la dhamana hadi sasa saa 48 zimeshapita tangu walipokamatwa, lakini hawajafikishwa Mahakamani. Jambo hilo ni kinyume na sheria.” – Wakili Ndusyebo.

No comments: