Friday, August 11, 2017

UMMY MWALIMU ATANGAZA WASHINDI WA SHINDANO LA AFYA NA USAFI WA MAZINGIRA ‘NIPO TAYARI’

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mapema leo Agosti 11, 2017, imetangaza matokeo ya washindi wa shindano la Afya na usafi wa Mazingira kwa mwaka 2017, iliyokuwa na kauli mbiu ‘Nipo Tayari’.

Akitangaza washindi hao mapema leo katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya, Jijini Dar es Salaam Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu amepongeza wadau mbalimbali kwa kuweza kufanikisha zoezi hilo zikiwemo Halmashauri zote zilizoshiriki. “Mashindano ya afya na usafi wa mazingira kwa mwaka huu 2017 hapa nchini yaliweza kushirikisha Halmashauri zote zaidi ya 185 huku, Halmashauri 73 zikishindanishwa Kitaifa baada ya mchujo ngazi ya Mkoa. Mchanganuo wa Halmashauri hizi ni; Majiji Manne, Manispaa 21, Miji 21 na Halmashauri za Wilaya 27. 

Kila mwaka, Wizara yetu imekuwa ikiratibu mashindano haya Kitaifa nchini kote ikiwa na lengo la kuinua hali ya afya na usafi wa mazingira katika ngazi ya Kaya na taasisi ili kulinda na kuboresha afya ya jamii.” Amesema Waziri Ummy Mwalimu. Waziri Ummy Mwalimu amewatangaza washindi wa kwa upande wa Halmashauri za Majiji na Manispaa ambapo Manispaa ya Moshi ikiibuka kidedea kwa kupata asilimia 78.5, mshindi wa Pili, Jiji la Arusha, Asilimia 78.1 na mshindi wa tatu, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Asilimia 67.2. Kwa upande Halmashauri za Miji, mshindi wa kwanza ameibuka Halmashauri ya Mji wa Njombe huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Halmashauri ya Mji wa Kahama na mshindi wa tatu ni Halmashauri ya Mji wa Tunduma. 

Washindi wa Halmashauri bora inayotekeleza kwa ufanisi Kampeni hiyo hususani katika ujenzi na matumizi ya vyoo bora, mshindi wa kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya Meru, kwa mshindi wa Pii imechukuliwa na Wilaya ya Njombe huku wa tatu ni Halmashauri ya Wilaya ya Makete. Waziri Ummy Mwalimu amewatangaza washindi wa Kijiji bora kinachotekeleza kwa ufanisi hiyo ya usafi ni Kijiji cha Kanikelele kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mshindi wa pili, Kijiji cha Nambala kutoka Halmashauri ya wilaya ya Meru, na cha tatu ni Kijiji cha Lyalalo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. 

Aidha Vijiji hivyo viliweza kupatikana baada ya kushirikisha jumla ya Vijiji na Mitaa 80 huku Kaya zake zikiwa zimefanikiwa kujenga na kutumia vyoo bora pamoja na sehemu za kunawia mikono kwa maji na sabuni. Washindi wengine wa shindano hilo ni pamoja na Hospitali Bora kwa usafi ambapo Mshindi wa kwanza ni Arusha Lutheran Medical Centre, mshindi wa pili, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisco na Ifakara – Morogoro na wa tatu, Hospitali ya Rufaa Mount Meru. Aidha, Waziri Ummy Mwalimu amewatangaza washindi kwa upande wa Hoteli, ambapo Hyatt Regency Dar es Salaam the Kilimanjaro, iliibuka mshindi wa kwanza huku wa pili ikienda Mount Meru Hotel, Arusha na ya tatu ni Aden Palace Mwanza. “Wizara itatoa zawadi ya gari la kubebea taka (trekta lenye tela) kwa Halmashauri ya Mji wa Njombe ambayo imeibuka mshindi wa kwanza kundi la Miji.

Aidha zawadi ya gari mpya aina ya Nissan itatolewa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru ambayo ilishika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira, na zawadi za pikipiki aina ya YAMAHA kwa washindi wote waliosalia ili kutoa motisha kwa mabwana Afya wote. Pia zawadi nyingine zitakazotolewa kwa washiriki katika makundi yote ni pamoja Vikombe na Vyeti maalum ambapo Wizara tutaandaa siku maalum kwa ajili ya kukabidhi zawadi hizo na tunawapongeza kwa ushindi” alimalizia Waziri Ummy Mwalimu. Katika kuongeza ufanisi wa mashindano hayo, Wizara iliunda kamati maalum ambayo iliratibu na kusimamia zoezi zima la uhakiki wa Mashindano huku wajumbe wakitoka Taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais– TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi - Muhimbili, Chuo Kikuu cha Ardhi, pamoja na wadau wa Maendeleo wanaojihusisha na shughuli za Afya na usafi wa Mazingira hapa nchini huku wakizingatia vigezo hali bora ya usafi wa mazingira kwa ujumla.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa Habari katika mkutano wa tukio hilo Jijini Dar es Salaam, la kutangaza washindi wa shindano la Afya na usafi wa Mazingira kwa mwaka 2017, iliyokuwa na kauli mbiu ‘Nipo Tayari’.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa Habari katika mkutano wa tukio hilo Jijini Dar es Salaam, la kutangaza washindi wa shindano la Afya na usafi wa Mazingira kwa mwaka 2017, iliyokuwa na kauli mbiu ‘Nipo Tayari’. Kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Usafi wa Mazingira, Theophil Likangaga.
Mratibu wa kampeni ya mashindano hayo ya Usafi wa Afya ya Mazingira, Bw. Anyitike Mwakitalima akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa tukio hilo. Anayemfuatia ni Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalumu na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Usafi wa Mazingira, Theophil Likangaga
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akiwa na nembo ya kampeni ya NIPO TAYARI ambayo inahamasisha usafi wa mazingira hasa usafi wa kunawa mikono na matumizi sahihi ya vyoo.
Mwanahabari wa mtandao wa Michuzi Media, Chalila Chibuda akiwa na nembo ya NIPO TAYARI
Mwanahabari wa Tumaini TV akiwa na nembo ya NIPO TAYARI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akiwa pamoja na baadhi ya wadau wa Wizara ya Afya katika habari na nembo hiyo ya NIPO TAYARI
Mratibu wa kampeni ya mashindano hayo ya Usafi wa Afya ya Mazingira, Bw. Anyitike Mwakitalima akiwa na nembo ya NIPO TAYARI
Wadau mbalimbali wakiwa wamebeba nembo ya NIPO TAYARI
Wadau mbalimbali wakivalishwa nembo maalum ya NIPO TAYARI kwa ajili ya kuhamasisha Afya ya Mazingira ikiwemo usafi wa mikono na vyoo bora vya kisasa
Wadau mbalimbali wakivalishwa nembo maalum ya NIPO TAYARI kwa ajili ya kuhamasisha Afya ya Mazingira ikiwemo usafi wa mikono na vyoo bora vya kisasa

No comments: