Saturday, September 16, 2017

MATAMSHI YA ULEVI WA MADARAKA YA SPIKA NDUGAI DHIDI YA MBUNGE ZITTO KABWE HAYAWEZI KUKUBALIKA

SIKU ya tarehe  13 Septemba, 2017 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  umma ulishuhudia na kusikia matamshi ya fedheha yaliyotolewa na Spika wa Bunge hilo ndugu Job Yustino Ndugai. Spika Ndugai alisikika akisema; ‘’………Zitto utapambana na Spika kweli!? Naweza  kukupiga marufuku kuongea humu mpaka miaka yako yote ikaisha na hakuna pa kwenda. Hakuna cha swali, hakuna cha nyongeza, hakuna cha kuongea chochote humu ndani ya Bunge... utanifanya nini?! Pambana na kitu ingine, siyo Ndugai.’’ mwisho wa kunukuu.

Matamshi hayo ya Spika Ndugai yalikuwa yakimlenga Mbunge wa Kigoma mjini ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Ndugu Zitto Kabwe. Spika Ndugai alikwenda mbali zaidi ya matamshi makali dhidi ya Zitto Kabwe, ambapo aliiagiza Kamati ya Maadili ya Bunge imuite na kumuhoji mbunge Zitto Kabwe kwa kile alichodai  kuwa ameudhalilisha mhimili wa Bunge. 

Pamoja na kwamba Spika Ndugai hakufafanua kwa kina chanzo na sababu za tuhuma zake kwa ndugu Zitto, tunashawishika kuamini kuwa chanzo cha hamaki ya Spika kwa Zitto ni ukosoaji na maoni mbalimbali juu ya mwenendo mbovu wa Bunge la Jamhuri, yaliyokuwa yakitolewa na ndugu Zitto kupitia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii. 

Ni ukweli ulio bayana kuwa, katika uhai wa Bunge hili la 11 chini ya uongozi wa Spika Ndugai, Mhimili wa Bunge umewekwa katika mateka ya serikali na Spika Ndugai kama kiongozi wa Bunge ameruhusu udhaifu huo. Rekodi na mlolongo wa matukio mbalimbali katika awamu ya Bunge hili inathibitisha ukweli huo. Fedheha ya hivi karibuni, inayothibitisha Bunge kuburuzwa na Serikali, ni kitendo cha Ripoti mbili za kibunge za Uchunguzi wa biashara ya Madini ya Almasi na Tanzanite kushindwa kuwasilishwa na kusomwa Bungeni ili Bunge litoe maazimio kwa serikali kama yalivyo matakwa ya Kanuni na utamaduni wa mabunge. 

Badala yake Spika Ndugai aliutelekeza ukumbi wa Bunge akabeba ripoti zote mbili  akaongozana na Kamati teule kwenda Ikulu Dar es salaam ili kupata maelekezo ya Rais! Vitendo vya namna hii ndivyo vinavyodhalilisha hadhi na nafasi ya Bunge letu kikatiba, na siyo tweet za Zitto Kabwe zinazogonga kengele ya tahadhari juu ya kupoteza mwelekeo kwa Bunge kama chombo cha wananchi. 

Hali hii ya uendeshaji wa Bunge kwa namna ya ajabu inayolidhoofisha Bunge kama chombo imara cha uwakilishi wa wananchi na usimamizi wa uwajibikaji wa serikali, ndio inayokosolewa na kulalamikiwa na wengi, akiwemo ndugu Zitto Kabwe. Tulitarajia kuona Spika Ndugai kusikiliza na kuchukua changamoto hizo kwa manufaa ya kurejesha nafasi na heshima ya Bunge ili kufikia dhana ya uwajibikaji wa serikali kwa wananchi, badala yake amegeuka mbogo dhidi ya wakosoaji.

Ieleweke kwamba Bunge haliendeshwi kwa mujibu wa matakwa na utashi binafsi wa Kiongozi wa Bunge. Bali linaendeshwa kwa kufuata na kuzingatia Kanuni za kudumu za Bunge. Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za kudumu za Bunge toleo la mwaka 2016, inaelekeza msingi wa mamlaka ya Spika katika kutekeleza majukumu yake kama yalivyotolewa na Katiba ya nchi kuwa ataongozwa na Kanuni za Bunge, Sheria za Nchi na Mila na Desturi za mabunge yenye kufanana na Bunge la Tanzania. Aidha, Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Bunge, inamwekea miiko ya kiapo Spika kuendesha Bunge na shughuli za Bunge kwa haki bila upendeleo. Pia Kanuni hiyo inamtaka atoe maamuzi kwa uadilifu bila chuki wala upendeleo wowote.
  
Chama cha ACT Wazalendo kinapenda kuelezea masikitiko yake makubwa kufuatia matamshi hayo yasiyokubalika. Chama kinalaani kwa nguvu zote majaribio yoyote ya uendeshaji wa Bunge kwa vitisho na udikteta unaoonekana kuota mizizi chini ya uongozi wa  Spika Ndugai. Tunamkumbusha Spika Ndugai kuendesha Bunge kwa njia za kiungwana, ustaarabu, demokrasia, busara na hekima kwa kuzingatia Kanuni za Bunge, Sheria na Katiba ya nchi.

Matamshi yaliyotolewa na Spika Ndugai si tu kuwa hayana msingi wa kisheria na kikanuni katika taratibu za uendeshaji wa Bunge, lakini pia yanakosa hekima, busara na ustahimilivu wa kiuongozi. Ni matamshi yaliyojaa ubabe, kibri na jeuri ya ulevi wa madaraka jambo ambalo ni kinyume na utamaduni wa uongozi bora wa kidemokrasia tunaojaribu kuujenga katika nchi yetu na kuwarithisha vizazi vijavyo.

Chama chetu kitaendelea kutoa wito na kuwahamasisha watanzania kupinga vikali hali na mwenendo wowote wa ujenzi wa uimla katika uendeshaji wa Bunge na mihimili mingine ya dola. Aidha, tunapenda kumtia moyo mbunge na Kiongozi wetu wa Chama kutorudi nyuma katika jitihada hizi njema za kuliepusha Bunge na mateka ya serikali. Bunge lililokamatwa na serikali, ni Bunge kibogoyo lisiloweza kuing’ata wala kuitishia serikali ili itii na kutekeleza ushauri na maagizo ya wawakilishi wa wananchi. Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa mbunge wake, kamwe hakitakubaliana na usaliti huo kwa umma wa watanzania.

Janeth Rithe,
Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa,
ACT Wazalendo.
Imetolewa leo tarehe 16 Septemba, 2017

No comments: