Tuesday, July 18, 2017

WAZIRI KIGWANGALLAH ATOA MAELEZO KUHUSU DAWA MPYA YA UKIMWI


BAADA ya hivi karibuni dawa mpya ya kupambana na Virusi Vya UKimwi kugundulika na kuanza kutumika nchini Kenya, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini imefunguka, Uwazi lina habari kamili.
Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Nsachris Mwamwaja alisema wao kama wizara wanafurahi kusikia dawa imepatikana lakini akafafanua kwamba bado haijaingia Tanzania.

Aliongeza kuwa kama dawa hiyo itapitia taratibu zote za usajili, wizara haina tatizo wala kipingamizi.
“Kwa sasa bado haijaingia Tanzania ila ikiingia tu tutawajuza wananchi ila lazima ipitie taratibu zetu za usajili baada ya hapo ndipo ianze kutumika,” alisema Mwamwaja.

Baadhi ya wananchi nchini walionesha kufurahishwa na ujio wa dawa hiyo nchini Kenya wakiwa na imani kwamba zitaingia nchini na kusaidia waathirika wa Ukimwi.

                                   

Dawa hiyo imeifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kutumia vidonge vya ugonjwa wa Ukimwi ambavyo vinaweza kuboresha afya na kurefusha maisha ya maelfu ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa nyemelezi ambayo hayakubali tiba nyingine.Jina la dawa hiyo kitaalamu ni Dolutegravir (DTG), lakini itajulikana kama Tivicay.

Imeelezwa kwamba, dawa hiyo imekuwa chaguo la kwanza la watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa miaka miwili iliyopita katika nchi za watu wenye kipato kikubwa kwa kuwa ina athari chache, ni rahisi kutumia kuliko dawa za ARV zinazotumika sasa (yaani kidonge kimoja kidogo kila siku).

Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza DTG iwe chaguo la kwanza kwa watu wazima na vijana, lakini hadi siku za karibuni watu wanaoishi na VVU katika nchi kama Kenya walikuwa hawawezi kupata dawa hizo.

Vidonge hivyo, ambavyo vilipitishwa kutumika nchini Marekani mwaka 2013, sasa vinagawiwa kwa wagonjwa 20,000 nchini Kenya kabla ya kupelekwa Nigeria na baadaye Uganda, kwa kusaidiwa na UNITAID, ambao ni wakala wa afya duniani.

DTG ni dawa inayotumiwa na watu wenye VVU ambao hawakuwahi kutumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi ARV.

Dk. Peter Kimuu, mkuu wa idara ya sera za afya na mipango katika Wizara ya Afya Kenya, aliwahi kusema dawa hiyo haina madhara mengi kwa wagonjwa wanaoaishi na HIV na haina hatari ya dawa kuwa sugu.

Alisema DTG ni nzuri kwa vile ina madhara madogo sana kulinganisha na dawa nyinginezo.

UNITAID, mshirika wa mpango huo, imetoa karibu chupa 148,000 za DTG kwa Wizara ya Afya ya Kenya ambayo itaweza kuwafikia asilimia moja tu ya watu wanaoishi na HIV nchini humo.

GLOBAL PUBLISHERS

No comments: